Tamu chungu ndege binafsi ya Diamond

Muktasari:

  • CEO wa lebo ya WCB na mwimbaji wa Bongofleva, Diamond Platnumz hivi karibuni akiongea na DW Africa alithibitisha kununua ndege binafsi (private jet) kwa lengo la kile alichoita ni kuongeza thamani yake.

CEO wa lebo ya WCB na mwimbaji wa Bongofleva, Diamond Platnumz hivi karibuni akiongea na DW Africa alithibitisha kununua ndege binafsi (private jet) kwa lengo la kile alichoita ni kuongeza thamani yake.

Kama alichokisema ni kweli, staa huyo anatarajiwa kuwa msanii wa kwanza Bongo kumiliki ndege binafsi, huku akiungana na baadhi ya wasanii wa Afrika kama Davido, Cassper Nyoves, P Square, DJ Cuppy na Wizkid.

Hata hivyo, utafiti wa hivi karibuni nchini Marekani umebaini mastaa wanaomiliki ndege binafsi, wanashiriki kwa asilimia kubwa kuchafua mazingira kwa ndege zao kutoa hewa ya Carbon dioxide (CO2) kwa kufanya safari nyingi zisizo na ulazima.

Utafiti huo wa Driven Digital Marketing Agency (Yard) umeeleza ndani ya mwaka mmoja pekee staa mmoja wa Marekani kutokana na matumizi ya ndege yake anazalisha tani 3,376.64 za CO2 ambazo ni zaidi ya mara 482.37 za uzalishaji wa hewa hiyo kwa mtu anayetumia ndege za umma ambapo huzalisha tani saba tu kwa mwaka.

Diamond ambaye utajiri wake unakadiriwa ni Dola10 milioni, wastani wa Sh23.3 bilioni alisisitiza mara baada ya kununua gari la kifahari aina Rolls-Royce Cullinan mwaka jana kwa bei ya Sh2.3 bilioni, sasa ni zamu ya ndege binafsi, ambayo kwa madai yake ameshainunua.

Katika mahojiano na kipindi cha ‘The Switch’ cha Wasafi FM, Diamond alisema ananunua ndege binafsi ili kumrahisishia safari zake, maana kuna wakati anapata safari ya ghafla na kulazimika kukodisha ndege binafsi ambapo ni gharama kubwa.

Akizungumza na gazeti hili, rubani kutoka Shirika la Ndege Tanzania (ATCL), Captain Brian Wamala alisema kikubwa anachonufaika mtu anayemiliki ndege binafsi ni kupanga mwenyewe muda wake wa safari, lakini anatakiwa kujipanga zaidi kiuchumi.

“Kikubwa inakuwa ni urahisi wa safari, anakuwa hapangiwi muda, yeye mwenyewe anapanga muda wake wa safari, ni kitu kikubwa kumiliki ndege binafsi, hasa kwa mtu mwenye safari nyingi za mbali anamiliki muda wake mwenyewe.

“Mwanzoni inakuwa ngumu kwa sababu ya gharama za vibali kama leseni n.k, baada ya hapo vingine vyote ni vyepesi tu, unaweza kuingia na kutoka katika viwanja vya ndege tofauti vya hapa nchini kwa sababu hiyo ndege inakuwa imesajiliwa kwa hapa Tanzania,” alisema Captain Brian.

Kuhusu uwezekano wa kuikodisha ndege hiyo, Captain Brian alisema ni biashara inayowezekana endapo atapata leseni za kukodisha, huku akiongeza kuwa ataweza kusafiri hadi nje ya nchi, ingawa gharama zake ni kubwa!.

“Ni jambo jema, lakini ni lazima ajipange sana, maana gharama zake sio za kitoto, zipo juu kwa kila kitu, kuanzia umiliki, mafuta, malipo ya wafanyakazi utakaowaajiri, hivyo gharama zipo juu,” alisema.

Akitoa maoni yake kuhusu Diamond kumiliki ndege binafsi, mkongwe wa Bongofleva, Joseph Mbilinyi ‘Mr. II’ ‘Sugu’ ambaye ni msanii wa kwanza Bongo kumiliki gari aina ya Honda Accord Inspire baada ya kuuza albamu yake, ‘Nje ya Bongo’ (1999), alisema ni kitu kizuri kwa tasnia ila atazungumza zaidi itakapotua nchini!

