Wanaimba kama wanasimulia hadithi

WANAMUZIKI wengi wa Bongo Fleva ya mwanzoni waliimba ngoma zao kwa mtindo wa kusimulia hadithi. Yaani badala ya msanii kuimba wimbo wa kujirusha na kula bata kama vile Attitude ya Harmonize, wao waliimba ngoma zinazosimulia stori kuhusu kula bata na kujirusha kama vile Mikasi ya marehemu Albert Mangwea.

Na tunaposema nyimbo za kusimulia inamaanisha wimbo ambao unasimulia kwa kufuata misingi ya uandishi wa hadithi. Yaani wimbo unakuwa na stori yenye mwanzo, kati na mwisho; ndiyo maana wimbo kama Mikasi unaanza na mstari unaosema ‘Asubuhi ninaamka ninapiga mswaki’ na kumaliza kwa mstari unaosema ‘Ishakuwa usiku, twenzetu tukachukue taksi’.

Kwa makadirio karibu asilimia 50 ya ngoma kubwa za Bongo Fleva zilizotoka kati ya mwaka 2000 hadi 2010 zote ziliimbwa kwa mtindo huo, ngoma kama Zali la Mentali na Nikusaidiaje za Profesa Jay, Starehe na Bosi za Ferooz, Blue ya Mr. Blue, Jini na Binti Kiziwi za Z Anto, Kafia Gheto ya Husein Machozi, Rita ya Marlow na nyingine nyingi.

Sasa kwa sababu wasanii wengi wa kisasa hawatumii tena mtindo huo kwenye ngoma zao, kupitia makala haya tunakuletea wasanii wapya wa kuanzia mwaka 2010 hadi leo ambao kwa namna moja bado wanaendelea kuenzi mtindo wa uandishi wa nyimbo wa kusimulia hadithi.


RAPCHA

Kwa sasa anavuma kwa jina la Mtoto wa Taifa baada ya kuachia wimbo wenye jina hilo hilo ambao humo ndani anasimulia stori ya safari ya mama yake kuanzia kutoka kuwa mama wa familia hadi mama wa Taifa; wimbo ambao kimsingi unahusu historia ya Tanzania kupata Rais wa kwanza wa kike, Rais Samia Suluhu.

Mtoto wa Taifa haukuwa wimbo wake wa kwanza kuimba kwa mtindo huo, alifanya hivyo kwenye moja ya ngoma za mwanzoni, wimbo unaoitwa Kisanga ambapo amesimulia stori ya alivyotongoza demu kwenye daladala mwisho wa siku akaja gundua ni ndugu yake.

Hit Song ya mwisho ya staa huyo inaitwa Lisa, wimbo ambao anasimulia jinsi alivyoponea chupuchupu kuuawa kisa penzi la mwanamke mdangaji. Kitakwimu, asilimia 60 ya nyimbo zote rasmi za Rapcha zimeimbwa kwa mtindo wa kusimulia hadithi.


HARMONIZE

Huwezi kumdhania lakini ukweli ni kwamba kati ya wasanii wakubwa wa Bongo Fleva wa kisasa wanaoimba, Harmonize anaongoza kwa kutumia mtindo wa kusimulia.

Wimbo wake wa Matatizo aliouachia mwaka 2016 ilikuwa ni stori ya namna maisha yake yalivyojaa shida kuanzia anapoamka asubuhi mpaka anaporudi kulala. Pia Atarudi, Never Give na hata singeli yake ya Anajikosha imeimbwa kwa mtindo huo.


SONGA

Ukisikiliza nyimbo za rapa huyu kutoka kundi la Kikosi Kazi ni kama unatazama filamu. Songa ambaye jina lake kamili ni Songaleli Mwangala amebobea kwenye aina hii ya muziki kiasi kwamba husimulia mpaka mapigano kupitia nyimbo zake na kwa inavyoonekana mashabiki wake wanavutiwa na staili hiyo kinoma.

Nyimbo kama Usiku, Enzi za Utoto, Beki Tatu, Mwizi na nyingine nyingi zote ni uthibitisho wa kwamba Songa ni moja ya wataalamu wapya wa simulizi kwa kutumia muziki.


BEST NASO

Unaweza kusema staa huyu kutoka Kanda ya Ziwa ameandikiwa hatma ya kuimba nyimbo za kusimulia tu kwa sababu nyimbo zake alizoimba kwa mtindo huo zimepata umaarufu kuliko alizoimba kinyume chake.

Kwa kifupi, ukisikiliza nyimbo za Best Naso ni sawa na kusoma riwaya kali ya kuhuzunisha kwa jinsi anavyobuni visa na kuvisimulia.

Nyimbo kama Mamu wa Dar, Narudi Kijiji, Maisha ni Utata na Usitoe ni ushahidi tosha wa kwamba jamaa huenda akatengeneza tamthilia kwa kupitia nyimbo.


DIZASTA VINA

Jina lake linaweza kuwa geni masikioni mwa mashabiki wa muziki wa kuimba, lakini wapenda Hip Hop wanamfahamu vizuri. Dizasta ni maarufu zaidi kwa mtindo wake wa kurap kama anaongea, huku nguvu yake ikiwa ni uwezo wake mkubwa wa kuandika.

Nyimbo karibu zote za mkali huyo asiyevuma ni simulizi, kiasi kwamba mpaka hutoa sehemu ya kwanza, ya pili na ya tatu kama vile Bongo Movie. Wimbo wa Hatia una sehemu ya kwanza, sehemu ya pili na ya tatu na zote ameimba kwa kusimulia na hata A.K.A yake inaelezea uwezo wake wa kuimba kwa kusimulia; anajiita Verteller, yaani msimuliaji.