Utom Boy ulivyombadilisha Wolper

Muktasari:
- Nyota huyo wa filamu na mjasiriamali, alisema enzi za ujana wake alikuwa akipenda kuvaa kiume na kusababisha kusakamwa na watu mtaani, jambo lililomfanya aanze kuvaa mavazi fulani ili kubadilisha mwonekano wake.
MWANAMITINDO Jackline Wolper amefunguka aliamua kuanza kuvaa magauni na kuvaa mawigi ili kuondoa ule muonekano wa kiume, 'Utom Boy' kama watu walivyokuwa wanamwambia.
Nyota huyo wa filamu na mjasiriamali, alisema enzi za ujana wake alikuwa akipenda kuvaa kiume na kusababisha kusakamwa na watu mtaani, jambo lililomfanya aanze kuvaa mavazi fulani ili kubadilisha mwonekano wake.
Akizungumza na Mwanaspoti juzi Jumamosi baada ya kutunukiwa tuzo kama mdau wa sanaa na utamaduni waliokopeshwa pesa na Mfuko wa Utamaduni na Sanaa na kurejesha mikopo yao vizuri, alisema miaka 10 iliyopita alikuwa mtu wa kuvaa nguo za kiume, alikuja kubadilika kuvaa nguo kubwa kubwa alipoanza kuwa mwanamitindo wa kushona nguo za kike.
“Watu wamekuwa wakinishangaa sana ninapovaa hizi nguo kubwa zenye kunipita mwili, yaani bora ya sasa lakini sio yule Wolper wa zamani ambaye kila mtu alikuwa ananiambia kwa nini navaa kama ki tom boy, zangu zilikuwa kaptula na mashati ya kiume na nafikiri ile ilikuwa ni ujana," alisema Wolper na kuongeza;
"Ili ubadilike unatakiwa ujibadilishe wewe mwenyewe usisubiri kubadilishwa na watu kwanza, hivyo akili iliponijia ya kuanzisha kushona nguo za zike na kuwa mwanamitindo wa kuwavalisha watu nikaona isiwe tabu ngoja nianze kutinga magauni na niweke nywele kichwani maana nilikuwa mtu wa kunyoa vipara tu.”
Kwa wapenda kutazama filamu, kama ulibahatika kutazama filamu Wolper akiwa anacheza, kuna filamu ilikuwa inaitwa Tom Boy au Dereva Taxi utamjua ni mwigizaji wa aina gani. Akiamua kuwa msichana mrembo katika filamu utapenda swaga zake, pia akisema awe mwanamke nunda, utafurahi na roho yako.
Jacqueline Massawe ndilo jina alilopewa na wazazi wake alipozaliwa kule kwao Moshi mkoani Kilimanjaro, lakini wadau wa filamu Afrika Mashariki wanamtambua kama Jacqueline Wolper.
Kama ni mpenzi wa kutazama filamu za kibongo, kitambo kidogo kuna kuna filamu inaitwa Tom Boy hii ukiangalia utamwona Wolper alivyocheza kiume na mavazi ya kiume.