TUONGEEKISHKAJI: Ngoma za TikTok ni kama wauza simu feki Kariakoo

KAMA hujawahi kufika Bongo, Dar es Salaam, ngoja nikusimulie moja ya staili za wizi na utapeli zinazofanyika katika jiji hili la wajanja ili ikitokea siku umekuja usiwe mgeni kivile.
Kuna staili ya kuuziwa sabuni kama simu. Picha linaanza uko zako Kariakoo mara anatokea mwana mmoja ameshika boksi la simu kali, Iphone macho matatu. Anakuita “white”  au “tall”  ama “big”  kutokana na muonekano wako.

Ukisimama tu anakuambia kuna simu hii hapa mwanangu, Iphone macho matatu nauza bei ya kutupa kabisa. Wewe kusikia bei ya kutupa si utatamani kujua ndo ipi hiyo utauliza bei gani. Atakuambia, “sikia kaka hii dukani pale bila shing’ laki nane hupati hii simu, lakini mimi nataka nikublesi nipe laki na nusu.”
Iphone macho matatu kwa laki na nusu lazima upagawe mwanangu, lakini kwa sababu wewe ni Mtanzania u’shazoea huwezi kununua kitu bila kuomba kupunguziwa bei basi unajikuta unamwambia “fanya laki basi.”

Mwana ili kukuzuga anaanza kulialia, “big, hii simu kali mwanangu, mi nimeichomoa dukani hapo kwa mdosi kwa sababu nina majanga yangu. Fanya hata laki na arobaini basi.”

Unaona isiwe kesi, unazama mfukoni, unachomoa laki na arobaini unampatia mwana. Jamaa anakupa simu, unaikagua unaona simu inawaka freshi, kisha anakwambia leta tuiweke kwenye boksi, unamrudisha, anaiweka kwenye boksi, anakupa boksi lako unaondoka unafurahi kinoma. Unajiona kama umeokota dodo mwanangu. Unawaza jinsi utakavyovimba mtaani na Iphone yako macho matatu.

Hata watoto utakuwa unawaokota kiulaini maana simu kali inafanya uonekane mnyama fulani hivi.
Basi unatembea zako hatua mbili tatu hadi kwenye kituo cha daladala unadandia zako daladala ya Gongo la Mboto. Unapata siti unasema sasa nifungue boksi nitoe Iphone yangu macho matatu nianze kuitumia ili hadi nikifika la Mboto niwe nimeshaizoea. Ile kufungua boksi tu unakutana na sabuni mzee baba.

Hapo ndo akili sasa inarudi kwamba ushaingizwa mjini. Kusema ukweli, nyimbo za wasanii wengi zinazotrendi kwenye mtandao wa kijamii wa Tiktok ni kama wauza simu wa Kariakoo. Wanapokutana na wewe wanakuuzia Iphone, lakini ukishachukua simu unagundua ni kipande cha sabuni.

Yaani ukiwa Tiktok unasikia ngoma inatrendi vibaya, lakini kwa sababu kule zinawekwa video fupifupi hata wimbo wenyewe utasikia kipande kifupi.


Kwa mfano kama ni wimbo wa Zuchu wa Honey, basi kipande utakachokisia Tiktok ni pale kwenye chorus tu ambapo Zuchu anaimba honey.
Sasa ukisikia kipande hicho utaona ni kama vile hii ngoma ni kali kinyama. Utatoka Tiktok na kwenda kokote unaposikiliza wimbo iwe Youtube, Apple Music, Spotify, Boomplay, Audiomack na kadhalika.
Ukifika huko ukianza kuusikiliza wimbo mzima ndiyo unagundua kwamba kipande cha Tiktok kilikudanganya wimbo hata sio mzuri kiivyo. Yaani mzuri kipande kidogo tu, lakni baada ya hapo hakuna chochote.
Nisingependa kutaja majina ya nyimbo ambazo binafsi nilivyosikia Tiktok na nilipokwenda kuzisikiliza mwenyewe nilihisi kama nimeuziwa sabuni wakati niliambiwa nanunua Iphone macho matatu.