Wasanii wavunja ukimya tuzo za filamu nchini

Baadhi ya wasanii nchini wamevunja ukimya kuelekea kwenye fainali ya tuzo za filamu itakayofanyika Desemba 4 mwwaka huu.

Tamasha la tuzo za filamu lililoandaliwa na Serikali kupitia bodi ya filamu nchini litashindanisha filamu 112 zitakazochuana kwenye vipengere 30 tofauti.

Vipengere hivyo ni tamthilia bora, filamu bora ndefu, muigizaji bora wa kike na wa kiume, muongozaji bora, muigizaji bora wa kike na wa kiume, muswada bora, muongozaji bora wa kike na wa kiume, muigizaji bora wa kike na wa kiume chaguo la Watanzania na filamu bora ya makala, filamu bora fupi na tuzo ya heshima.

Vipengere vingine ni filamu bora katika animesheni, sauti, uhariri, muziki, mavazi, haiba, mandhari, usanifu, mapambo, ucheshi, mchekeshaji bora, muigizaji bora chipukizi wa kike na wakiume na vipengere vingine.

Wasanii baadhi wamesema uwepo wa tuzo hizo utaongeza hamasa kwa wasanii kufanya kazi bora zaidi.

"Tofauti na mwanzo tulikuwa tunafanya filamu tu basi umemaliza, lakini sasa tnafanya tukitegemea mwisho wa mwaka kuna kuwania tuzo, bahati nzuri tumeambiwa tuzo hizi zitakuwa ni endelevu," amesema Suzan Lewis "Natasha".

Mzee Yusuph ambaye wengi wanamfahamu kwenye muziki wa taarabu lakini alianza uigizaji kabla ya kuingia kwenye muziki alisema kama kauli mbiu ya tamasha hilo isemavyo, filamu biashara, hivyo tuzo hizo zitafungua milango kwa wasanii kujikita kutengeneza filamu za kibiashara zaidi.

Mjumbe wa kamati ya tuzo, Hatibu Madudu amesema filamu 112 zimeingia kwenye fainali na mchakato wa kuzipigia kura utaanza hivi karibuni baada ya kuonyeshwa  kwenye chaneli y sinema zetu ya Azam Tv kuanzia kesho Alhamisi.

Amesema kutakuwa na aina tatu za kura kwa asilimia 100 ambayo ya kwanza ni za majaji na nyingine ya watazamaji na kura ya tatu itakuwa asilimia 60 ya kura za majaji na asilimia 40 ya kura za watazamaji.

"Mchakato ulianza tangu Septemba 11, kwa hatua ya awali ya kupokea filamu ambazo hadi pazia linafungwa tulipokea filamu 600, zikachujwa na kubaki 112 ambazo zimeingia kwenye fainali," amesema.

Programu meneja wa Azam Media kwenye tuzo hizo, Fatma Mohammed amesema kuanzia kesho filamu hizo zitaanza kuonyeshwa kuanzia asubuhi hadi usiku.

"Lengo ni kuwapa watazamaji nafasi ya kupigia kura kitu ambacho wanakifahamu, hivyo asilimia 80 ya filamu zitakazoonyeshwa kuanzia kesho kwenye caneli ya sinema zetu itakuwa ni filamu zinazowania tuzo kwenye tamasha la filamu," alisema.