“Kiukweli ni kitu kizuri, lakini maoni yangu nitatoa atakapokuja nayo, nitakupa maoni chanya, ni kitu kizuri sana lakini naomba nihifadhi maoni yangu mpaka pale itakapokamilika,” alisema Sugu.

Ikumbukwe ukiachana na wasanii, pia wacheza soka wa kulipwa Afrika, waliokwenda kukipiga Ulaya kwa mafanikio wengi wao wana ndege binafsi, wakiwamo marafiki wa Diamond, Samuel Eto’o na Didier Drogba.

Mtandao wa Driven Digital Marketing Agency (Yard), ambao ulifanya utafiti kuhusu mastaa wenye ndege binafsi wanavyozalisha COZ, iliwataja mastaa kumi wa Marekani wanaotumia zaidi usafiri wa ndege binafsi na kuchafua mazingira.

1. Taylor Swift

Hadi sasa amefanya safari 170 sawa dakika 22,923 au siku 15.9 alizotumia angani, safari zake ni kama ziara za kimuziki ambapo safari moja huchukua kuanzia dakika 80 wastani wa umbali wa maili 139.36. Hivyo kwa ujumla amezalisha tani 8,293.54 za CO2.

2. Floyd Mayweather

Bondia huyu amezalisha tani 7,076.8 za CO2 katika safari zake 177, wastani wa safari 25 kila mwezi, huku ikitajwa safari fupi zaidi ya ndege aliyowahi kuifanya ilitumia dakika 10 tu angani!

3. Jay-Z

Rapa huyu amefanya safari 136 zilizozalisha tani 6,981.3 za CO2 ambazo ni zaidi ya mara 997.3 za hewa hiyo anayotoa binadamu mmoja kwa mwaka. Safari zake hizo ni sawa ametumia wiki mbili akiwa angani, zikijumuisha za kibiashara na mambo yake binafsi huku akiwa hajafanya ziara ya kimuziki tangu 2017.

4. A-Rod

Mstaafu huyu mpira wa kikapu aliyewahi kuwa na mahusiano na Jennifer Lopez (J.LO), kazalisha tani 5,342.7 za CO2 katika safari zake 106, inakadiriwa ametumia dakika 80 kwa kila safari tangu Januari mwaka huu.

5. Blake Shelton

Mwimbaji huyo wa miondoko ya Country Music katika safari zake 111 alizofanya amezaliwa tani 4,495 za CO2, safari hizi ni sawa na dakika 12,424 akiwa angani.

6. Steven Spielberg

Director huyu wa filamu amezalisha tani 4,465 CO2 katika safari 61 ambapo safari ndefu zaidi alitumia dakika 47, katika safari zote ametumia dakika 12,341 sawa na siku tisa angani.

7. Kim Kardashian

Mwanamitindo huyu na mke wa zamani wa Kanye West, katika safari zake 47amezalisha tani 4,268.5 za CO2 sawa na mara 609.8 za hewa hiyo ambayo hutoa binadamu mmoja kwa mwaka. Safari zake ni wastani wa dakika 85.49 zinazokadiriwa kuwa na umbali wa maili 99.78, huku safari yake fupi zaidi ikichukua dakika 23 huko California.


8. Mark Wahlberg

Mwigizaji huyu amezalisha tani 3,772.85 za CO2 katika safari zake 101 ambazo ni sawa na dakika 10,428, wastaani wa siku saba akiwa angani, ikijumuisha safari za kawaida ambazo angetumia hata usafiri wa gari.

9. Oprah Winfrey

Mtangazaji huyu kwa kutumia ndege yake yenye thamani ya Dola75 milioni amezalisha tani 3,493.17 za CO2 katika safari zake 68, safari fupi zaidi aliyowahi kuifanya ilitumia dakika 14 ambayo ilizalisha tani 1 ya CO2.

10. Travis Scott

Rapa huyu ambaye ni mpenzi wa Kylie Jenner, amezalisha tani 3,033.3 za CO2, tangu Januari ametumia dakika 8,384 au siku 5.8 akiwa angani, huku umbali wa safari zake ukiwa ni maili 7.31 ambapo inaelezwa iwapo angetumia gari, basi katika safari hizo angekuwa anatumia dakika 10 pekee.