WENGE MUSICA BCBG Mbuyu usiofutika licha ya kuvunjika - 2

JANA tulianza makala ya kundi la Wenge Musica BCBG, lililoteka na kuwapagawisha mashabiki na wapenzi wa muziki wa lingala kutokana na ngoma zao kali kwa kusimulia jinsi lilivyoasisiwa na miaka ya mwanzoni ya 1980.
Wakali hao waliosambaratika rasmi mwaka 1997, hivi karibuni walikusanyika pamoja na kupiga bonge la moja ya shoo lililotikisa nchini DR Congo, kiasi cha mashabiki wa kundi hilo kutamani kuona kundi likirejea na kuwapa ile burudani waliyoikosa kwa muda mrefu.
Leo tunaendelea na simulizi ya kundi hilo na safari yao nzima kabla ya kuvunjika na kuzaliwa makundi kadha wa kadhaa yaliyobeba nembo ya Wenge, ikiwa kama moja ya masharti waliyopeana waasisi wa kundi hilo kutaka jina hilo liendelea kudumu daima milele. Endelea...
...
TAMASHA LA KWANZA
Kwa ujumla wote walikuwa bado wanafunzi na walifanya mazoezi ya pamoja kipindi cha likizo, baadhi walikosa hata hayo mazoezi kwa sababu wazazi wao hawakuwaruhusu kuchanganya muziki na masomo kwa pamoja. Tamasha lao la kwanza kufanya kama waimbaji ni katika baa ya Olympia kipindi cha likizo mwaka 1982 na baada ya hapo wote wakarudi shule.
Mwaka 1983 na 1984 wakaanza kufanya matamasha zaidi, muda mwingi wakiimba nyimbo za Victoria Eleison na Viva la Musica.
Jina la Wenge lilikuja kutoka katika timu ya mpira wa miguu ya huko Bandal iitwayo Wenge, na jina Musica walilikopi kutoka katika Benid ya Viva la Musica (ni bendi waliyokuwa wakivutiwa nayo sana).
Wakati huo maraisi wa bendi hawakuwa wanamuziki wa kundi hilo. Mfano maraisi wawili wa kwanza wa kundi hili walikuwa ni wafadhili wao ambao ni Papy Kimbi na Mavo Voka.
Mwaka 1985 kundi likaanza kubadilika na kufanya kazi zake kiweledi zaidi baada ya kupewa nafasi ya kupiga na kutumbiza kama watangulizi katika matamasha yaliyozihusisha Bendi za Viva la Musica, Empire Bakuba na Victoria Eleison.
WATUNGA NYIMBO ZAO
Walianza kuimba nyimbo walizotunga wenyewe kama Laura ya Blaise Bula, Bebe ya Alain Mwanga ‘Zing Zong, Kine Bouger na Ginette za JB Mpiana, Caserine ya Werrason na nyingine nyingi.
Mwaka 1985 Adolphe Ebondja ‘Dominguez’ rasmi akajiunga na kundi hili, lakini haikuchukua muda wazazi wake wakampeleka Ulaya kwa ajili ya masomo.
Ni kipindi hiki ambacho miongoni mwa waasisi ambao ni Aime Buanga na Alain Mwanga ‘Zing Zong’ nao wakapelekwa Ulaya na wazazi wao kwa ajili ya masomo, pia Christian Zitu naye akapelekwa Ulaya na wazazi wake na huu ndio ukawa mwisho wao kuitumikia Wenge Musica (isipokuwa Dominguez aliyerejea mwanzoni mwa miaka ya 90). Wengine ni Dede Masolo ‘Deno Star aliyejitoa katika bendi na kuwa mchungaji (muhubiri) huku Wes Koka akiugeukia muziki wa Injili.
ALBAMU YA KWANZA
Taratibu kundi likaanza maandalizi ya albamu yao ya kwanza na wakati huohuo Werrason akamgundua mwanamuziki mdogo, Alain Mpela Tshwkulenda huko Kingasani (sio Kisangani) wakati huo akiwa likizo (kiasili Mpela anatoka Mji wa Matete).
Alain Mpela alikuwa akiimba nyimbo za Victoria Eleison hasa wimbo wa Ngabelo ndipo Werrason akamgundua. Pia, kipindi hiki mwimbaji Ricoco Bulambemba akajiunga na kundi la Wenge Musica.
Mwaka huohuo, mkaanga chipsi (dramu) aitwaye Pipo na mpiga gitaa la rhythm, Djolina Mandudila waliwasili katika bendi, pia, mpiga gitaa la mi-solo (second solo) Blaise Kombo na mpiga gitaa la besi Eddy Kandimbo nao wakajiunga.
