Zuchu vs Nandy ni bonge la ligi

New Content Item (1)
New Content Item (1)

KITENDO cha Nandy kumtambulisha msanii mpya na wa kwanza katika lebo yake, The Africa Princess ni uchokozi wa makusudi kabisa kwa Zuchu ambaye amekuwa mshindani wake mkubwa katika Bongofleva miaka ya hivi karibuni.

Januari 20 Nandy alimkaribisha Yammi katika familia ya The Africa Princess akiwa mkononi na EP yake 'Three Hearts' yenye nyimbo tatu ambazo hajamshirikisha msanii yeyote.
Siku moja moja baada ya tukio hilo, Zuchu kutokea WCB Wasafi akatangaza kuwa Januari 27 atakuwa na jambo lake bila kuweka wazi ni kipi hasa atakuja nacho!.
Hata hivyo, hisia za wengi ni kuwa huwenda Zuchu akajibu mashambulizi hayo kufuatia uchokozi wa Nandy kwa kumtambulisha Yammia ambaye anaimba miondoko ya Baibuda sawa na Zuchu!.

Zuchu aliwahi kuiambia Wasafi FM kuwa anachojivunia katika muziki wake ni 'tone' yake ya Baibuda, anaamini hii ndio slaa yake inayomtofautisha na wasanii wengine wa kike, na ndicho kilimchomvutia Diamond hadi kumsaini WCB Wasafi.

Hivyo Nandy amejua ulipo uimara wa Zuchu na ameamua kuelekeza mashambulizi yake eneo hilo, huu ni mtego mwingine kwa Zuchu; ashindane na Yammi upande wa Baibuda au ashindane na Nandy kimuziki kama ilivyokuwa hapo awali.

Lakini huwenda Zuchu akaachia wimbo wake mpya ila wenye mahadhi ya Baibuda maana amekuwa na utamaduni wa kufanya hivyo kila Januari ya kila mwaka.
Januari 20, 2021 Zuchu aliachia wimbo wake 'Sukari' ukiwa umetayarishwa na Maprodyuza wawili; Trone na Lizer Classic, Januari 21, 2022 akaachia wimbo wake 'Mwambieni' uliotengenezwa na Prodyuza Mr. LG.

Je, ni kwa namna gani hasa Zuchu na Nandy wamekuwa na ushindani katika muziki wa Bongofleva?, makala haya yanaenda kuangazia vipengele vichache kwa wasanii hao;
Hadi sasa Nandy tayari ana albamu mmoja, The African Princess iliyotoka Novemba 2018 chini ya Epic Records, pia ana EP tatu; Wanibariki (2020), Taste (2021) na Maturity (2022), ila Zuchu hana albamu, bali ana EP moja, I Am Zuchu (2020).
Zuchu ndiye msanii wa kwanza wa kike Tanzania na Afrika Mashariki kuweza kufikisha 'views' milioni 100 YouTube ambapo sasa amefikia milioni 431.0, baada ya mwezi mmoja, Nandy naye akafanya hivyo akiwa msanii wa pili na sasa amefikisha milioni 173.5.

Na ikumbukwe hadi sasa hawa ndio wasanii pekee wa kike Afrika Mashariki wenye 'subscribers' zaidi ya milioni 1 YouTube.
Nandy alifanya vizuri katika shindano la kwanza la karaoke barani Afrika, Tecno Own The Stage nchini Nigeria aliposhika nafasi ya pili na kuondoka na Tsh36 milioni, huku Zuchu akishindwa kufua dafu kwenye shindano hilo na kutoka hatua za awali.

Mama mzazi wa Zuchu ni Khadija Kopa ambaye ni Malkia wa muziki wa Taarabu nchini Tanzania, huku Baba mzazi na Nandy, Charles Mfinanga akiwa amewahi kuwa DJ.
Nandy anajisimamia mwenyewe kimuziki kupitia Lebo yake, The African Princess ambayo imeanza kusaini wasanii huku ikiwa na ushirikiano emPAWA ya Patoranking wa Nigeria, ila Zuchu anasimamiwa na WCB Wasafi ambayo ni Lebo ya Diamond Platnumz.

Zuchu ni shabiki wa Simba SC na amewahi kutumbuiza kwenye tamasha la timu hiyo 'Simba Day' mara mbili, huku Nandy akiwa ni shabiki wa Yanga SC na amewahi kutumbuiza kwenye tamasha la timu hiyo 'Siku ya Mwananchi' mara moja.
Kwa misimu zaidi ya minne, Nandy amekuwa akiendesha tamasha lake la 'Nandy Festival' kwa mafanikio, ila Zuchu hana tamasha lake binafsi zaidi ya kutumbuiza Wasafi Festival.
Wasanii wa kimataifa waliofanya kolabo na Nandy ni Willy Paul (Kenya,) Joeboy, Mr Eazi na Oxlade (Nigeria) na Koffi Olomide (DR Congo), huku Zuchu akiwa na Joeboy, Olakira na Adekunle Gold (Nigeria), Spice Diana (Uganda), Bontle Smith na Tyler ICU (Afrika Kusini).

Hadi sasa hawa ndio wasanii waliobahatika kupigiwa simu na Rais wa Tanzania, Samia Suluhu wakiwa katika shoo zao, Nandy aliipokea simu ya Rais akiwa Dodoma katika Nandy Festival, huku Zuchu akiipokea akiwa Zanzibar katika Home Coming Show.
Nandy ameshinda tuzo nyingi kubwa za ndani na kimataifa kuliko Zuchu, ameshinda AFRIMA (2017 & 2020) - Nigeria, AFRIMMA (2020) - Marekani, AEAUSA (2020) - Marekani na Maranatha Awards (2018) - Kenya, huku Zuchu akiwa na mbili za kimataifa, AFRIMMA (2020 & 2022) - Marekani.

Katika tuzo za muziki Tanzania (TMA) 2021 ambazo WCB Wasafi walisusia, Nandy alijizolewa nne akiwa ndiye msanii wa kike aliyeshinda tuzo nyingi zaidi.

Alishinda vipengele vya Mwanamuziki Bora wa Kike wa Mwaka Bongofleva, Mwanamuzi Bora wa Kike wa Mwaka na Mwanamuzi Bora Chagua la Mashabiki Kwenye Mitandao ya Kijamii - Mwanamke, huku wimbo wa Darassa 'Loyalty' aliyoshirikishwa ukishinda kama Wimbo Bora wa Kushirikiana.