TUONGEE KISHKAJI: Rayvanny atatoboa bila bifu na Wasafi?

Tuesday August 02 2022
rayvany pic
By Kelvin Kagambo

BAADHI ya watu wanasema sababu kubwa inayomfanya Alikiba aendelee kuwa msanii mkubwa leo ni kwa sababu ana bifu na Diamond.

Wanadai kimuziki, Alikiba alikuwa ameshapotea zamani lakini mashabiki walipoanza kumshindanisha na Diamond ndiyo hapo akaanza kuonekana bado ana umuhimu kwenye gemu.

Kuna watu wanasema kinachomfanya Rich Mavoko aonekane kama vile hayupo kwenye gemu, ni kwa sababu alipotoka Wasafi aliendelea na maisha yake, hakutaka kutengeneza mabifu na Diamond wala mtu yeyote pale Wasafi.

Wanaosema hivi wanatoa ushahidi kwa Harmonize yeye alipotoka aliendeleza bifu na Wasafi na ndiyo hilo linalomfanya sasa hivi anaonekana anawasumbua Wasafi.

Sio Diamond, sio Salam, sio Tale, kila mtu pale Wasafi akipata upenyo wa kuongea lazima amuongelee vibaya Harmonize.

Kuna watu wanasema, ili uwe msanii wa muziki unayesikilizwa sana hapa Bongo unatakiwa uwe na ka-ugomvi japo kadogo na Wasafi.

Advertisement

Ukibishana na wanaosema hivi watakwambia, taja wasanii wakubwa 10 wanaofanya vizuri Tanzania sasa hivi, kisha ukishakuwa na majina yao fikiria uhusiano wao na Wasafi ukoje? Utakuta asilimia 80 hawako sawa na Wasafi.

Alikiba hayuko sawa na Wasafi, Harmonize hayuko sawa na Wasafi, Nandy hapikiki chungu kimoja na Wasafi, Darasa wakati ana hit tulisema hayuko sawa na Wasafi, kila mtu ambaye anafanya vizuri lazima kuwe na tetesi za chinichini za bifu lake na Wasafi.

Sasa nawaza, kwa jinsi Rayvanny alivyoka Wasafi, Je, ataweza kuendelea kuwa msanii mkubwa kama kipindi alipokuwa Wasafi au hata kuwa mkubwa zaidi ya pale?

Kwa sababu Rayvanny ametoka kwa amani zaidi ya msanii yeyote aliyewahi kufanya kazi na taasisi hiyo. Rich Mavoko ametoka kwa vita wakapelekana hadi Basata, Harmonize hadithi yake kila mtu anaijua.

Sio wasanii tu, hata watu waliokuwa wanafanya kazi idara zingine hapo Wasafi wengi wameondoka kwa shari.

Mwarabu Fighter ambaye alikuwa ni bodyguard wa Wasafi hakuondoka kwa amani, Q Boy msafi ambaye alikuwa ni mbunifu wa mavazi hapo Wasafi hakuondoka kwa amani, Kifesi ambaye alikuwa ni mpiga picha pale Wasafi hakuondoka kwa amani, na wengi walijaribu kutumia ugomvi huo kama chachu ya kuendelea kuhit mjini lakini hawakudumu.

Kwa hiyo ndio maana nawaza, Je Rayvanny akiendelea kufanya muziki wake bila bifu na Wasafi atatoboa au ataishia kuwa kama Rich Mavoko?

Je, akisema atengeneze bifu na Wasafi ndiyo afanye muziki atafanikiwa au ndiyo atashindwa bifu na kubuma moja kwa moja kama kina Q Boy msafi wengine?

Au pengine labda Rayvanny aifanye lebo yake ya Next Level Music ambayo ndiyo anayofanya nayo kazi kwa sasa iwe kama Wasafi B?

Ametoka lakini aendelee kujipendekeze kwa Wasafi? Muda utatupa jibu la Rayvanny atatumia njia gani kuendelea kuishikilia nafasi yake kwenye muziki.

Advertisement