TUONGEE KISHKAJI: Kwenye lebo za muziki tuliruka stepu mapema

UKIKAA na wasanii wa Bongofleva ambao hawapo kwenye lebo watakuambia kwanini hawafanyi muziki na lebo. Watakuambia Tanzania mambo ya lebo ni kudanganyana tu. Lebo itakupa pesa, lakini na masharti kibao kama mganga wa kienyeji. Mara upangiwe muda wa kutoa nyimbo kwa madai kwamba inabidi utoe nyimbo kwa ‘plan’, mara upangiwe shoo za kufanya kwa madai ya kwamba muziki ni chapa (brand) ukifanya kila shoo utashusha brand.

Na hata kwenye hizo shoo ambazo lebo inakubaliana nazo mkipata pesa, pande kubwa linakwenda kwa wamiliki wa lebo badala ya msanii mwenyewe. Kwa hiyo mwisho wa siku ndio inakuwa ile msanii BRAND KUBWA lakini mfukoni hamna kitu.

Lakini upande wa pili, ukikaa na wasanii wanaofanya kazi na lebo wanakuambia jinsi gani kufanya kazi na lebo kuna faida. Hutumii pesa yako kumlipa prodyuza, kutengeneza video, kufanya promo, kutafuta shoo, kutafuta madili wewe kazi yako ni kutengeneza muziki mzuri tu. Wanakuambia ukiwa msanii ‘yatima’ unatakiwa ujifanyie mwenyewe kila kitu. Lakini, licha ya kusema yote hayo, bado sioni wasanii wakidumu sana kwenye lebo.

Idadi ya wasanii waliofanya kazi na lebo na kutoka ni kubwa kuliko wasanii waliofanya kazi wenyewe na kuamua kuingia kwenye lebo. Na mara nyingi wengi wanaotoka wanatoa ushuhuda unaodhihirisha kwamba kwenye lebo mambo sio shwari

Nikiwaza Harmonize alivyotoka Wasafi, nikiwaza Killy na Cheedy walivyotoka Konde Gang na sasa nikiwaza kauli za Ibra wa Konde Gang kwenye mitandao ya kijamii kuhusu hali yake ya muziki ambapo anasema imekuwa ngumu sana, najikuta nashindwa kujizuia kuegema upande wa wasanii wanaosema kibongo bongo lebo bado sana.

Na hili nimeshawahi kulizungumza zaidi ya mara moja miaka ya nyuma. Tanzania tuna shida kubwa ya kimfumo ambayo inasababishwa na kuruka ‘steps’. Yaani Tanzania ni kama mtoto ambaye baada ya kukaa akaruka hatua ya kutambaa na kusimama, akaenda moja kwa moja kwenye hatua ya kutembea.

Kwa mtoto ni sawa, lakini kwenye biashara hilo ni tatizo kubwa kwa sababu kila hatua inakupa funzo la jinsi gani unatakiwa kujiweka ngangari na kujiandaa.

Nadhani kwa Tanzania watu tumekimbilia kuwa na lebo za muziki.

Mfumo wa lebo sioni kama ni mfumo sahihi sana wa biashara ya muziki kwa Tanzania.  Na kama ni tayari, basi pengine wanaofanya na mfumo wa lebo sio watu ambao wana uzoefu.

Kwa sababu ukizatama lebo za muziki Bongo ambazo zinafanya vizuri au zinafanya namna ambavyo msanii anatakiwa kufanyiwa na lebo hazizidi tatu.

Nadhani tungejipa muda kwenye mfumo wa kusaidia kama enzi zile za kina Ustazi Juma Namusoma, Tale na Fela pamoja na Ruge Mutahaba kisha kupitia mfumo uleule tungeanza kutambulisha mambo ya mikataba.

Hlafu polepole tungeanza kujitumbukiza kwenye mambo ya lebo za kueleweka na sio hivi sasa hivi msanii akiwa na uwezo wa kununua monita za studio na kinanda pamoja na kumuweka dogo mmoja awe anatengeneza midundo anadhani tayari anaweza kuwa na lebo.