TUONGEE KISHKAJI: Fella Kuti, TX Moshi wanashangilia huko walipo

New Content Item (1)
New Content Item (1)

NIKO Tiktok nakumbana na video moja inayonivutia na kunifanya nisiivuke kwenda kwenye nyingine, niitazame kwanza.

Ni video inayomuonYesha jamaa akiwa mtaani nchini Uingereza akisimamisha watu waliovaa earphone au headphone na kuwauliza wanasikiliza nyimbo gani. Video hiyo moja ikanifanya nitamani kwenda kutazama video zake zingine, na nilipoingia kwenye akaunti yake nikagundua hiyo ndiyo staili yake ya kusimamaisha watu na kuwauliza unasikiliza nyimbo gani.

Asilimia 30 ya video nilizotazama watu walioulizwa wanasikiliza nyimbo gani walitaja za Afrika. Na hapo kuna kaujumbe kakaingia akilini mwangu, ujumbe unaosema, ‘Afrika muziki wetu umefanikiwa sana.’ Nadhani ujumbe huo ulikuja kwa sababu, chaneli hiyo ni ya Uingereza, na asilimia kubwa ya watu wanaoulizwa swali ni Wazungu, kuona kwamba asilimia 30 wanasikiliza ngoma za Afrika inatoa ishara kwamba muziki wetu kama bara umekua ukilinganisha na ilivyokuwa hapo zamani.

Na sio kwao tu, ushahidi wa hilo unaonekana hata hapa nchini. Zamani ukienda klabu ngoma zinazopigwa ni za wasanii wa Marekani kina kina Chris Brown na wenzake. Lakini kama ni mtu wa kwenda klabu lini mara ya mwisho lini ulienda  ukakuta DJ amefululiza kugonga ngoma za nje ya Afrika.

Kimsingi, siku hizi unaweza kwenda klabu na hadi unaondoka usikikie ngoma hata moja ya mbele. Ukisikia ngoma ni za humu Afrika. Utawasikia wapopo A.K.A Wanaija, wasanii wa Afrika Kusini, Ghana, Tanzania, Kenya na kadhalika yaani ni humuhumu.

Na sio klabu tu hata kwenye playlist, siku hizi sio ujanja tena kuwa na playlist iliyojaa ngoma za mbele. Ukisikiliza redi, playlist za watu kwenye simu zao wengi wana bang ngoma za humuhumu Afrika. Yaani kwa kifup, sasa hivi Waafrika tumeanza kujizingatia wenyewe. Na sio sisi wenyewe tu, hata hao wasanii wa mbele wameanza kutuzingatia. Tazama jinsi wa nje ya Afrika wanavyokimbizana Afrika kuomba kolabo na wasanii wetu? Mwanzo haikuwa hivyo wasanii wetu ndiyo walikuwa wanaleta shobo na wasanii wao.

Nadhani hakuna wakati mzuri wa msanii wa Afrika kuishi na kufanya kazi kama wakati huu. Wazee wetu kina Fela Kuti, Tx Moshi William, Athuman Momba, Muhidini Gurumo wa Msondo Ngoma, pengine hawakupata nafasi kama hii mbali na kuwa na muziki mzuri. Nina uhakika, huko walipo wanajivunia sana baada ya kuona njia waliyoichonga kwa miaka mingi sasa inawafaidisha vitukuu na wajukuu zao.