TUONGEE KISHKAJI: Master Jay hii ilikuwa na haja?

Muktasari:
- Sasa, kama kuna kitu ambacho kinaweza kusababisha moto ukawaka kwenye mitandao ya kijamii ni kugusa jina la Alikiba, na hivyo ni wazi moto uliwaka!
JUZI kati prodyuza mkongwe wa muziki Tanzania, Master Jay alitikisa meza kwa kutoa maoni yanayoashiria kwamba msanii Bien wa Kenya ni bora zaidi ya Alikiba.
Na alitoa maoni hayo kwa namna ya kuchoma kwelikweli akisema Alikiba ni 'mbana pua'.
Sasa, kama kuna kitu ambacho kinaweza kusababisha moto ukawaka kwenye mitandao ya kijamii ni kugusa jina la Alikiba, na hivyo ni wazi moto uliwaka!
Alikiba naye hakuwa na muda wa kupoteza. Akaja na majibu ya kombora akimwambia Master Jay ajiheshimu na kuacha kutoa maoni akitoa mfano ambao si mzuri kuandikika. Eeeh! Hapo ndo ikawa kama vile amechochea moto kwenye mitandao.
Lakini kwanza nimchape swali Master Jay, "eti Master ilikuwa lazima kumshindanisha Bien na Alikiba?" Muziki ni sanaa na wasanii kila mmoja ana ladha yake. Bien anafanya yake Kenya na Alikiba naye anakinukisha Tanzania kwa Mama Samia. Kuwapambanisha ni kama kusema chai ni bora kuliko kahawa, wakati kila kimoja kina mashabiki waliokufa na kuoza.
Master angeweza kutoa maoni yake bila kuchochea moto wa ushindani usio wa lazima. Tena ushindani kwa watu ambao inaonekana wanapatana vizuri. Mwaka 2016, Sauti Sol akiwemo Bien walimshirikisha Alikiba kwenye ngoma yao ya Unconditional Bae na ilihiti vizuri. Hakukuwa na haja ya kuwashindanisha.
Swali lingine ni je "mbana pua" ni tusi au sifa? Yaani Master aliposema Alikiba ni mbana pua alikuwa anamponda au anamsifia? Ingawa jibu linaweza kuwa alikuwa anamponda kwa sababu kwa miaka mingi jina la mbana pua limekuwa likitumika kuwadharau wasanii wa kuimba.
Kwa mujibu wa rekodi, Alikiba ameendelea kutamba katika top five ya wasanii wakubwa Tanzania kwa zaidi ya miaka 10. Sasa kama miaka yote hiyo amekuwa akiimba kwa kubana pua na bado anapendwa, basi hiyo ni mbinu yake ya mafanikio. Mbana pua, lakini ana hiti za kutosha, shida iko wapi hapo?
Hivyo kusema 'mbana pua' kama ni kosa ni sawa na kumshutumu Messi kwa kuwa mfupi, lakini bado anafunga mabao kibao. Alikiba ni Alikiba na pengine huko kubana pua ni staili yake na kama kuna tatizo, basi tatizo lipo kwa wale wanaopenda hiyo staili. Na ni wengi.
Kama mkongwe wa muziki, Master Jay ana haki ya kuwa na maoni yake. Lakini tatizo ni jinsi alivyoyawasilisha. Watu wanamzingatia kwa sababu anaheshima kubwa kwenye gemu, lakini wakati mwingine ni vizuri kuchuja maneno kabla hujayarusha.
Mwisho wa siku muziki ni burudani. Tusitafute migogoro isiyo na maana, bali tusherehekee vipaji tofauti bila kuweka chuki. Bien, Alikiba na Master Jay wote ni 'icons' kwa njia zao. Kila mmoja ana mashabiki wake na badala ya kupoteza muda kwenye mijadala ya nani bora hebu tusikilize muziki na tufurahie maisha.