Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

TUONGEE KISHKAJI: Namba zinambeba Macvoice, Instagram inamuangusha

Muktasari:

  • Dogo anaimba vizuri. Ana ngoma kadhaa zilizobahatika kwenda mjini kama vile Nenda na Only You aliyoimba na Mbosso. Kwa kifupi ana mashabiki wake, lakini vyote hivyo havijamzuia kuingia kwenye rekodi ya wasanii waliowahi kuchekwa kwa kufanya shoo za vichochoroni a.k.a shoo za chaka to chaka.

KAMA humfahamu Hamisi Shabani a.k.a MacVoice naomba nikutambulishe; huyu ni msanii wa muziki wa Bongofleva kutoka Lebo ya Next Level Music ya Rayvanny. Alitambulishwa 2021 baada ya Rayvanny kujitoa Wasafi na kuanzisha lebo yake hiyo.

Dogo anaimba vizuri. Ana ngoma kadhaa zilizobahatika kwenda mjini kama vile Nenda na Only You aliyoimba na Mbosso. Kwa kifupi ana mashabiki wake, lakini vyote hivyo havijamzuia kuingia kwenye rekodi ya wasanii waliowahi kuchekwa kwa kufanya shoo za vichochoroni a.k.a shoo za chaka to chaka.

Iko hivi, juzi kulikuwa na video inazunguka mtandaoni ikimuonyesha Macvoice anaimba sehemu ambayo ni kama kwenye banda hivi. Kwenye video hiyo watu walikuwa wakikomenti kwamba dogo alishafulia na sasa anafanya shoo za chaka to chaka, na wengine wakisema lebo yake ya Next Level imeshindwa kumsaidia mpaka anafikia kujidhalilisha kwa kuimba kwenye shoo za vichochoroni namna hiyo.

Sitaki kuzungumzia tuhuma za lebo yake kushindwa kumuhudumia, lakini nakubaliana na waliokuwa wakikomenti. Ni kweli hali ya dogo kwenye gemu ni kama vile hahudumiwi vizuri. Hatoi ngoma, hasisiki, haeleweki kama yupo au alishakata ringi. Yaani bado anajitafuta na kujipambania sana.

Kitu ambacho sikubaliani nacho ni mashabiki kumcheka kwamba anafanya shoo za vichochoroni kwani kusema ukweli kwa hali ya muziki wa Macvoice nadhani namba zinambeba kufanya shoo za vichochoroni. Twende kwenye namba.

Shoo za vichochoroni au chaka to chaka zimepata umaarufu mbaya siku hizi kwa sababu ya Instagram. Unajua huko Instagram kila msanii anajifanya ni msanii mkubwa, msanii mwenye levo za juu na ni msanii wa kimataifa. Kwa hiyo mashabiki nao wanategemea kumuona kwenye shoo zilizokwenda shule, zinazoeleweka, za kimataifa - yaani shoo zenye hadhi.

Lakini, ukweli ni kwamba sio wasanii wote wanabahatika kupata shoo za aina hiyo na hiyo inawafanya wakae muda mrefu bila kufanya shoo. Na shoo ni moja ya njia kuu ya msanii kujiingizia kipato. Kwa hiyo kama hafanyi shoo maana yake hapati pesa. Na hapo ndipo umuhimu wa shoo za chaka to chaka zinapoingia.

Kwenye shoo za chaka to chaka msanii anakwenda vijijini ndanindani huko na kufanya shoo za viingilio vya bia, ambapo kwa shoo moja anaweza kuondoka na hata Sh500,000. Na mara nyingi wasanii wanapokwenda chaka to chaka hufanya shoo nyingi kwa mpigo. Unakuta anafanya shoo hata 10 katika wilaya moja. Na anakuwa na wiki ya kuzunguka hata zaidi ya wilaya tatu akipiga shoo.

Sasa vuta picha msanii kama Macvoice ambaye hatumuoni kwenye shoo za kueleweka. Akienda chaka to chaka akafanya zake shoo kibao za lakini tano maana yake anafunga hesabu ya si chini ya Sh5 milioni ndani wiki. Ukiniuliza mimi nitakwambia ni bora hivyo kuliko kusubiri shoo za mjini ambazo nyingi zitamlipa si zaidi ya Sh10 milioni na anaweza akakaa miezi mitatu asipate hata moja.

Kwa maana hiyo namba zinawabeba wasanii wa levo ya Macvoice kufanya shoo hizi. Na ukweli ni kwamba hakuna msanii ambaye hajawahi kufanya hizi shoo. Hata Diamond amefanya chaka to chaka. Ukiwa msanii mdogo kama Macvoice na ukiwa msanii mkubwa ambaye muda wako wa kuvuma ulishapita shoo za chaka to chaka ni kimbilio na ndizo zitakuokoa na kukuweka mjini.

Kwa hiyo pengine wadau wa Instagram tuache kuwacheka wasanii wanaojitafuta tunapoona wanafanya shoo za chaka to chaka. Hizi shoo ni kimbilio.