Mbosso: Ni kweli nimerudi kijijini, ila...!

Muktasari:
- Hivi karibuni msanii huyo aliyetamba na nyimbo kama 'Kupenda', 'Over', 'Amepotea', 'Umechelewa' na nyingine nyingi ameonekana katika picha za Instagram akiwa kijijini kwao Kibiti, Pwani na wengi kudhani maisha yake yamekuwa magumu tangu aondoke katika lebo hiyo.
STAA wa muziki wa Bongo Flava, Mbosso Khan amesema madai ya kurudi kijijini baada kuondoka katika lebo ya muziki ya WCB, ametafsiriwa vibaya na watu mitandaoni.
Hivi karibuni msanii huyo aliyetamba na nyimbo kama 'Kupenda', 'Over', 'Amepotea', 'Umechelewa' na nyingine nyingi ameonekana katika picha za Instagram akiwa kijijini kwao Kibiti, Pwani na wengi kudhani maisha yake yamekuwa magumu tangu aondoke katika lebo hiyo.
Hata hivyo, akipiga stori na Mwanaspoti, Mbosso alisema ni kweli alienda kijijini kwao Kibiti, lakini sio kuwa mambo yake yamekuwa magumu kama baadhi ya watu wanavyodai.
"Wakati mwingine huwa nayafurahia sana maisha ya mitandaoni na wakati mwingine huwa yanakera sana, mimi kwenda nyumbani kwetu Kibiti ndiyo maisha yangu yamekuwa magumu jamani? Inamaana kila anayeenda kwao basi mjini pamemshinda? Mie nimeenda kule kuna ndugu, jamaa na marafiki pamoja na shughuli nyingine huwa nazifanya kule mbali na muziki," alisema Mbosso.
Mbosso alisema ukimya wake wa kutotoa nyimbo tangu atoke lebo ya Wasafi ni kutokana na anajipa muda kwanza, hivyo mashabiki wasiwe na shaka kwani kazi zipo tayari na zingine zinaendelea kutengenezwa.
"Naona mashabiki zangu wakililia kazi mpya, niwaambie tu vilio vyao nimevisikia na navifanyia kazi, ila nimejipa muda kidogo wa kuweka baadhi ya mambo sawa, ila kazi zipo na zingine naendelea kuzitengeneza muda siyo mrefu mashabiki zangu wataondoa kiu waliyonayo," alisema.
Mwanaspoti lilimuuliza gharama alizotozwa kiasi gani cha pesa na lebo hiyo inayomilikiwa na Diamond Platnumz baada ya kutaka kuondoka na alisema;
"Huwezi kuamini. Nimekuwa chini ya lebo ya Diamond Platnumz kwa takriban miaka saba. Nilipoamua kuondoka sikupewa masharti ya kulipa chochote, hiki ni kitendo cha upendo mkubwa sana kuniruhusu niondoke bila masharti," alisema Mbosso.