TUJIKUMBUSHE : Kanumba afariki, Lulu ang’ang’aniwa

Muktasari:

Kanumba alikumbwa na mauti nyumbani kwake maeneo ya Sinza Vatican, Dar es Salaam baada ya kuanguka wakati wa ugomvi na mpenzi wake, mwigizaji mwenzake, Elizaberth Michael ‘Lulu’.

ZIKIWA zimesalia siku tisa tu kabla ya marufuku ya kuzuiwa kwa shughuli za mikusanyiko ya muda wa mwezi mmoja kufikia tamati, leo tunajikumbusha tukio lililoleta simanzi na majonzi makubwa kwa wadau wa filamu za Kibongo nchini na Watanzania kwa ujumla.

Ndio, tarehe kama ya leo yaani Aprili 7, ila mwaka 2012, Watanzania waliokuwa wakijiandaa kuadhimisha kumbukumbu ya Karume Day, walipatwa na mshtuko baada ya mapema alfajiri ya siku hiyo kuenea taarifa za kifo cha ghafla cha nyota wa filamu, Steven Kanumba ‘Pioneer’.

Kanumba alikumbwa na mauti nyumbani kwake maeneo ya Sinza Vatican, Dar es Salaam baada ya kuanguka wakati wa ugomvi na mpenzi wake, mwigizaji mwenzake, Elizaberth Michael ‘Lulu’.

“Alikuwa anagombana na Lulu. Lulu akamsukuma Kanumba, akaangukia kichwa, ndio akafa, ilikuwa saa tisa usiku,” chanzo cha wakati huo kilifichua msiba huo.

Mwigizaji aliyeibuliwa na Kanumba, Patcho Mwamba naye alikiri juu ya chanzop cha kifo cha Kanumba ambaye licha ya daktari wake kujaribu kumpigania uhai wake na kuwahishwa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, ilishindana na nyota huyo kuiaga dunia.

Kanumba alizikwa kwenye makaburi ya Kinondoni, siku tatu baadaye na maelfu ya waombolezaji wakiwamo wasanii wenzake, viongozi wa kisiasa na kiserikali na watu wa mashabiki huku baadhi wakishindwa kuhimili hisia za uchungu na kuzimia.

Kifo hicho cha Kanumba kilimweka pabaya Lulu na kujikuta akishikiliwa na vyombo vya dola kabla ya kufikishwa mahakamani na kuja kuhukumiwa kifungo cha miaka miwili kwa kosa la kuua bila kukusudia Novemba, 2017.

Enzi za uhai wake, Kanumba aliyezaliwa Januari 8, 1984 mjini Shinyanga, alijijengea umaarufu mkubwa kwenye faini ya uigizaji akianzia kundi la Kaole kabla ya kuanzisha kampuni yake ya filamu iliyozalisha kazi mbalimbali zilizomtangaza anga za kimataifa.

Umaarufu wake ulijengeka zaidi baada ya kuwashirikisha wakali wa Nollywood hasa kutoka Nigeria kama Ramsey Nouah, Mercy Johnson na wengine.

Mbali na uigizaji, Kanumba alikuwa pia ni mtunzi, muimbaji muziki, mchekeshaji na muongozaji na mtayarishaji wa filamu kupitia kampuni yake ya Kanumba The Great.

Baadhi ya kazi zake ni Dar to Lagos, She is My Sister, Uncle JJ, Oprah, Sikitiko Langu, Dangerous Desire, Red Valentine, Cross My Sin, Village Pastor, Family Tears, Devil Kingdom, Big Daddy, The Shock, Moses, Because of You, Ndoa Yangu na kazi ya mwisho ikiwa ni Love&Power.