TUONGEE KISHKAJI: Mwaka wa uchaguzi tuache wasanii wawe wananchi

Muktasari:
- Kuna wale wanaoimba kwenye kampeni, wanaopanda majukwaani kuwanadi wagombea au hata wale wanaosema waziwazi misimamo yao ya kisiasa; mimi ni CCM, mimi ni Chadema.
LEO tuongee kisiasa. Mwaka wa uchaguzi ndo huu umefika. Natabiri lazima kutakuwa na mijadala mitandaoni na vijiweni kuhusu wasanii wanaojihusisha na siasa.
Kuna wale wanaoimba kwenye kampeni, wanaopanda majukwaani kuwanadi wagombea au hata wale wanaosema waziwazi misimamo yao ya kisiasa; mimi ni CCM, mimi ni Chadema.
Lakini, aina zote hizo za wasanii wanaoshiriki kwenye siasa zinafanana kwenye jambo moja - kusimangwa na raia wenye hasira kali. Raia wamekuwa na kawaida ya kuwashambulia wasanii wanaoshiriki kwenye siasa. Wanasema wanatumika. Wanadai msanii unatakiwa uwe nyutro au hujulikani ni shabiki wa chama au mwanasiasa gani kwa sababu unaweza kupoteza mashabiki ambao wako kinyume na mtazamo wako wa kisiasa.
Na tunasema kwa kujiamini utadhani kuwa msanii kunawaondolea haki zao kama raia wa Tanzania.
Swali tunalopaswa kujiuliza ni hili, kwa nini tunawanyima wasanii nafasi ya kushiriki siasa?
Kwanza, tunatakiwa kukumbuka kwamba msanii pia ni Mtanzania kama mimi na wewe. Wanalipa kodi, wanapiga kura na wanapata huduma sawa na kila mwananchi. Hakuna kipengele kwenye Katiba kinachosema, ukianza kuimba, kucheza au kuigiza unakosa haki ya kisiasa. Hili ni jambo la msingi kuelewa kabla hatujaanza kuwashambulia mitandaoni na kufosi wawe nyutro.
Pili, wasanii wana nguvu ya ushawishi. Wanapochagua kumuunga mkono mgombea fulani hawafanyi hivyo kwa bahati mbaya. Ni kwa sababu wanaamini maono ya mgombea huyo yanaweza kuboresha maisha ya Watanzania. Na kama hawatakubaliana na mgombea mwingine hususan ambaye wewe unampenda, basi huo ni uhuru wao wa mawazo – kitu ambacho kila mmoja wetu anapaswa kuheshimu.
Tatu, tukumbuke kuwa sanaa yenyewe ni siasa kwa namna fulani. Wimbo, filamu au maigizo mengi huakisi jamii. Yanazungumzia changamoto na matumaini ya watu. Kwa hiyo msanii anayesimama jukwaani na kuimba kuhusu maendeleo sio kioja, bali ni mwendelezo wa kazi yake ya kupaza sauti kwa niaba ya wengi.
Lakini kuna wale wanaosema ukishakuwa msanii kaa kimya linapokuja suala la kisiasa. Hili ni sawa na kusema kwa nini unatembea kwa miguu wakati una gari? Kuwa na gari hakukunyimi haki ya kutembea kwa miguu kama ambavyo kuwa msanii hakukunyimi haki ya kushiriki haki zako za kikatiba.
Muda mwingine tunawapa mifano ya nchi za nje kwamba mbona wasanii wa nchi fulani hawajihushi na siasa. Ni sawa kwa sababu haki sio kujihusisha au kutojihusisha na siasa, bali haki ni kuwa huru kuchagua aidha ujihusishe au usijihushe na siasa.
Tunapaswa kuwaacha wasanii wetu wajisikie huru kuunga mkono chama au mgombea wanayemwamini. Mwisho, tusiwatazame wasanii kama mashine za burudani tu. Ni binadamu wenye mawazo, ndoto na matarajio kama sisi. Kama wanataka kutumia majukwaa yao kuhamasisha mabadiliko au kuunga mkono wagombea, basi tuwaheshimu kama wao wanavyoheshimu uamuzi wetu wa kuwa mashabiki wa vyama vya kisiasa tunavyovitaka.