TUZO ZA GRAMMY: Hapa kina Mondi, Alikiba, Nandy kuna vigezo, wataweza?

Muktasari:
- Zipo sababu nyingi za nchi hiyo ya Afrika Magharibi kufanya vizuri sio tu kwenye tasnia ya burudani pia hata kwenye soka, nyota kama Victor Osimhen anayekipiga Galatasaray S.K ya Uturuki, Ademola Lookman (Atalanta) na Asisat Oshoala anayekipiga Bay FC Ligi ya Wanawake Marekani.
PENGINE baadhi ya watu wamekuwa wakijiuliza kwa nini muziki wa Nigeria unazidi kukua siku hadi siku na wasanii wao wakichaguliwa kuwainia tuzo mbalimbali kubwa za muziki zikiweko za Grammy.
Zipo sababu nyingi za nchi hiyo ya Afrika Magharibi kufanya vizuri sio tu kwenye tasnia ya burudani pia hata kwenye soka, nyota kama Victor Osimhen anayekipiga Galatasaray S.K ya Uturuki, Ademola Lookman (Atalanta) na Asisat Oshoala anayekipiga Bay FC Ligi ya Wanawake Marekani.
Kukua kwa muziki wa Afrobeat kimataifa inaweza kuwa moja ya sababu ya nchi hiyo kukinukisha vyema duniani kutokana na aina ya muziki huo.
Wasanii kama Burna Boy, Wizkid na Tems ni miongoni mwa nyota wa Nigeria wanaoufanya mziki wa Afrobaet kuendelea kusikilizwa siku hadi siku.
Ukiachana na hilo pia hata mafanikio ya Burna Boy kwenye mziki huo waliofungua njia kwa kizazi kipya cha wanamuziki wa Kiafrika akishinda Grammy. Albamu yake Twice As Tall ilishinda tuzo ya 'Best Global Music Album' mwaka 2021 na hii iliwatia moyo wasanii wengine wa Nigeria.
Tofauti na Tanzania ambayo imepakana na nchi za Afrika Mashariki, Nigeria kuna kundi kubwa la Wana Diaspora hasa Wamarekani na Waingereza ambao wamekuwa na mchango mkubwa wa kuwaunga mkono wasanii wao na wana nguvu ya ushawishi wa tuzo za Grammy inayosaidia kueneza mziki huo.
Pia kuimarika kwa tasnia ya muziki wa Afrika ambao umekuwa ukikubalika zaidi duniani mfano waandaaji wa Grammy wameanzisha kategori kama 'Best Global Music Album' ambayo imefungua fursa ya wasanii wa Afrika kuangaziwa zaidi.
Hivyo mafanikio ya Nigeria kwenye tuzo za Grammy si ya bahati, bali ni matokeo ya kazi ngumu, ubunifu na uwekezaji wa muda mrefu katika tasnia yao ya muziki.
Kwa mantiki hiyo inatoa taswira ya kwa nini Bongo Fleva ama wasanii wa Tanzania hawapati soko kubwa la kimataifa tofauti na Nigeria ama Afrika Kusini.
Kwetu Bongo msanii Diamond Platnumz amekuwa akipambania ufalme wake kwenye soko la kimataifa akifanikiwa kufanya kolabo na wasanii mbalimbali kama Rick Rose, Morgan Heritage, Omarion na wengine.
Licha ya juhudi hizo Diamond alishindwa kuileta tuzo hiyo Bongo mbele ya Wanigeria hao ambao wameukamata ulimwengu wa burudani.
Tangu Mei 4, 1959 kwenye sherehe za kwanza za ugawaji wa tuzo hizo hadi sasa Tanzania haijawahi kuleta Grammy.
Mara ya kwanza nyimbo za Chibu kuingizwa kwenye tuzo hizo ilikuwa mwaka 2020 wimbo wa 'Jeje' na 'Baba Lao' katika kinyang'anyiro hicho na kuishia hatua ya kwanza yaani Consideration na mwaka jana 'Komasava' ikiingia kwenye tuzo hizo na kugonga mwamba mbele ya Yemi Alade 'Tomorrow'.
Hadi sasa Chibu ana tuzo mbalimbali za kimataifa ikiwemo MTV Africa Music Awards kama Best Live Act mwaka 2015, MTV Europe Music Awards mwaka huohuo kama Best African and Indian Act na Afrima mwaka 2019 kama Best Live Act.
