TUONGEE KISHKAJI: Wanamuziki wanaoandika sana wanahitaji huruma yetu
INADAIWA binadamu wa kisasa wamepoteza kabisa uwezo wa ku-focus, wazungu wanaita ‘Attention Span’. Takwimu za mwisho zinadai kwamba wastani wa mtu wa kisasa ku-focus ni sekunde nane. Na hiyo ni sawa na kusema kwamba, mtu anaweza kuzingatia kufanya kitu kwa sekunde nane tu na kuhisi amekichoka, anataka kingine.
Takwimu kama hizi zinanifanya ninawaze wanamuziki ninaowakubali ambao wote wana kitu kimoja ambacho binafsi nakithamini zaidi kwenye muziki au wimbo wowote ule, uandishi wa mashairi. Wasanii wote ninaowapenda wanajua sana kuandika na binafsi nadhani kwenye uandaaji wa muziki, uandishi ni kitu kigumu zaidi ya vyote.
Hata hivyo, nyimbo zilizoandikwa sana mara nyingi huhitaji umakini kwenye kusikiliza ili kuelewa kilichoandikwa na kuweza kugundua umahiri wa mwandishi. Swali ni kwenye umakini huu wa kusikiliza au kutazama au kufuatilia vitu kwa sekunde nane, Je, kuna nafasi kwa wasanii wa aina hii kutamba?
Na hii sio kwenye muziki tu, utaona kwenye vitu vingi sana, siku hizi hata movie mtu anatazama huku anachezea simu. Yaani watu hawawezi kufanya kitu kimoja pekee kwa muda mrefu.
Na hiyo ndiyo sababu ya mitandao kama Tik Tok kubamba kwa sababu yenyewe inashikia bango video fupi fupi zinazowapa burudani watumiaji kabla hawajaanza kujisikia kuchoka na kutamani kitu kingine.
Pengine ndiyo maana wasanii wengi wanaobamba siku hizi ni wanaopiga chafya kwenye ngoma zao. Wimbo mzima unasikia mdundo wa kuchezeka, na chafya za msanii za hapa na pale, kisha wimbo unaisha. Watu hawana muda wa kusikiliza umeandika nini kwahiyo pengine nyimbo za aina hiyo ndiyo kimbilio la wasikilizaji wa kisasa.
Kwa maana hiyo nadhani wasanii wanaondika sana wanahitaji kitu kimoja kati ya hivi vitatu. Kwanza, waandike sana lakini kwa staili mpya ambayo itawafanya wasikilizaji wa kisasa wasiopenda kusikiliza sana waendelee na aina yao ya usikilizaji huku wakiendelea kuona umahiri wa uandishi wa wasanii wazuri kwenye uandishi wa nyimbo.
Au wasanii wenyewe waamue kwamba, atakayetaka kuwasikiliza na awasikilize, na asiyetaka asiwasikilize kwa sababu muda mwingine wanasema, mtu hawezi kukosa muda kwenye kitu anachokipenda. Kwahiyo kama msikilizaji anapenda muziki ulioandikwa vizuri atawasikiliza, na asiyependa atakwenda kusikiliza anachopenda.
Na tatu ni pengine wasanii hawa wanahitaji huruma yetu mshabiki, kwamba wakati tunaziruka ngoma zao kwenda kusikiliza ngoma zingine tukumbuke nguvu waliyoitumia kuonyesha umahiri wao kwenye uandishi. Kwahiyo kujifanya tunahitaji vitu vyepesi vyepesi tunakuwa hatuwatendei haki hata kidogo.