Tuzo za filamu Tanzania 2022 vipengele 25 kuwaniwa

Muktasari:

  • Filamu zitakazoshindanishwa katika utoaji wa tuzo hizo ni zile zilizotoka kuanzia Januari 2021 hadi Julai 2022

Dar es Salaam. Utoaji tuzo wa za filamu Tanzania unaingia msimu wake wa  pili ukiwa unasimamiwa na serikali, ambapo mwaka huu tuzo hizo zinatarajiwa kutolewa jijini Arusha.


Akizungumza leo Oktoba 30, 2022 katika ufunguzi wa dirisha la upokeaji tuzo, Katibu Mtendaji wa bodi ya filamu, Dk Kiagho Kilonzo amesema tuzo zitakazoshindanishwa zitatoka maeneo mbalimbali ya nchi kuanzia leo wanaanza kuzipokea shughuli itakayoenda mpaka Oktoba 30 mwaka huu.


Dk Kilonzo amesema malengo ya utoaji tuzo hizo ni katika kutambua mchango wa wasanii wa filamu kutambua vipaji,kuongeza hamasa za uzalishaji wa filamu nyingi, kusisimua fursa katika tasnia ya filamu na kuongeza uzalishaji wa filamu bora.


Katibu huyo amesema tofauti na msimu uliopita, wamefanya baadhi ya maboresho katika utoaji tuzo hizo ikiwemo muonekano mpya wa tuzo yenyewe.


"Utofauti mwingine tuliokuja nao ni namna ya kupiga kura ambapo tofauti na mwaka jana ilikuwa ni kwa njia ya mtandao tu ila mwaka huu watu watapiga pia kwa njia ya kutuma  ujumbe mfupi wa kwenye simu zao," amesema Katibu Mtendaji huyo.


Emmanuel Ndumukwa ambaye ni Mkurugenzi wa Maendedeleo ya Filamu amesema vipengele 25 vitashindaniwa katika tuzo hizo ikiwemo filamu bora ndefu,Tamthiliya bora, muongozaji bora wa kike na wa kiume, muigizaji bora wa kike na wa kiume na mswada bora.


Vipengele vingine Ndumakwa amevitaja ni filamu bora ya makala, filamu bora fupi, filamu bora animesheni, filamu bora sauti, filamu bora muziki, filamu bora mavazi na filamu bora haiba.


Pia ipo filamu bora picha, filamu bora uhariri, filamu bora mandhari, filamu bora mapambo, filamu bora usanifu, filamu bora ucheshi, mchekeshaji bora wa kiume na wa kike, tamthiliya bora ya ucheshi, muigizaji chipukizi wa kike na wa kiume.


"Vilevile kipo kipengele cha muigizaji bora mpambe wa kike na wa kiume,filamu bora iliyotangaza utamaduni,chaguo la watazamaji kwa msanii wa kike na wa kiume na tuzo ya heshima kwa mwanaume na mwanamke,"amesema Mkurugenzi huyo.


Kuhusu vigezo amesema lazma filamu iwe ni kazi halali za muhusika,washiriki kutoa nakala za leseni ya udereva kitambulisho cha taifa au hati ya kusafiria,filamu inaweza kuwa ya mazungumzo au ya kimya.


Baadhi ya wasanii waliozungumza katika hafla hiyo akiwemo Lucas Mhavile maarufu Joti,aliiopongeza serikali kwa hatua yake ya kuendesha tuzo hizo na kueleza sasa wanaona mwanga katika tasnia ya filamu.


Wakati Abdul Usanga ambaye ni muongozaji filamu ya kombolela na ile ya mama Kimbo,amesema tuzo hizo zimefungua fursa nyingi kwa wasanii akiwemo yeye  aliyehinda mwaka jana katika kipengele cha tamthilia bora ya ucheshi na kushauri wasanii wajitokeze kwa wingi kushiriki mwaka huu.