Tunamkosea Shilole kumfananisha na JLo

Muktasari:
- Hatua hiyo imesababisha baadhi ya mashabiki kuanza kumfananisha Shilole na Jennifer Lopez, 55, staa wa filamu na muziki kutoka nchini Marekani ambaye ndoa yake ilivunjika hivi karibuni, lakini ni kosa kuwafananisha wawili hao.
MWIMBAJI wa Bongofleva, Shilole, 36, amemtambulisha mpenzi wake mpya kufuatia ndoa yake na Rajab Issa 'Rommy' iliyodumu kwa takriban miaka mitatu kuvunjika ikiwa ni ndoa ya tatu kwake kushindwa kufua dafu.
Hatua hiyo imesababisha baadhi ya mashabiki kuanza kumfananisha Shilole na Jennifer Lopez, 55, staa wa filamu na muziki kutoka nchini Marekani ambaye ndoa yake ilivunjika hivi karibuni, lakini ni kosa kuwafananisha wawili hao.
Shilole ambaye ni mama wa watoto wawili kwa mara ya kwanza aliolewa akiwa na umri wa miaka 17 katika ndoa iliyovunjika 2009, kisha akawa na uhusiano na msanii mwenzake Nuh Mziwanda ambaye Desemba 2014 alimvisha pete ya uchumba.

Baada ya kuachana na Nuh, Shilole alifunga ndoa na Ashiraf Sadick 'Uchebe' hapo Desemba 2017 kabla ya kuachana Julai 2020 kwa madai ya kupigwa. Kufika Aprili 2021 ndipo akafunga ndoa ya tatu na Rommy ambaye alikuwa mpigapicha wake.
"Mimi na aliyekuwa mwenzangu Zuwena Mohamed (Shilole) naona tumefikia mwisho na siyo vibaya nikakubali matokeo na kumpisha kijana mwenzangu aendeleze gurudumu hili na maisha yaendelee," alisema Rommy, Mei 2024 akithibitisha kuvunjika kwa ndoa yao.
Licha ya kuvunjika kwa ndoa zake tatu kisha kutangaza ya nne na kuwatambulisha hadharani wanaume wake wanne akiwa kama staa wa muziki na filamu, bado litakuwa kosa kubwa kumfananisha Shilole na Jennifer Lopez.

Ni kosa kwa sababu ndoa ya kwanza ya Lopez aliolewa akiwa na umri wa miaka 27 wakati Shilole ilikuwa miaka 17, Lopez kafunga ndoa nne ambazo tayari zimevunjika wakati Shilole ni tatu zimevunjika, pia Lopez ana historia ya kuwa na wapenzi wengi zaidi, wanane.
Lopez ambaye hivi karibuni amefika mahakamani kushughulikia talaka yake na mumewe Ben Affleck. Aliolewa kwa mara ya kwanza 1997 na Ojani Noa, lakini ndoa hiyo ilivunjika kwa talaka baada ya kudumu kwa miezi 11.
Awali Lopez alikuwa na David Cruz waliyekutana shule wakadumu hadi katikati ya miaka ya 1990, baadaye ndipo akaolewa na Ojani Noa kutokea Cuba na waliachana Januari 1998, huku mahakama ikimzuia Noa kuchapisha kitabu kuhusu ndoa yao.

Mwaka 1999 hadi 2001 Lopez akawa penzini na mtayarishaji muziki Puff Daddy au Diddy, uhusiano uliokuwa na misukosuko mingi na waliwahi kushtakiwa kwa kosa la kumiliki silaha na mali za wizi.
Katika mahojiano na Vibe 2003, Lopez alitaja usaliti kama mojawapo ya sababu ya kuachana na Diddy, baba wa watoto sita kutoka kwa wanawake wanne.
Lopez alifunga ndoa ya pili na dansa wake, Cris Judd hapo Septemba 2001 na kudumu hadi Januari 2003. Cha kushangaza kabla ya talaka na Judd kukamilishwa, Lopez akaanzisha uhusiano na mwigizaji mwenzake Ben Affleck.
Wawili hao waliocheza pamoja filamu mbili, Gigli (2003) na Jersey Girl (2004) walikuwa na uhusiano 2002 hadi 2004, kisha Lopez akawa na mwanamuziki Marc Anthony na kujaliwa mapacha, Emme na Maximilian (2008), huku wakicheza filamu inayoitwa El Cantante (2006).
Oktoba 2011 hadi Agosti 2016, Lopez akawa na uhusiano na dansa wake Casper Smart na kuachana kwao kukampa nafasi ya kuanzisha uhusiano na mcheza kikapu, Alex Rodriguez hapo Februari 2017 na walikuja kuachana Aprili 2021.
Hata hivyo, baada ya miaka 18, Lopez alirudiana na Ben Affleck hapo Julai 2021 na walichumbiana kwa mara ya pili Aprili 8, 2022 na kufunga ndoa huko Las Vegas Julai 16, 2022 ikiwa ni ya nne kwa Lopez. Je, huyo ni sawa na Shilole?
"Siogopi maneno ya watu kuambiwa naolewa sana na kuachika, ila ukweli naujua ndio maana naolewa tena hivi karibuni na mchumba wangu wa sasa ambaye watu wananiona naye," Shilole aliliambia Mwanaspoti hivi karibuni.
Shilole anajadiliwa sana upande huu kutokana na umaarufu wake. Huyu ni msanii wa pili wa kike wa Bongofleva mwenye wafuasi wengi Instagram akiwa nao milioni 10.6. Kwa ujumla ametanguliwa na Diamond Platnumz na Hamisa Mobetto.

Kwa Afrika Mashariki Shilole ni mwanamke wa tano kuwa na wafuasi wengi Instagram baada ya Zari The Bosslady (Uganda) milioni 12.1, Hamisa (Tanzania) milioni 11.8, Wema Sepetu (Tanzania) milioni 11.5 na Lupita Nyong'o (Kenya) milioni 11.3.
Na katika muziki Shilole ana lebo yake, Shishi Gang akiungana na mastaa wengine wa kike Bongo walioanzisha lebo zao awali ambao ni Shaa (SK Music), Vanessa Mdee (Mdee Music), Nandy (The African Princess Label), Hamisa Mobetto (Mobetto Music) na kadhalika.
Ikumbukwe nyimbo za mwanzo zilizompa umaarufu Shilole katika Bongofleva ni kama Nakomaa na Jiji (2013), Paka la Baa (2013) ft. Hasani Vocha, Namchukua (2013), Chuna Buzi (2014), Malele (2014), Nyang'anyang'a (2015) na Say My Name (2016) ft. Barnaba.