The Vikings

Muktasari:

  • Wimbo huo ulimuweka Papii Kocha na baba yake, Nguza Viking kwenye ramani ya juu kabisa kwenye muziki wa dansi nchini, lakini miaka kadhaa baadaye wakaingia hatiani kwa makosa ya ubakaji na kuhukumiwa kifungo cha maisha jela.

“NATAKA nitoke na mpenzi wangu Seyaaa…ujue Seya nakupenda sana eeeh!” imewachukua mashabiki wa muziki wa dansi miaka takribani 10 hivi kumuona mwanamuziki nyota Papii Kocha a.k.a Mtoto wa Mfalme, akiimba wimbo huo laivu.

Wimbo huo ulimuweka Papii Kocha na baba yake, Nguza Viking kwenye ramani ya juu kabisa kwenye muziki wa dansi nchini, lakini miaka kadhaa baadaye wakaingia hatiani kwa makosa ya ubakaji na kuhukumiwa kifungo cha maisha jela.

Papii na Nguza walihukumiwa kifungo cha maisha wakati wimbo huo ukitamba vilivyo kwenye anga za muziki nchini. Juzi Jumamosi kwa mara ya kwanza, Papii na Nguza walikuwa jukwaani wakiwapa burudani mashabiki wao waliokuwa wakiisubiri kwa hamu kubwa ile shoo ya Usiku wa Viking, The Vikings.

Baba na mwana hao walikaa gerezani wakitumikia adhabu hiyo kwa miaka 14 kabla ya kutoka kwa msamaha wa Rais John Magufuli.

Shoo yao hiyo iliyovuta hisia za wengi ilifanyika Ukumbi wa King Solomon, Namanga jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na mastaa wachache wakiwemo malkia wa Bongo Movie, Wema Sepetu, Husna Sajent, Shetta, Q Chilla, Mboni Masimba, Faiza Ally, Aunt Ezekiel, Jose Mara na Totoo Ze Bingwa.

Hata hivyo, shoo hiyo ilikuwa kinyume na matarajio ya wengi, kutokana na muitikio wa watu kuwa mdogo. Haijulikani kama wameamua kususia ama ni ukata ambao umewafanya watu kupunguza kula bata.

Licha ya hayo, ndani ya ukumbi, licha mashabiki kupendeza kwa kutinga pamba kali, lakini hawakuwa na uchangamfu ulitarajiwa kutokana na kuwa na shauku ya kuwaona kwa mara ya kwanza wakifanya yao jukwaani tangu walipotolewa kwenye kuta za jela.

Mambo yalianza kuchangamka pale Q Chilla alipoitwa jukwaani na Papii Kocha na kutumbuiza na ndiye aliyeibeba shoo hiyo kutokana na nyimbo zake na uchezaji wake huku mashabiki wakiachia viti na kucheza mara kwa mara.

SHOO ILIVYOANZA

Mambo yalionekana kuwa na dosari baada ya kuanza saa 6:10 usiku, kitu ambacho hakikutarajiwa. Wengi waliamini shoo hiyo ingeanza mapema ili kuwapa fursa ya kupata burudani kwa muda mrefu, hivyo baadhi kuanza kuuliza kulikoni.

Aliyefungua pazia katika shoo hiyo ni msanii Barnaba alipopanda na kuimba wimbo wake wa Mapenzi Jeneza kisha Daima milele.

Baada ya hapo akafuata swahiba wa familia hiyo na rafiki mkubwa wa Babu Seya na Papii, Bushoke na wimbo wake ‘Msela jela’ kisha akaimba na wimbo wake wa zamani unaitwa ‘Barua’.

PAPII APANDA SAA 7:00

Papii Kocha na Babu Seya walipanda jukwaani na kuanza na wimbo wao wa ‘Waambie’ na baada ya hapo wakagonga Salima, Seya na nyingine nyingi za bendi za zamani.

AMTAMBULISHA BINTIYE

Kundi la The Movick lilipanda stejini saa 7:52 usiku na baadaye Papii Kocha alirudi jukwaani na kuanza kuimba kopi za bendi mbalimbali ikiwemo bendi ya Maquiz na nyimbo ‘Kadiri Kasimba’ na ’Ngalula’, kisha akampandisha jukwaani mwanaye wa kike na kumtambulisha kwa mashabiki.

Dakika chache zilipita Papii Kocha akamuita baba yake mbele ili apige gitaa.

Saa 8:23 usiku Papii Kocha alishika kipaza sauti na kuanza kusambaza upendo kwa kuwaita wanamuziki waliohudhuria shoo hiyo, ili wapande jukwaani waimbe pamoja.

Alianza Q Chilla ambapo aliimba wimbo wake wa Nikilala naota, Mboni na Maria, akafatiwa na Shetta aliyepiga ‘Shikorobo’ na ‘Namjua’

Papii Kocha hakuishia hapo, alimpandisha jukwaani Jose Mara na kuimba wimbo wa ‘Kuachwa’wa mapacha watatu, pia akamwita Rapa maarufu Totoo Ze bingwa na kuanza kushusha masebene.

Papii Kocha alimaliza shoo kwa kuimba wimbo wa Injili uitwao ‘Hakuna Mungu kama wewe’, ambao uliwainua watu kwenye viti na kuanza kucheza.

PAPII KOCHA ABOA

Tangu mwanzo wa shoo hadi inamalizika, Papii Kocha alikuwa akilitaja jina la Wema Sepetu hadi kukazuka mino’ngono ukumbini hapo.

Hali hiyo, ilionekana kuwakera hadi wanamuziki wenzie, ambapo Q Chilla baada ya kupanda jukwaani alisema, sasa ni zamu ya (Jacquiline) Wolper kutajwa wengine wanatosha.

“Sasa ni zamu ya Wolper kutajwa, hao wengine washatajwa sana, Wolper heshima yako sana, natambua uwepo wako hapa,” alisema Q Chilla.