TUONGEE KISHKAJI; Msanii mpya ndo huyo, Bongo movie mjiandae kumpeleka mjini

HAYA haya hayaaaaa! Msanii mpya wa Wasafi ndo huyo katambulishwa kinadada wa Bongo Movie mjiandae kufanya kazi  ya kumpeleka mjini.

Na yeyote tutakayempa kazi itabidi afuate plani hii. Ataanza na picha za mabusu, kisha tumkabidhi mtu mmoja azivujishe kwenye mitandao ya kijamii na kuzitrendisha. Halafu tutakuita kwenye intavyuu na kukuuliza kama kweli unatoka na dogo… kataaa.

Kisha, mwakani ukiwa unasherehekea bethidei yako ya kutimiza miaka 23 kwa mara ya 10, atakuja dogo na kukupa zawadi ya Toyota, Harrier new model. Rangi tutajua baadaye, lakini mimi napendekeza iwe nyeusi au pinki.

Kisha online TV zikikuuliza dogo amekupa gari kama nani? Utasema kama dada yake. Hata ukibanwa vipi hakikisha hausemi kwamba wewe na dogo mnatoka pamoja.

Kisha baada ya wiki mbili tangu upewe gari ndo sasa mtaanza kuweka mahusiano yenu wazi. Mara mpostiane mkiwa out, mara uende kwenye set akiwa anashuti video ilimradi tu watu wajue kwamba mko kwenye penzi shatashata.

Halafu baada ya muda atakupeleka kwao Temeke. Utaenda pale umevaa dela mwenyewe au abaya… ila naona, bora uvae abaya. Kisha madera utayavaa ukiwa unafanya kazi za nyumbani.

Enewei, kwa hiyo ukiwa huko mtapiga picha nyingi sana na mama mkwe (kama yupo) kama hayupo hata mashangazi sio mbaya. Kisha utapiga picha ukiosha vyombo, ukiokota kuni, ukichuma mchicha, ukipika chakula kwenye jiko la kuni, ukichota maji kisimani. Yaani ukijionyesha kwamba wewe ni waifu matirio.

Baada ya hapo mtakaa wiki nne kwenye penzi halafu buuuuuum! Mnaachana. Lakini hamuwaambii watu. Tunaanza kupenyeza udaku Insta. Na wewe ukiulizwa chochote kuhusu penzi lenu jibu “no comment”.

Halafu usisahau kitu kimoja. Usisahau kufuta picha zenu zote kwenye akaunti yako ya Instagram na ‘kumu-unfollow’ dogo. Na yeye pia atafanya hivyo. Kisha baada ya kuachana dogo ataanza kutoa nyimbo za kukunanga ex wake. Mara atakuimba kwamba una kichwa kama chepe na mambo mengine mepesi mepesi ambayo hayataleta shida Basata.

Kisha baada ya hapo na wewe utalipuka na kuanza kuongelea jinsi gani dogo hana shukrani na utaanza kutaja mambo yote uliyomsaidia. Utasema kuhusu Kiingereza ulichomfundisha. Utasema alikuwa hata kuvaa kijanja hajui umemsaidia. Utasema kuhusu yote hayo. Kazi yako itakuwa imeishia hapo. Atakuja mwingine na kuendelea na dogo na tutajua plani itakuwaje. Unajua sanaa ni moja tu, muziki, filamu zote ni sanaa. Kwa hiyo hakuna haja ya kupambana kuinua sanaa ya filamu wakati unaweza kuinua dogo mmoja wa Bongofleva na sanaa ya muziki ikazidi kukua.