Ujio wa umaarufu wa mtandaoni na dhana ya ‘Famous’ kwa vijana

Muktasari:
- Tukirudi nyuma kidogo, enzi za watu kama Michael Jackson, Bob Marley na hata miaka ya kina Mr. Nice, kabla ya mitandao ya kijamii, umaarufu ulikuwa wa ukweli na wenye mizizi kwenye maisha ya halisi.
WASANII wa siku hizi wanaamini kuwa na 'followers' milioni moja na kadhaa Instagram ni sawa na kuwa Wako Jako wa Bongo. Unakuta mtu anavimba kwa sababu ana tiki ya blue kwenye akaunti yake na followers laki nane na nusu. Lakini hebu tujiulize, umaarufu wa followers ni umaarufu wa kweli au ni umaarufu hewa.
Tukirudi nyuma kidogo, enzi za watu kama Michael Jackson, Bob Marley na hata miaka ya kina Mr. Nice, kabla ya mitandao ya kijamii, umaarufu ulikuwa wa ukweli na wenye mizizi kwenye maisha ya halisi.
Mastaa wa zamani walikuwa mastaa kweli kweli na hii ni kwa sababu wengi walikuwa mastaa wa dunia. Kumbuka kwenye filamu, tulikuwa tunamjua Van Damme utadhani alikuwa ni mtanzania mwenzetu. Tulikuwa tunamjua Schwarzenegger utasema tunakaa naye mtaa mmoja, hao kina Jet Lee na Jack Chan ndo usiseme. Lakini siku hizi mtu ukiambiwa utaje mastaa wa muvi watano tu unashindwa. Kwa nini? Kwa sababu nguvu ya umaarufu imepungua sana. Msanii ana followers wengi Instagram lakini kwenye maisha halisi, watu hawamjui kiivyo kama anavyodhani.
Zamani mtu unakuwa unafahamu 50 Cent hata kama hupendi Hip Hop. Watu tulikuwa tunawajua wachezaji mpira wengi bila hata kupenda mpira, kina Zidane, Gaucho, Ronaldo, Beckham, lakini siku hizi ukimtaja Messi na Cristiono umemaliza.
Siku hizi, wasanii wengi wanadhani kuwa na wafuasi wengi mtandaoni ni tiketi ya kuwa maarufu. Wanafanya kila kitu kwa ajili ya content: wanapika drama zisizo na skendo na kutengeneza kiki za kiduwanzi, wanapigana hadharani, wanavaa uchi ilimradi wapate likes. Haya yote hufanya wajione maarufu, lakini ukweli, nje ya simu zao, hakuna anayewajua.
Hali hii huwapa stresi kubwa wanapokutana na maisha halisi. Unaenda kwenye sehemu, hakuna anayekutambua. Unajaribu kuuza bidhaa, hakuna anayenunua. Wanafikiri umaarufu wao wa mtandaoni unamaanisha mafanikio ya kweli, lakini wanapogundua si hivyo, huzama kwenye dimbwi la huzuni na wasiwasi.
Dogo wa Wasafi, D Voice alisimulia alivyokwenda South Africa kwa mara ya kwanza alidhani yeye ni staa, ajabu ni, alivyoingia Supermaerkt hakuna mtu hata mmoja aliyemshobokea. Ndo dogo akagundua kumbe mie bado sana.
Kuwa maarufu mtandaoni ni sawa na kujenga nyumba ya karatasi. Ikiwa Instagram itapotea kesho, ni wangapi wataendelea kuwa na ushawishi? Ni wangapi wataweza kusimama kwa miguu yao bila msaada wa mitandao ya kijamii?
Umaarufu wa kweli haupimwi kwa idadi ya wafuasi, bali kwa athari unayoacha kwenye jamii. Hili ndilo walilofanya Bob Marley, Michael Jackson na hata Mr. Nice na mastaa wa zamani. Umaarufu wao ulijengwa kwenye kazi ya kweli. Siku hizi madogo wengine wanajiita wasanii na hawana hata kazi wanayofanya.
Fanya kazi yenye thamani: Badala ya kufukuza likes, jenga kazi inayoweza kudumu. Hata kama huna mamilioni ya wafuasi, kuwa na watu wachache wanaothamini unachokifanya ni bora zaidi.
Tambua tofauti ya umaarufu na athari: Umaarufu wa mtandaoni ni wa muda mfupi. Athari ya kweli inahusisha kubadilisha maisha ya watu kwa namna chanya.