TUONGEE KISHKAJI: Cheche za Super Nyota Young Killer na Super Kingereza

Muktasari:
- Albamu kama albamu haina baya, albumu ni kali, midundo imepikwa kisawasawa na mistari yake ya Kiswahili haina mpinzani! Lakini kuna sehemu zingine, ndiyo, zile alipoamua kuchana kwa Kingereza, hapo ndipo ametuchanganya.
Hapo zamani za kale wahenga walikaa chini wakatengeneza msemo unaosema, ‘Jifunze lugha ili usipotee’. Nadhani Super Nyota, Young Killer Msodoki alijifunza, lakini... alipotea bado! Hii ni baada ya kusikiliza albamu yake mpya, Super Nyota 2.
Albamu kama albamu haina baya, albumu ni kali, midundo imepikwa kisawasawa na mistari yake ya Kiswahili haina mpinzani! Lakini kuna sehemu zingine, ndiyo, zile alipoamua kuchana kwa Kingereza, hapo ndipo ametuchanganya.
Kabla hatujaendelea tuelewane; hatucheki Young Killer hajui Kingereza, hapana! Tupo hapa kujadili, sio kusimanga. Kwa nini? Kwa sababu sisi Watanzania tunaojivunia lugha yetu ya Kiswahili, ambayo ni tamu kama asali ya wanyamwenzi wa Tabora, tunajiuliza: Kwa nini msanii mwenye kipaji kikubwa kama Young Killer asivimbe na Kiswahili chake tu?
Kwa mfano, kuna mistari kwenye albamu yake mpya ambayo inakufanya ujiulize: ‘Amezungumza nini hapa?’ Hiki si Kingereza cha New York, si cha London, hata sio cha shule ya kata’, ni Kingereza cha ‘Na mimi nachana kwa kizungu’.
Ukiwauliza wasanii watakuambia kinachowakwamisha kwenda kimataifa ni lugha. Laiti kama tungekuwa tunaimba Kiingereza ngoma zetu zingeenda mbali sana. Lakini wanaijeria wanaimba sana kwa lugha za kwao na ngoma zinatembea. Asilimia kubwa ya ngoma za Sauzi zilizovuka boda hazijaimbwa kwa Kiingereza na zimebamba ile mbaya mpaka Ulaya na Marekani kwa watu wanaozungumza Kiingereza.
Mimi naamini sio kuhusu lugha, ni kuhusu muziki mzuri. Wataalamu wa muziki wenyewe wanasadiki, muziki ni lugha tosha. Mtu anaweza kucheza na kuimba ngoma ambazo hajui hata kinaongelewa nini. Si mnakumbuka tulivyokuwa tunaimba masongi ya kihindi wakati neno pekee la kihindi tulalolijua ni ‘Nehi’.
Leo hapa ukimchukua mtoto anaweza kukuimbia ‘Kuch kuch hotai’ utadhani maneno anayoimba ni ya kihindi kweli.
Kwa hiyo, tunamshangaa tu Msodoki, ikiwa tuna hazina kubwa kama Kiswahili, kwa nini tujikite kwenye lugha ambayo hatujaimaster kikamilifu? Kwa nini usipige mistari yako kwa Kiswahili tu?
Kiingereza kinaweza kuvutia, lakini Kiswahili kinashika moyo. Tunafahamu wasanii wanapenda kuchanganya lugha, wanataka kuvutia mashabiki kutoka nje ya mipaka ya Tanzania. Ni sawa, tunakuelewa. Lakini je, ni lazima kutumia Kiingereza kinachokatika kama umeme wa Tanesko? Naona huko ni kuumiza kuliko kusaidia muziki kwa sababu wakati mwingine lugha inayosikika vibaya inaweza kupunguza uzito wa ujumbe wako.
Hatutaki Young Killer asande kwenye safari yake ya muziki kwa sababu ya lugha. Tunataka afanikiwe na kubaki kuwa mmoja wa wasanii wa hip hop wanaoweza kusimama kidete, wakiwakilisha Tanzania na Kiswahili.
Kwa hiyo, Super Nyota Msodoki, tuko hapa kukushawishi ‘unapopiga mistari yako ya moto, tafadhali tu, weka Kiswahili mbele! Lugha yetu ni nyota ya kweli, na inakufanya kuwa Super Nyota wa kweli kwenye gemu ya muziki wa Tanzania.