TUONGEE KISHKAJI: Sanaa yetu inabadilika ndio somo

SIKU moja muongoza filamu mkongwe wa Marekani, Martin  Scorsese alisema filamu zinazobamba enzi hizi Marekani na duniani kote  filamu za ‘Super Heroes’ kama vile Black Panther, Spider-Man na Batman yeye hazitambui kama filamu kwa sababu akilinganisha na zile walizokuwa wakitengeneza wao miaka ya 1990 na 1980 anaona za kwao zilikuwa bora.

Anasema za kwao zilikuwa zinaongelea mambo halisi ya kwenye maisha ya watu. Zilikuwa zinagusa hisia za watu. Anasema hizi za sasa ni kama Theme Park. Kwa Kiswahili unaweza kusema ni kama kiwanja cha starehe. Unaingia, unafurahi, unatoka, basi. Hakuna kitu cha maana cha kukumbuka, hivyo anadhani filamu hazistahili kuwa hivyo.

Maneno kama hayo amewahi kuyasema P Funk Majani kuhusu muziki unaofanywa na wasanii wa kisasa. Alisema wasanii wa kileo wanaimba vitu visivyokuwa na maana. Vitu visivyoeleweka. Wanaimba matusi, huku maprodyuza wengine wakiwa hawajui hata kutengeneza midundo kwa ubora zaidi ya ‘ku-sample’  kuangalia Nigeria wanafanya nini na kuigizia. Kuangalia kwa Madiba wanafanya nini na kupiga chabo.

Maneno kama hayo pia amewahi kuambiwa kina P  Funk wakati wanaanzisha Bongo Fleva muziki ambao kwa kipindi kile ndiyo ulikuwa mpya na ndiyo ulikuwa unakwenda kuitwa muziki wa kisasa.

Waliambiwa muziki wenu huu wa kisasa ni wa kihuni hauna maadili mnaimba kwa lugha chafu, lugha za matusi, isitoshe hauna hata kitu kipya mnachofanya zaidi ya kuangalia Marekani wamefanya nini kisha kukopi na kupesti.

Na hata waliokuwa wanawaambia kina Majani maneno hayo nao wanaanza kufanya muziki wao waliambiwa maneno hayo hayo na wanamuziki waliowatangulia kwamba, muziki wetu hakuna kitu.

Hii inazalisha swali la je sanaa inaporomoka? Kwamba kila kizazi kinakuja na muziki mbovu zaidi ya kizazi kilichopita au kila kizazi kinakuja na filamu mbovu zaidi ya kizazi kilichopita?

Kitu ambacho wote hatuwezi kupinga ni ukweli kwamba sanaa inabadilika na mabadiliko ya sanaa yanapokuja mara nyingi ni lazima kuna kundi la watu waachwe nyuma na mara zote watu hao ni wale ambao walishiriki kwa kiasi kikubwa kutengeneza sanaa iliyokuwepo kabla ya mabadiliko na ni ama wasanii wenyewe au mashabiki.

Kwa mfano prodyuza kama vile Master Jay ambaye ameishi miaka zaidi ya 20 akitengeneza muziki wa Bongo Fleva, ikija aina mpya ya Bongo Fleva lazima ataachwa nyuma kwa sababu tayari alikuwa na falsafa zake kuhusu Bongo Fleva nzuri.

Kwa hiyo vinapokuja vitu vya tofauti anashindwa kwenda navyo sambamba. Vinamuacha nyuma, na sababu ni kitu ambacho hakipendi. Kwa haraka anaanza kuona upungufu wa hiyo sanaa mpya ambayo labda ni kweli yapo.

Kwa hiyo badala ya kila kizazi kupiga madongo kizazi kipya, ni bora wakongwe wenyewe waelewe kuwa sanaa kubadilika ni lazima. Ni ama wabadilike nayo au waache kizazi kipya kifanye kazi.