Nyota huyo na wengine kutoka Tanzania ambao wanafanya vizuri hawako mbali kwenye mafaniko ya kimuziki kama ya kina Wizkid isipokuwa kuna vitu wanapaswa kufanya ili heshima ya Grammy itue Bongo.
Ili Diamond na wasanii wengine Bongo warudi na tuzo hivi hapa ndio vigezo vya kupenya huko.

UANACHAMA
Kwanza lazima uwe na mwanachama (kutoka Grammy) mwenye haki ya kupiga kura katika Recording Academy.
Kabla ya kuingiza wimbo au albamu yako unatakiwa kuhakikisha una wanachama wengi zaidi wa kukupigia kura ili pindi utakapoingiza kazi zako basi hao ndio watakaokusukuma ili kuingia katika kinyang’anyiro hicho.
KUHUDHURIA MIKUTANO
Mbali na kuwa na wanachama pia utatakiwa kuanza kuhudhuria mikutano ya Grammy ya ana kwa ana pamoja na ile inayofanyika kwenye mitandao ili kujua taratibu na sheria za tuzo hizo.
Pili mshiriki anapaswa kufanya maandalizi mapema (miezi 12-24) kabla ya Grammy.
WIMBO WA VIWANGO
Hakikisha wimbo unaochagua kuingia katika kinyang’anyiro hicho unakuwa bora kwani wanachama wa ‘Recording Academy’ wanahimizwa kupigia kura muziki kwa kuzingatia ubora, si umaarufu.
Hapa ina maana kuwa haiangaliwi kama wimbo huo umekuwa maarufu kiasi gani bali ubora wa wimbo kuanzia ulipotengenezwa.
Lakini waandaji wa tuzo hizo wanashauri wanaoingiza nyimbo zao kwa mara ya kwanza kufanya utafiti wa kategori pamoja na kuomba ushirikiano au kuwauliza washindi wa tuzo hizo wa nyuma.
TIMU ILIYOSHIBA
Aidha msanii anatakiwa kuwa na timu iliyonyooka asitumie bajeti kubwa kwenye kurekodi, anatakiwa kuhifadhi kiasi kikubwa cha bajeti ili kuajiri washauri, wasimamizi, mapromota, wataalamu au maajenti wa masoko ambao watakakusaidia kuendesha kampeni za kupigiwa kura katika hatua ya kwanza ya Grammy iitwayo ‘For Your Consideration’.
KUJIANDAA MAPEMA
Kutoa ngoma mapema na kuweka mkakati madhubuti wa kuusambaza muziki wako. Kama mwaka huu tuzo hizo zimekupita basi unatakiwa kutazamia kwa mwaka mwingine na utatakiwa kutoa ngoma kuanzia sasa kufanya promosheni, kusambaza muziki kwa lengo la kuweka 'attention' kwenye mitandao ya kijamii na platform mbalimbali ili iwe rahisi baadaye kuingiza katika tuzo hizo.
Kufanya kampeni hatua ya kwanza ya kupigiwa kura ‘For Your Consideration’
Baada ya kuingiza wimbo wako katika hatua hiyo ya kwanza na Grammy ikakubali basi unachotakiwa ni kuanza kufanya kampeni kwa kuwajulisha wanachama wenye haki ya kukupigia kura waweze kukupigia raundi ya kwanza.
KUFUNGUA TOVUTI YA FYC
Msanii utatakiwa kuweka vitu vyako kadhaa ikiwemo video za nyuma ya pazia za wimbo wako, historia fupi kuhusu muziki wako, wasifu wako kama msanii, orodha ya timu na washiriki.
Lakini katika tovuti hiyo hupaswi kuingiza vitu kama kuweka maneno ya kashifa kutoka kwa msanii mwingine, kutumia nembo ya Grammy na kuwahonga wapiga kura.
Wimbo utakaopendekeza utatakiwa kuwa na matokeo kwa jamii
Mfano mwanamuziki kutoka Nigeria, Yemi Alade wimbo wake wa Tomorrow umepenya kutokana na kuitia moyo jamii ambayo imekata tamaa.
Vigezo hivi ndivyo vinaweza kuwapitisha wasanii wa Bongo kama Harmonize, Ali Kiba, Nandy, Maua Sama na wengine wengi ambao wamekuwa wakifanya vizuri.