Wakazi ampa moyo Lulu Diva, agusia ishu ya Babu Tale

Wednesday June 08 2022
WAKAZI PIC
By Nasra Abdallah

Baadhi ya wasanii wameendelea kutoa maoni yao kuhusu kauli aliyoitoa Mbunge wa Morogoro Kusini Mashariki, Hamis Taletale maarufu kwa jina la Babu Tale na safari hii msanii Wakazi naye hakuwa nyuma.

Akiwa anachangia bajeti ya Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo katika vikao vya bunge vinavyoendelea jijini Dodoma, mbunge huyo aligusia suala la mirabaha kuwa haitolewi kwa haki.

Katika hilo alitolea mfano ugawaji wa mirabaha uliofanyika Januari mwaka huu, kuwa haukuwa wa haki na kueleza kuwa haiwezekana msanii Lulu Diva katika ugawaji huo akapata Sh550,000 huku msanii wake Kassim Mganga, akipata Sh50,000.

“Mi natoa mfano, nina msanii wangu anaitwa Kassim Mganga anatokea Tanga, hakuna asiyeimba nyimbo zake kwenye msimu wa harusi.

Kupitia ukurasa wake wa Instagram leo Jumatano Juni 8, wakazi ameandika; ”Tupambanie kiwanda na sio msanii mmoja mmoja,"

Wakazi ambaye jina lake halisi ni Wabiro Wassira amesema ni muhimu kuhoji, ila vizuri zaidi kushiriki kwenye kutatua kwa kutoa mapendekezo ya kipi kifanyike.

Advertisement

“Ila vibaya zaidi hapa babu Tale amedogosha jitihada za Mtoto wa Kike lulu Diva ili tu kutetea msanii wake Kassi Mganga (Gwiji). Sio sawa,” ameandika Wakazi.

Hata hivyo amesema ameona kipande cha hoja za MwanaFA, amehoji vizuri kuhusu numba, na kupitia hapo zipo njia ambayo zinaweza kutumika na Wizara, Cosota, kuboresha.

“Ili kusiletwe mambo ya mazoea alafu tukadogosha ambao tunawachukulia poa. Mimi binafsi ninaheshimu anachofanya Lulu, jitihada zake hazijifichi. Viongozi tupambane ili kila mtu apate zaidi na sio kuona mwingine hastaili anachopata tena Binti, ambaye haihitaji hata maelezo kwa mtu kujua wanapitia vikwazo vingapi.

Divana usisononeke, tupo na wewe! Ila Gwiji Kassim, kama kuna chako hujapewa kitakuja na utakipata,” ameandikamsanii huyo wa Hiphop.


Advertisement