Ukimya wa Lava Lava mwaka mmoja nje ya WCB
Muktasari:
- Lava Lava, mkali wa kibao cha Basi Tu (2021) alichoshirikiana na Mbosso, kwa sasa amekaa zaidi ya miezi 10 bila kuachia kazi yoyote mpya kwa ajili ya mashabiki wake.
UKIWA umetimia mwaka mmoja tangu aachane na lebo ya WCB Wasafi, msanii Lava Lava, 33, ameonekana kujipa kama likizo katika upande wa muziki kutokana na ukimya wake, hali ambayo ni ya kwanza kushuhudiwa tangu alipoanza safari yake ya kimuziki takribani miaka tisa iliyopita.
Lava Lava, mkali wa kibao cha Basi Tu (2021) alichoshirikiana na Mbosso, kwa sasa amekaa zaidi ya miezi 10 bila kuachia kazi yoyote mpya kwa ajili ya mashabiki wake.
Ukimya huu mrefu zaidi kuwahi kushuhudiwa kwa Lava Lava unakuja baada ya kuondoka kwake ndani ya lebo iliyomtoa kimuziki ya WCB Wasafi ya Diamond Platnumz.
Mwaka mmoja uliopita, Lava Lava aliondoka WCB Wasafi akiwa ni msanii wa sita kufanya hivyo, akiwemo Rich Mavoko, Harmonize, Rayvanny, Queen Darleen na Mbosso.
Utakumbuka Lava Lava alitoka kimuziki baada ya kusainiwa na WCB Wasafi ambapo kwa mara ya kwanza alisikika rasmi kupitia wimbo wake Bora Tuachane (2017) uliotayarishwa na Laizer Classic wa Wasafi Records.
Hata hivyo, kabla ya kusainiwa WCB Wasafi, Lava Lava alipitia taasisi ya ukuzaji vipaji ya muziki ya Tanzania House of Talent (THT), ambapo alipata mafunzo ya muziki yaliyomjenga na kumfanya kuwa mwimbaji mwenye uwezo mkubwa.
Taasisi ya THT imewahi kuwatoa wasanii wengi maarufu wa Bongo Fleva, baadhi yao wakiwa Mwasiti, Barnaba, Linah, Amini, Recho na Ally Nipishe, mshindi wa Tuzo za Muziki Tanzania (TMA) kama Msanii Bora Chipukizi 2013.
Kwa hivyo, inaweza kusemwa kuwa WCB Wasafi walimsaini Lava Lava akiwa tayari na msingi mzuri wa muziki, jambo linalojidhihirisha katika ubora wa utunzi na uimbaji wake unaogusa zaidi masuala ya mapenzi na maisha kwa ujumla.
Baada ya takribani miaka minane akiwa na WCB Wasafi, mnamo Juni 2025, Lava Lava alithibitisha kuachana rasmi na lebo hiyo na kuanza safari mpya ya kimuziki akiwa na lebo yake binafsi ya Bite Gang.
Muda mfupi baadaye, aliachia Extended Playlist (EP) yake ya pili iitwayo Time (2025) yenye nyimbo sita, akiwashirikisha Billnass na Yammi, msanii ambaye awali alikuwa chini ya The African Princess, lebo ya Nandy.
EP hiyo ilijikita katika masuala ya mapenzi na starehe kupitia mchanganyiko wa melodi laini, midundo yenye mvuto na mashairi yenye maudhui ya kisanaa.
Hata hivyo, licha ya matarajio makubwa, mapokezi ya EP hiyo katika majukwaa ya kidijitali hayakuwa makubwa kama ilivyotarajiwa, ambapo hakuna wimbo wowote ulioweza kufikisha hata kiwango cha usikilizaji wa angalau mara milioni moja katika mitandao iliyohusika.
Baada ya kuachia EP hiyo, Lava Lava amezidi kuingia kwenye ukimya, ambapo sasa ni zaidi ya miezi 10 bila kutoa wimbo mpya, jambo linalozua maswali kwa mashabiki wake iwapo ni mapumziko ya kimuziki au kuna changamoto katika usimamizi wa kazi zake ambazo hazijawekwa wazi.
Kipindi cha kuondoka kwake WCB Wasafi, Diamond Platnumz aliahidi kumpa mtaji wa fedha ili aanzishe maisha mapya ya kimuziki nje ya lebo hiyo, ingawa baada ya muda Lava Lava alieleza kuwa ahadi hiyo bado haikuwa imetekelezwa wakati huo.
Hata hivyo, Diamond Platnumz alionekana kuwa na mchango mkubwa katika kumtangaza Lava Lava kupitia ushirikiano wa nyimbo kadhaa kama Jibebe (2018), Far Away (2021), Bado Sana (2021), Tuna Kikao (2023) na Kibango (2024).
Mbali na muziki, Lava Lava pia amekuwa kimya katika mitandao ya kijamii, ambapo ukurasa wake wa Instagram wenye wafuasi zaidi ya milioni 3.9 haujaweka posti mpya tangu Januari 13.
Ikumbukwe kwamba Lava Lava ni miongoni mwa wasanii waliowahi kuondoka WCB Wasafi na kuanzisha lebo zao binafsi, ambapo sasa anaendesha kazi zake kupitia Bite Gang.
Kwa sasa, Lava Lava ameungana na wasanii wengine waliowahi kuachana na WCB Wasafi kama Rich Mavoko (Bilionea Kid), Harmonize (Konde Music Worldwide), Rayvanny (Next Level Music) na Mbosso (Khan Music), kila mmoja akiendelea na safari yake ya muziki binafsi.
Hivyo, ukimya wa Lava Lava unaendelea kuwa mjadala mkubwa miongoni mwa mashabiki na wadau wa muziki, baadhi wakijiuliza kama ni sehemu ya maandalizi ya mradi mpya au changamoto katika safari yake ya muziki wa kujitegemea.