TUONGEE KISHKAJI: Bongo Star Search ni Tunu ya Taifa

Muktasari:
- Lakini kwa sasa Bongo Star Search imevuka mipaka ya Tanzania ina washiriki kutoka nchi tatu za Afrika Mashariki — Tanzania, Kenya na Uganda.
NITAKUAMBIA kwa nini. Mara ya mwisho kuona kipindi cha TV kama Bongo Star Search (BSS) kinaanzia Tanzania kisha kinakuza mbawa zake kwenda nje ya mipaka ya TZ ni lini? Mimi hata sikumbuki.
Lakini kwa sasa Bongo Star Search imevuka mipaka ya Tanzania ina washiriki kutoka nchi tatu za Afrika Mashariki — Tanzania, Kenya na Uganda.
Hili si jambo dogo. Kwa muda mrefu tumekuwa tukishuhudia vipindi vikubwa vya burudani vya kikanda vikianzia nje ya nchi, lakini sasa kupitia Bongo Star Search tumethibitisha kwamba hata Tanzania inaweza kuwa chimbuko la vipaji vya kimataifa.
Kipindi hicho sio tu kinatengeneza mastaa wa muziki, bali pia kinatufundisha kuwa tuna uwezo wa kuanzisha kitu kikubwa kinachovutia macho ya Afrika nzima.
Kwanini nasema BSS ni tunu ya taifa kwa sababu ya mambo matatu makubwa nayokwenda kuyaongelea.
Jukwaa linaunganisha Afrika Mashariki kisanii.
Kitu cha faida kubwa kuhusu msimu huu ni kwamba washiriki hawa kutoka nchi tofauti wanashiriki warsha moja. Hii inamaanisha wanajifunza pamoja, wanashauriana na wanajenga urafiki wa kisanii unaovuka mipaka. Kesho na keshokutwa hao vijana watakuwa na mtandao mpana wa ushirikiano wa kisanii na haya yote yameanzia kwenye jukwaa letu la Bongo Star Search.
Tukiangalia historia wasanii wakubwa duniani mara nyingi huwa na safari zilizoanza kushirikiana na wenzao kutoka mataifa mbalimbali. Mfano wa Nigeria na Ghana — kwa sasa muziki wa Afrobeat unatawala dunia kwa sababu wasanii wao walianza kushirikiana na kujenga tasnia pamoja.
Tanzania, Kenya na Uganda zinaweza kufanya hivyo pia na Bongo Star Search ni hatua ya kwanza kuelekea huko. Kwa mara ya kwanza tunaona jukwaa ambalo linawaleta pamoja wasanii wa Afrika Mashariki kabla hata kuwa mastaa.
Uthibitisho kwamba mambo makubwa yanaweza kuanzia Tanzania zaidi ya kuwa shindano la kusaka vipaji, Bongo Star Search inatufundisha jambo moja muhimu - mambo makubwa yanaweza kuanzia hapa nyumbani. Tumezoea kuona mashindano makubwa yakizaliwa nje, lakini sisi wenyewe tumekuja na kitu chetu na Afrika Mashariki nzima inakitazama.
Hii ni nafasi ya Tanzania kuwa kinara wa burudani katika Afrika Mashariki na Kati. Kama tumefanikisha hili na Bongo Star Search basi kesho inaweza kuwa filamu, tamasha kubwa au hata kiwanda kizima cha burudani.
Wasanii wanaibuka, ndoto zinatimia. Tunaweza kuona kwamba washiriki wa Bongo Star Search si tu wanapigania kushinda tuzo ya mwisho, bali pia wanapambana kujenga ndoto zao. Katika misimu iliyopita tumeshuhudia vijana waliokuwa na ndoto na sauti nzuri wakigeuka kuwa mastaa wa muziki wa Bongo Flava. Phina, Asagwile, Kayumba, Kala Jeremiah na wengine. Sasa madogo wanapewa jukwaa kubwa zaidi linalovuka mipaka. Kwa hiyo tunapowashuhudia washiriki wa msimu huu wakipambana tusione tu shindano la kawaida. Tunaona ndoto zinazoanza kutimia urafiki wa kisanii unaotengenezwa na historia mpya ya burudani inayojengwa. Na yote haya yanatokea hapa Tanzania. Ukweli usemwe - Bongo Star Search ni zaidi ya shindano ni daraja la wasanii wa Afrika Mashariki.