TUONGEE KISHKAJI: Filamu hazihitaji uhalisia, zinahitaji kuaminika

WASHIKAJI wanasema Filamu za Bongo hazina uhalisia, kisha wanaanza kusimuliana kuhusu muvi za Rambo, jamaa ambaye yuko pekee yake kwenye uwanja wa vita, anapambana na waveti zaidi ya mia moja na anawamaliza wote na anaondoka na ushindi.

Wanasema filamu za Bongo hazina uhalisia kisha wanachukua ‘flash’ zao na kwenda kwa waweka muvi na kuweka muvi ya Avatar ya James Cameroon, movie ambayo inahusu kampuni kubwa ya kisayansi ya Marekani ambayo imegundua madini ya thamani sana ya Unobtanium yanayopatikana kwenye sayari inayoitwa Pandora na kuamua kupeleka wanajeshi kwa ajili ya kuchukua madini hayo kinguvu na kupelekea kuharibu makazi na amani kwa viumbe wanaoishi kwenye sayari hiyo.

Wanasayansi mtuambie, kuna sayari inayoitwa Pandora? Mtuambie, kuna madini yanayoitwa Unobtanium? Mtuambie, kila kinachoonekana kwenye filamu ya Avatar tumeshawahi kukiona kwenye maisha halisi?

Ninachofahamu mimi ni kwamba filamu hazihitaji kuwa na uhalisia na ndiyo maana zinaitwa filamu. Filamu zinatakiwa kuaminika tu. Na ili wewe mtazamaji uamini, mtengeneza filamu anatakiwa akupe sababu ya kila unachokiona kwenye filamu husika.

Kama kuna mtu anapaa, inabidi mtengeneza filamu afafanue kupitia filamu kwanini mtu anapaa. Na hii inatakiwa hata kwenye filamu za kawaida za drama, unatakiwa uonyeshe kwanini mtu anafanya maamuzi fulani. Kwa sababu kila anayetazama anajua kuwa anatazama uongo lakini anaamini kiasi cha kufikia hatua ya kuogopa kama ni filamu ya kutisha, kulia kama ni filamu ya kuhuzunisha na kucheka kama ni filamu ya kuchekesha.

Kulazimisha filamu ziwe na uhalisia ndiyo kunawafanya wasanii wetu wa Tanzania washindwe kutengeneza filamu zenye mawazo makubwa.

Kulazimisha filamu ziwe na uhalisia kunafanya wasanii wetu waishie kutengeneza filamu za uswahilini pekee, watu wanasutana, kelele za hapa na pale kwa sababu ndiyo vitu wanavyoviona kwenye maisha ya kila siku.

Na hapa sina maana kwamba filamu za uswahilini za watu kusutana ni mbaya. Hapana. Huo ulikuwa ni mfano, na maana ya mfano huo ni kwamba, filamu zinatakiwa ziwe njia ya kutoroka kwenye uhalisia.

Watengeneza filamu wanatakiwa kuwaza vitu ambavyo binadamu hatujawahi kupata nafasi ya kuviishi. Filamu kuhusu Dar es Salaam ya miaka 100 ijayo, filamu kuhusu Tanzania ya miaka 60 iliyopita, filamu kuhusu watu wanapaa, filamu kuhusu watu wanaongea kwa kuimba. Filamu inatakiwa iwe mlango wa kutufanya tuishi ndoto zetu.

Tunapompenda Rambo sio kwa sababu tunapenda anayoyafanya, hapana. Bali ni kwa sababu tunatamani kuwa kama Rambo. Kuwa na uwezo wa kupambana na watu zaidi ya mia, lakini kwa sababu hatuwezi, basi filamu inatupa uwezo wa kuishi maisha hayo kupitia kuitazama.

Ndiyo maana ajenda nyingi mbaya na nzuri huwekwa kwenye filamu kwa sababu filamu zina nguvu ya kumsafirisha mtu na kumbadilisha.

Sasa basi, kama vipi kuanzia leo tuache kuwalazimisha wasanii wetu watengeneze filamu zenye uhalisia. Kama tunataka uhalisia tuchukue viti tukae barazani tutawatazame majirani zetu.