Wizkid, Iba One wafunika tuzo za Afrima

Tuzo za All Africa Music Awards (Afrima)  mwaka 2021 zimefika tamati, huku msanii Wizikid na Iba One wa Mali waking'ara kwa kubeba tuzo nyingi.

Tuzo hizo zilifanyika usiku wa  jana Jumapili Novemba 21, 2021 jijini Lagos nchini Nigeria.

Katika tuzo hizo, Wizkid ameondoka na tuzo tatu ikiwemo ya kipengele cha msanii bora wa mwaka, wimbo bora wa mwaka wimbo bora wa kushirikiana kupitia wimbo wake wa Essence aliomshirikisha Tems.

Kwa upande wa msanii Iba kutoka nchini Mali kashinda vipengele vitano katika  tuzo hizo  ikiwemo msanii  bora wa kiume nchi za Magharibi, msanii mwenye ushawishi, msanii bora wa muziki  Pop, albam bora na mwandishi bora.

Wengine walioshinda ni Edy Kenzo wa nchini Uganda katika kipengele cha msanii bora wa kiume Afrika Mashariki huku Nikita Kering akishinda kile cha msanii bora wa kike katika ukanda huo.

Wengine ni mwanamuziki Koffi Olomide alipewa tuzo ya heshima na msanii mwenye mafanikio na Fally Pupa aliyeshinda kipengele cha msanii bora wa kiume Afrika ya Kati na Sauti Sol walioshinda kipengele cha kundi bora.