Wasanii wa muziki waomba kukutana na Rais Samia

Wasanii wanaounda Shirikisho la Muziki Tanzania (SHIMUTA), wameomba nafasi ya kukutana na Rais Samia Suluhu, kama anavyofanya kwa makundi mengine.

Wito huo umetolewa na Rais wa Shirikisho hilo, Ado Novemba alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mambo mbalimbali yanayohusu shirikisho hilo.

Ado ambaye alikuwa ameongozana na viongozi wa vyama mbalimbali vya muziki, amesema wamekuwa wakishuhudua Rais huyo akikutana na makundi mbalimbali ikiwemo ni hivi majuzi kakutana na chama cha Wanasheria, hivyo ana Imani atawapa nafasi hiyo pia wasanii wa muziki kwa kuwa wanaisubiri sana.

“Tukiwa wasanii tuna mengi ya kumwambia Rais Wetu tukiwa naye ana kwa ana kwani mbali ya kuongoza nchi vizuri lakini kubwa amekuwa akifanya mambo mbalimbali katika tasnia ya muziki ambapo tutatumia muda huo pia katika kumpongeza.

“Mfano zamani tulikuwa tukitambulika na jamii kama wahuni kupitia kazi zetu na hata pale mtu anapokuwa na tabia mbaya anaambiwa acha usanii, lakini sasa mama ametuheshimisha tunaoneka watu mbele za watu,”amesema Ado.

Vilevile amesema kitendo cha kuwaundia mfuko wao wa Sanaa na Utamaduni na sasa kukopeshwa bila riba, kumekuja kuinua sekta hiyo na kubainisha kuwa ana imani miaka michache ijayo haitakuwa hapo ilipo.

Katika hatua nyingine Novemba aliwaasa wasanii kuacha kutunga nyimbo ambazo zinaligawa Taifa kwa kuwa mashairi yao yana nguvu kama moto wa petroli  hivyo ni muhimu wanapoyaandika kuzingatia na utaifa kwanza.

Msanii Whitney Kibonge Mwepesi, ambaye pia ni Katibu wa Chama cha Bongo Fleva, alisema anashangaa kuona nyimbo ambazo zina tungo zenye ukakasi ndizo zinaopewa kipaumbele na wasanii wake kupata nafasi ya kuhojiwa katika vyombo vya habari, huku wale wenye tungo za kuelimisha jamii na zinaweza kusikilizwa na rika zote wakiachwa.

Katibu Chama cha Muziki wa Taarabu, Siza Mazongera alisema wasanii wanapaswa kujua Sanaa ni kazi na Sanaa ni ajira, hivyo wana kila sababu ya kuiheshimu na wako tayari kufanya kazi na mtu yeyote.