Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Zaiid: Aah wapi! Tafuta Bwana una maana tatu

Muktasari:

  • Katika mahojiano na Mwanaspoti, Zaiid anasema tangu aanze kufanya muziki wimbo wa Tafuta Bwana umemuongezea namba za watu na umepokewa kwa ukubwa ndani ya wiki mbili tofauti na Wowowo ambao ulichukua miezi miezi mitatu kusikika kila kona.

MSANII wa Hip Hop, Abdullah Jamal Mnete 'Zaiid' ambaye kwa sasa anatamba na wimbo mpya wa Tafuta Bwana amezungumzia namna ulivyompa matokeo ya haraka kutokana na mapokeo ya mashabiki wake.

Katika mahojiano na Mwanaspoti, Zaiid anasema tangu aanze kufanya muziki wimbo wa Tafuta Bwana umemuongezea namba za watu na umepokewa kwa ukubwa ndani ya wiki mbili tofauti na Wowowo ambao ulichukua miezi miezi mitatu kusikika kila kona.

"Sina namba kubwa mitandaoni, ila nikiposti wimbo huo napata watu wengi umevunja rekodi kwa mapokeo na unafanyiwa chalenji na watu kutoka Kenya, Uganda na Tanzania ila wamechukua kwa 'engo' moja ya wanawake.

"Una engo tatu nyingine ni watu wamrejee Bwana Mungu na wanaume watafute pesa umri wao unasonga mbele," anasema Zaiid anayefafanua jina hilo ni kifupi cha jina Zaidi.


WOWOWO ILITOKANA NA RIHANNA

Zaiid anasema mara nyingi anafanya nyimbo kwa kuangalia midundo ya wasanii wa nje ambayo awali washikaji zake walikuwa wanachukulia poa kulingana na aina ya muziki anaoufanya.

"Baada ya kuusikia wimbo wa Rihanna wa Work nilipata wazo la kuandika wimbo wa Wowowo ambalo ni neno la kizamani lilikuwa linatumika na kaka zetu tukiwa wadogo akipita binti mwenye makalio makubwa wanaita wowowo," anasema Zaiid.

"Wimbo huo umepitiwa na maproduzya wengi hadi kufikia hatua ya kuuachia. Unaishi hadi leo kutokana na aina ya maisha wanayoishi wadada wengi wa mjini kutengeneza shepu zao na wengi wanadhani labda ni aina ya maisha yangu. Mimi napenda wasichana wenye maumbo ya kawaida, wazuri na wenye akili kubwa kichwani."

Anasema wimbo huo ndiyo ulimtambulisha kwa jamii na ulimsaidia kujifunza gemu la rapu. "Ukiacha kizazi cha kina Profesa Jay, Albert Mangwea (marehemu), Afande Sele ambao miziki yao ilikuwa inavuka hadi vijijini tofauti na sasa asilimia kubwa wanaimbiwa watu wa mjini, ila Wowowo ilipenya chochoro kwa chochoro kijiji kwa kijijni."


PISI KALI

Msanii huyo anasema wimbo wa Pisi Kali unawakumbusha wanaume kusikika katika jamii kwa sura za kimamlaka na kupunguza tabia za kufanya vitu vya hovyo katika mitandao ya kijamii inayopoteza thamani zao.

"Wimbo wa Pisi Kali ni kombinesheni yangu na P Mawenge. Ni kati ya nyimbo zilizopo katika albamu yetu ambayo hatujaiachilia. Nilipata wazo hilo kutokana na kuchangamka kwa mitandao ya kijamii kuona wanaume wanakuwa soft tofauti na baba au mababu zetu walikuwa wafalme (king), na ili upate sifa hizo ilitokana na misimamo na mitazamo yao kwa ajili ya jamii inayowazunguka," anasema Zaiid.

"Vijana wa kizazi hiki asilimia kubwa wanapoteza sura za kimamlaka wanaishi maisha feki ya kushindana na mabinti. Wakati mwingine unaona wanabinua midomo badala ya kupambana na kuonyesha tumaini la vizazi vijavyo, tukaona tuwakumbushe warudi katika mstari na hiyo ndiyo maana halisi ya hip hop."


SOKO LA HIP HOP

Kwa Zaiid soko la muziki wa hip hop bado ni gumu na anaona ni wakati wa wawekezaji kujitokeza kwa wingi ili kuwarahisishia kufikisha inavyotakiwa ujumbe mzito wanaouimba kwa jamii.

"Japo muziki wote wa Bongofleva soko ni gumu, ni wasanii wachache wana unafuu. Ila hip hop ndio ngumu zaidi kwa sababu haina kiki wala kutaka kuvuma. Lengo lake ni moja tu kufikisha ujumbe sahihi kwa jamii," anasema Zaiid ambaye bado hajatoa wimbo unaohusu maisha yake akitarajia kufanya hivyo mbeleni.

Anasema wasanii wa hip hop wapo wazuri wakipata sapoti katika vyombo vya habari kupiga miziki yao inakuwa rahisi jamii kuelewa ujumbe wao na inaweza ikafikia hatua wakafikia anga za kina Jay-Z.

"Kuna wasanii wanajua kuchana mistari kwa Kiswahili, Kifaransa, Kiingereza na wakisapotiwa kuna siku wataingia anga za kina Jay -Z. Ukiona muziki wa rap unapigwa, basi katohoa kwa mfumo wa amapiano," anasema.

Kuhusu ushirikina kuwepo katika muziki, anasema kazi hiyo ni kama nyingine akidai, "kuna watu wanafanya kazi katika sekta na bado wanaamini ushirikina, hivyo katika muziki haviwezi kukosekana kwa wale wanaoviamini kwa namna ambavyo wanavisimulia, ingawa binafsi sijawahi kuviona zaidi ya kuwasikia."

Anapozungumzia mapenzi, anasema kwamba hajawahi kuumizwa kiasi cha kushindwa kufanya majukumu yake isipokuwa kuingia kwa mtu asiye sahihi na kukumbana na matukio asiyotarajia.

"Nimeona marafiki zangu ambao wamepigwa na matukio hadi kufikia hatua ya kutaka kufanya uamuzi mbaya kama kujiua, kuleta ugomvi uliopitiliza hadi wa kukamatwa na polisi. Siwezi kujiona bingwa maana nipo na mchakamchaka wa ujana. Naomba nisifike huko," anasema Zaiid anayemtaja msanii wa kike Zuchu kuwa na mwendelezo wa kufanya kazi nzuri na ndiye anayemsikiliza zaidi.


ANGEKUWA MKULIMA

Zaiid anasema kama asingekuwa msanii wa muziki, kwa sasa angekuwa anajishughulisha na ishu za kilimo.

"Nisingefanikiwa katika muziki ningekuwa nafanya shughuli za kilimo na ufugaji. Ilikuwa ndoto yangu tangu nipo mdogo na ndicho kitu ninachokifuatilia zaidi katika mitandao ya kijamii. Ratiba zangu zikikaa vizuri napenda kuishi nje ya mjini niwe na mabwawa ya samaki, nilime, nifuge, nisikie kelele za ndege na miti ikipunga upepo," anasema.

Mbali na hilo, anasema ni shabiki wa Yanga na wachezaji anaopenda kuwafuatilia ni Fiston Mayele ambaye kwa sasa anaichezea Pyramids, Shomari Kibwana, Djigui Diarra, Kouassi Yao, Mudathir Yahya na Stephane Aziz Ki aliyejiunga na Wydad Athletic ya Morocco kwa uchache.