Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Taylor Swift na Travis Kelce wa NFL penzi moto 

Showbiz Pict

Muktasari:

  • Wawili hao walithibitisha uhusiano wao hapo Oktoba 2023 baada ya kuonekana wameshikana mikono kwenye tafrija ya Saturday Night Live na tangu wakati huo, Kelce amezungumza kuhusu Swift katika mahojiano mbalimbali.

MWIMBAJI wa Pop, Taylor Swift, 35, kwa zaidi ya mwaka mmoja sasa yupo katika uhusiano na mchezaji wa Ligi ya Soka Marekani (NFL), Travis Kelce, 35, mshindi wa Super Bowl mara tatu anayekipiga Kansas City Chiefs tangu 2013. 

Wawili hao walithibitisha uhusiano wao hapo Oktoba 2023 baada ya kuonekana wameshikana mikono kwenye tafrija ya Saturday Night Live na tangu wakati huo, Kelce amezungumza kuhusu Swift katika mahojiano mbalimbali.

Naye Swift, mshindi wa tuzo 14 za Grammy amemuimba sana Kelce katika majukwaa pamoja na albamu yake ya 11, The Tortured Poets Department (2024) ambayo tayari imefikia mauzo ya platnum mara sita.

Utakumbuka Swift ndiye msanii wa kwanza kuwa bilionea duniani kutokana na muziki pekee ambapo utajiri wake sasa unafikia Dola1.6 bilioni, alitangazwa rasmi kuwa bilionea baada ya mafanikio makubwa ya ziara yake, Taylor Swift: The Eras Tour.

SH 01

Je, ni lini na wapi wawili hawa walikutana na wanazungumziaje uhusiano wao?

Julai 8, 2023, Swift alimuona kwa mara ya kwanza Kelce katika ziara yake ya Eras iliyofanyika kwenye Uwanja wa Arrowhead ambao hutumiwa pia na Kansas City Chiefs.

Akizungumza katika podcast yake na kaka yake Jason, New Heights hapo Julai 26, 2023, Kelce alisema baada ya kumalizika onyesho hilo alijaribu kukutana na Swift ili kumuomba hata namba ya simu lakini ilishindikana.

“Nilisikitika kufuatia kujua kwamba hazungumzi kabla au baada ya maonyesho yake kwa sababu lazima ahifadhi sauti yake kwa ajili ya nyimbo 44 ambazo yeye huimba kila mara katika maonyesho yake,” alisema Kelce.

SH 02

Hata hivyo, mnamo Septemba 20, 2023 Jason akiongea na SportsRadio 94 WIP, alisema Kelce ana uhusiano na Swift, hivyo habari zilizoripotiwa na baadhi ya vyombo vya habari zina ukweli kwa asilimia 100 lakini hajui mengi kuwahusu.

“Ni vigumu kujibu yote kwa sababu sijui mengi kuhusu maisha ya mapenzi ya mdogo wangu Kelce. Ninajaribu kuweka biashara yake kama biashara yake na kujiepusha na ulimwengu huo wa udaku,” alisema na kuongeza:

“Baada ya kusema hivyo, jamani, nadhani wanafanya vizuri na yote yanayosemwa ni kweli kwa asilimia 100 na nina matumaini jambo hili litaenda mbali zaidi ingawa sijui ni nini kitachotokea huko mbele.”

SH 03

Septemba 24, 2023, Swift alihudhuria mchezo wa Kansas City Chiefs, alionekana akitazama mchezo huo kwa furaha pamoja na mama yake Donna, na baadaye alinaswa akishangilia baada ya Kelce kufunga bao.

Baada ya kumalizika mchezo huo wawili hao waliondoka pamoja huku vyanzo mbalimbali vikidai kuwa Kelce ndiye alimwalika Swift kwenye mchezo huo ili kuifurahia wikiendi yake na kudumisha penzi lao. 

Siku tatu mbele Kelce alirejea katika podcast ya New Heights, katika kipindi cha Wave Sports + Entertainment, alisema anafurahia maisha na kwa hakika wikendi ilikuwa ya moto sana na kumpongeza Swift kwa uthubutu wake wa kwenda uwanjani.

Na kwa mara ya kwanza hapo Desemba 6, 2023, Swift akazungumza kuhusu uhusiano wake na Kelce, alisema yote yalianza baada ya Kelce kumvutia sana kupitia podcast ya New Heights, hivyo kuanzia hapo aliichoka akili yake.

SH 04

“Tulianza kujumuika mara baada ya hapo, kwa hivyo tulikuwa na wakati mzuri ambao hakuna mtu aliyejua, hivyo ninashukuru kwa sababu tulifahamiana vizuri,” alisema mwimbaji huyo wa kibao, Blank Space (2014).

Pia alisema alipoonekana katika mchezo wa Kansas City Chiefs hapo Septemba 24, 2023, tayari walikuwa katika uhusiano kwa muda kidogo tofauti na wengi wanavyohisi kuwa siku hiyo ndio walifungua ukurasa huo.

“Nafikiri baadhi ya watu wanadhani kwamba tulianza kupendana na kuwa na uhusiano siku hiyo ya mchezo! Hapana, ikiwa tuna akili timamu hatuwezi kuwa na uamuzi wa namna hiyo kwa siku ya kwanza tu,” alisema Taylor Swift.

Septemba 11 mwaka huu baada ya Swift kushinda tuzo ya MTV Video Music Awards (VMAs) 2024 kupitia wimbo wake, Fortnight (2024) alimshukuru Kelce kwa kuwa na mchango katika kazi hiyo tangu mwanzo hadi kufikia mafanikio hayo.

SH 05

Alisema licha ya video hiyo kuwa ya kusikitisha sana lakini kwa kweli ilikuwa kama ya kufurahisha zaidi kipindi inafanyika kutokana na yale aliyokuwa akiyafanya Kelce wakati huo wakiiandaa.

“Kila kitu anachogusa mtu huyu kinageuka kuwa furaha na nguvu ya ajabu kwa hivyo nataka kumshukuru Kelce kwa kuongeza hilo kwenye video yetu kwa sababu nitalikumbuka hilo kila wakati,” alisema Swift, mshindi mara 30 wa MTV VMAs.

Utakumbuka uhusiano wa wawili hao ulikuja baada ya Taylor Swift kuachana na mchumba wake na muigizaji kutoka Uingereza, Joe Alwyn ambaye walikuwa pamoja kwa miaka sita.

Hata hivyo, wawili hao hawakuwahi kufunga ndoa licha ya uvumi kuwa walifanya hivyo baada ya Swift kuonekana amevaa pete katika dokumentari yake, Miss Americana iliyoruka Netflix 2020.

Ikumbukwe Swift na Alwyn walikutana kwa mara ya kwanza kwenye Met Gala 2016 na walianza kuwa pamoja miezi michache baadaye ila mwaka 2017 ndipo waliweka wazi uhusiano wao lakini kwa kipindi chote mambo yao yalitawaliwa na usiri mkubwa.

Na katika muziki, Taylor Swift, mzaliwa wa Pennsylvania, Marekani, ameuza rekodi zaidi ya milioni 200 duniani kote, ndiye mwanamuziki wa kike anayesikilizwa zaidi Spotify na ndiye mwanamuziki wa kike tajiri zaidi duniani baada ya kumpiku Rihanna.