TUONGEE KISHKAJI: Komedi imeanza kutumika vibaya hapa nchini

NAHISI kama komedi imeanza kutumika vibaya nchini. Washkaji wanavaa madela, mawigi, wanapaka shedo na hereni na kuongea au kufanya mambo ya ajabu halafu wanajitetea kwamba wanafanya komedi.

Yaani matukio yanayoendelea sasa hivi yanafanya nikumbuke kitu nilichowahi kukisema hapahapa kwamba sanaa ndiyo inaamua jamii iweje.

Nakumbuka kipindi Sensa ya Watu na Makazi inaendelea chombo kimoja cha habari kilienda kuripoti jinsi inavyofanyika katika Mkoa wa Manyara ndanindani kwenye jamii ya Wahadzabe. Watu huko kwanza wana maisha tofauti kidogo na mjini na tofauti hata na vijijini pia. Baadhi yao bado wanaishi kwa kuwinda wanyamapori na kula mizizi.

Mwandishi akamfuata dogo mmoja akamuuliza una miaka mingapi? Dogo akajibu mitatu. Mwandishi hakuamini akamuuliza tena mingapi? Jamaa akarudia kusema mitatu wakati kwa kumtazama tu anaonekana ana miaka sio chini ya 18. Na alijibu hivyo sio kwa sababu labda ana matatizo ya akili, hapana. Alijibu hivyo kwa sababu hajui kuhesabu. Kwa hiyo hajui mambo ya namba kabisa. Huko kwao kuna shule - sawa, lakini wengi hawana hata mpango nazo.

Lakini huyo dogo alikuwa na ‘dread’ kichwani. Tena sio dread zilizojinyonganyonga tu, hapana. Ni dread ambazo zinaonekana zimetengezewa vizuri saluni. Dread kwa juu na chini amechonga kidogo. Mwandishi akamuingizia swali la mtego akamuuliza unasoma? Akajibu hapana. Akamuuliza, umemaliza masomo au huendi shule kwa sababu ya hizi nywele?

Jamaa akajibu hapana. Sio kwa sababu ya dread. Halafu akaongeza kitu ambacho hata hakuulizwa, akasema, “hizi dread nimesuka kama Diamond.” Mwandishi akamuuliza tena utadhani hajasikia vizuri. Umefanyaje? Jamaa akajibu nimesuka kama Diamond.

Ukiniuliza mimi nitakuambia jibu la dogo linamaanisha alichokiweka kichwani kimechagizwa na Diamond ambaye ni nani? Ni msanii. Hajataka kunyoa kama Mwigulu Nchemba wala kama daktari aliyewahi kumuona. Yeye kataka kusuka kama Diamond. Na hiyo ni sehemu ya ndani kabisa ambayo pengine huyo Diamond mwenyewe hata hamuoni mara nyingi kama vile mtoto wa Sinza Dar es Salaam es Salaam ambaye ana redio, TV, simu, kompyuta, magazeti na kila kitu.

Ndiyo maana nawaambia muda mwingine tunaweza kuchukulia poa hawa wasanii wetu, lakini wao wana mchango mkubwa sana kwenye kutengeneza jamii kuliko tunavyodhani. Jamii yoyote huwa inafanana na sanaa zao.

Ukiona sehemu watu wanapenda pombe, ngono, uasherati wala usitafute mchawi nenda kasikilize muziki wanaosikiliza. Nenda kaangalie filamu wanazotazama. Nenda katazame picha wanazochora.

Na ndiyo maana wanasema wasanii ni kioo cha jamii maana yake ni kama ambavyo ukisimama mbele ya kioo unaona picha yako ndiyo vivyo hivyo ukisikiliza sanaa kinachoonyeshwa kwenye tasnia ndiyo picha ya jamii unayoishi.