Wakati wa kiangazi 1987, mwimbaji Marie Paul Kambulu alijiunga na bendi. Mwishoni mwa mwaka huo 1987, Jean Baptise Mileya maarufu kama Manda Chante alijiunga na bendi lakini yeye akianzia katika wanamuziki wa akiba.
Eddy Kandimbo alijitoa katika bendi mwanzoni mwa mwaka 1988 na nafasi yake ikachukuliwa na Christian Mwepu Mabanga aliyejiunga mwezi mmoja baadaye tangu kuondoka kwa Eddy.
Mwanamuziki Christian Mwepu alijiunga siku moja na kaka yake Alain Mwepu aliyekuja kuwa msaidizi wa Alain Makaba katika gitaa la solo.
Kundi liliandaa albamu yao ya kwanza katika Studio ya Bobongo na kwa mara ya kwanza Rais wa kundi alitokana na waimbaji wa kundi.
MPELA ASIMAMA KWENYE KRETI
Hadi kufikia mwaka 1988, bendi ilikuwa chini ya uongozi wa wao wenyewe ambao ni Werrason (akiwa Mkurugenzi wa Fedha), Alain Makaba (Mkurugenzi wa Sanaa) na JB Mpiana (Rais wa Bendi). Katika albamu yao ya kwanza walichagua nyimbo nne tu na kati ya hizo tatu za JB Mpiana na moja ni ya Alain Makaba.
Hali hii haikumfurahisha Blaise Bula na kusababisha akose sehemu kubwa ya kurekodi nyimbo hizi katika studio ya Bobongo na nafasi yake ilichukuliwa na kijana mdogo Alain Mpela ambaye muda mwingi alikuwa anasimama kwenye kreti ya soda akiwa studio ili aweze kuifikia kipaza sauti, mwishoni mwa kurekodi albamu hii, Blaise Bula alikubali kushiriki huu ukawa mwanzo mzuri wa Kundi la Wenge Musica BCBG na kuwazidi mahasimu wao hasa Dakamuda Lavinora.
WENGE KAMA VICTORIA ELEISON
Albamu yao ya kwanza Bouger Bouger (maarufu kama Mulolo) ilirekodiwa studio za Bobongo ikawa na mafanikio kiasi, Wenge Musica kwa kiasi kikubwa iliakisi uimbaji wa bendi ya Victoria Eleison (Werrason akiimba kama King Kester, Blaise Bula kama Joly, JB Mpiana kama Debaba).
Wimbo wa Mulolo ulichaguliwa kama wimbo bora wa mwaka Congo kwa kipindi hicho.
Mulolo uliimbwa kwa Kilingala, Kifaransa na Kimbala ambayo ni lugha ya asili ya mama yake Werrason ikitumika sauti iliyotiwa na mjomba wake Werrason, Nico Buakongo. Kundi likawavutia wengi kutokana na mafanikio yake.
Safu ya uimbaji katika albamu ya Bouger Bouger ilikuwa ni Werrason, JB Mpiana, Blaise Bula na Ricoco Bulambemba.
(Alain Mpela, Marie Paul na Manda Chante wakitumika kama wanamuziki wa akiba), gitaa la solo akiwa Alain Makaba, Djolina akiwa katika gitaa la kati ‘rhythm’, Blaise Kombo akiwa katika second solo, Didier Masela akiwa katika gitaa la besi, Don Pierrot akiwa katika tumba (Mbonda), na Maradona akiwa mkaanga chips (drams). Atalaku (rapa) alikuwa ni Noel Ngiama ‘Werrason’.
Muda mfupi tangu kutoka kwa albamu hii mpiga gitaa la pili, Collegien Zola, mpiga gitaa la besi, Delo Bass na mwimbaji Jean Didier Loko(JDL) walijiunga na Wenge Musica, lakini kabla hata hawajamaliza mwezi katika bendi, JDL alipelekwa na wazazi wake masomoni Ufaransa, hivyo ikawa ndio mwisho wa yeye katika bendi hii.
Kundi la Wenge Musica likawa maarufu sana Kinshasa na Congo kwa ujumla. Hivyo wakaona wapanue wigo wa kujulikana zaidi Ulaya na duniani kwa ujumla, wakaamua kufanya maonyesho Ulaya kwa ajili ya kutambulisha albamu yao ya kwanza na pia kwenda kurekodi ya pili nje ya Congo.