Wadau wampongeza Diamond Platnumz

Dodoma. Msanii wa muziki Diamond Platnumz ametajwa kuwa ni msanii ambaye  ameitangaza lugha ya Kiswahili duniani kutokana na kutumia majukwaa ya kimataifa kutumbuiza kwa lugha hiyo.
Mbali na pongezi hizo, pia Diamond Platnumz mwaka juzi alipewa Tuzo ya kuendeleza lugha ya Kiswahili na Swahili Vision Internaational Association (SVIA) kama msanii anayeitangaza zaidi lugha hiyo kupitia muziki wake.
Hayo yamesemwa leo wakati uwasilishaji wa  mada ya Ubidhaishaji wa Lugha ya Kiswahili katika siku ya pili ya maadhimisho ya Siku ya Kiswahili yanayofanyika kwenye ukumbi wa Hazina jijini Dodoma,
Akiwasilisha mada hiyo, Profesa Fabian Senkoro amesema  msanii Diamond Platnumz amekuwa na mchango mkubwa katika kukuza na kueneza Kiswahili nje ya mipaka ya Tanzania.
“Msanii wa Muziki Diamond Platnumz amekuwa akiimba kwa lugha ya Kiswahili na watu wanacheza hata kama hawaelewi, lakini hiyo ni njia ya kukitangaza nje ya mipaka ya Tanzania,” amesema Profesa Senkoro.
Amesema upo umuhimu wa kuweka mikakati kwa ngazi ya kidunia, Kiafrika, Tanzania na mtu binafsi ili kuipa thamani lugha ya Kiswahili.
Profesa Senkoro alisema kiongozi wa Libya ambaye kwa sasa ni marehemu, Muammar Gaddafi aliwahi kuwa na mikakati ya kukifanya Kiswahili kuwa lugha jumuishi Afrika.
Alisema kiongozi huyo aliwahi kuomba walimu wa Kiswahili 9,000 nchini kwa ajili ya kutimiza azma yake, lakini ombi lake halikufanyiwa kazi.
Pia, alimema Rais wa zamani wa Gabon, Omar Bongo aliwahi kuomba mwalimu wa Kiswahili ili amfundishe lugha hiyo, lakini ombi hilo nalo halikufanyiwa kazi.
Leo ni siku ya mwisho ya Siku ya Taifa ya Kiswahili ambapo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla atatoa tuzo kwa watumiaji bora wa Kiswahili akiwamo Rais John Magufuli ambaye atapewa nishani ya juu ya Shaaban Robert.


Imeandikwa na Gadi Solomon