Washiriki 12 Bingwa kuwania Toyota Crown

HATIMAYE siku 90 za kumpata mshindi wa Bingwa msimu wa pili zimefikia ukingoni huku zawadi kubwa zaidi ikitangazwa mbele ya washiriki 12 ambao wamesalia katika jumba hilo.

Zawadi hiyo imetambulishwa na kampuni ya Startimes ambayo ni gari aina ya Toyota Crown mpya yenye thamani ya zaidi ya Sh20 milioni ambayo atakabidhiwa wiki ijayo pamoja na fedha taslimu.

Mkurugenzi wa Masoko na Maudhui wa Startimes David Malisa amesema mshindi wa kwanza si ataondoka na zawadi hizo bali atakuwa na fursa nyingine ya kuwa balozi wa Bingwa na kupewa muongozo wa kuishi kistaa.

Shindano la bingwa msimu wa pili lilizinduliwa Julai mwaka huu na kushirikisha washiriki 24 ambao ni mastaa mitandaoni waliokaa katika jumba moja maalum kuonesha uhalisia wa maisha yao na kuoneshwa kwenye televisheni ya Tv3.

 “Tunawashukuru Watanzania wanaoendelea kufuatilia vipindi vyetu, msimu huu wa sikukuu tunawaambia Lipa Tukubusti, lipia vifurushi tofauti upate nyongeza na kushuhudia fainali hii kuona bingwa ni nani msimu huu,” alisema Malisa

Meneja mradi wa shindano hilo, Ombeni Phiri alisema umekuwa msimu mzuri na washiriki waliobakia ni 12 wanaochuana katika fainali na  wiki ijayo mshindi mmoja ataondoka na gari hilo.