TUONGEE KISHKAJI: Kontawa alivyorudia makosa ya Fid Q

MWAKA 2017 Fareed Kubanda Fid Q alitoa ngoma kali ya kuitwa Fresh. Ilikuwa ni ngoma kali iliyotembea yenyewe bila mbwembwe. Na ili kukuhakishia kuwa ilikuwa ni ngoma kali, mmoja wa wasanii ambao wanatajwa kuwa ni wagumu kufanya nao kolabo, Diamond Platnumz alichukua simu akampigia Fid na kuomba kufanya remix. Fid akakubali, remix ikafanywa.

Remix ilipoachiwa kwanza iliwashangaza wengi. Diamond hakuimba kwenye hiyo ngoma, bali alichana tena vizuri tu. Ilikuwa ni ngoma nzuri mpaka pale ilipofika sehemu ambayo Diamond akachana mstari unaosema “Ukinichukia sikosi hela, hivyo kwangu sio kesi, kuni-compare na Cinderella haiwezi kuwa fresh”. Akaona haitoshi akaongeza mstari mwingine “Viuno vyembamba wanataka pensi ya Pepe Kale, si walitaka kiti nikawapa hadi kitanda wakalale.”

Kwa sisi tuliosoma Cuba tulielewa hiyo mistari yote ilikuwa ikimlenga Alikiba kwa sababu Cinderella ni wimbo wa kwanza uliomtambulisha Alikiba. Na pia Alikiba wakati anarudi kwenye gemu baada ya kuwa kimya kwa muda mrefu alikuwa na kampeni aliyoiita mfalme narudi kwenye kiti chake. Kwa hiyo aliposema alitaka kiti nikampa hadi kitanda akalale, wadau tulijipa majibu kwamba anamwambia Alikiba hasa ukizingatia kipindi hicho ndiyo bifu lao lilikuwa limenoga.

Sasa licha ya kwamba aliyemdisi Alikiba kwenye wimbo alikuwa ni Diamond, lakini watu wakamtupia mzigo wa lawama Fid Q. Wakamwambia kuruhusu Diamond afanye vitu kama vile kwenye wimbo wake ni sawa na kumvunjia heshima Alikiba.

Uzuri ni kwamba Fid Q alikiri kuona ukakasi kwenye mistari hiyo, lakini alijitetea kwamba walipokuwa studio hakuielewa kama mashabiki walivyoilewa baada ya ngoma kutoka. Miaka mitano mbele msanii mwingine, tena msanii anayechipukia anarudia kosa kama hilo.

Kontawa ni rapa ambaye aliachia ngoma nyingi sana lakini majuzi alipoachia wimbo wake wa Champion aliomshirikisha Ney wa Mitego ulipata airtime sana. Airtime kwa sababu vitu alivyokuwa akiimba vilikuwa vinatugusa Watanzania wengi wenye maisha ya chini. Na sio kutugusa tu, bali vinatupa imani kwamba ‘One Day Yes’.

Lakini ngoma ilipoanza kuhit tu, watu wakaisikia na mmojawapo akiwa ni Harmonize Konde Boy Jeshi Tembo. Konde akamcheki Kontawa na kumwambia wafanye remix. Kontawa akakubali na nadhani sio yeye tu, msanii yeyote anayechipukia asingekataa kufanya ngoma na staa mkubwa kama Harmonize.

Lakini ajabu kwenye hiyo ngoma Harmonize naye kafanya mambo yaleyale aliyoyafanya Diamond kwa Fid. Kaimba mipasho ambayo imeonekana kuiua ngoma ya dogo badala ya kuipaisha kama ambavyo pengine Kontawa alitegemea itakuwa. Mistari ya Konde inasema “Nimetoboa mbele ya mkubwa na Tale, kipara na Asaki wa Tandale”

Ambayo kwa mashabiki wanaelewa kuwa Harmonize alikuwa anamaanisha amefanikiwa kimuziki licha ya kupata upinzani mkubwa kutoka Wasafi ambayo iko chini ya Mkubwa Fela na Babu Tale, pia Sallam SK (kipara) na Diamond Platnumz (Asaki wa Tandale).

Mwanzo sikuwa naona tatizo la mistari kama hiyo kwenye ngoma ya Kontawa, lakini baadaye akili ilipokuja kurudi nimegundua inaweza ikawa mibaya kwake kwani inamfanya aonekane amechagua timu, na ni mbaya sana kwa msanii mdogo kama yeye kuonekana yuko upande.