Tamasha la Sanaa na Utamaduni Zanzibar kukutanisha nchi 54

Tamasha la Sanaa na Utamaduni Zanzibar kukutanisha nchi 54

Muktasari:

  • Tamasha la Sanaa na Utamaduni lijulikano kwa jina la Festac Africa 2022 kukutanisha nchi 54 kutoka bara la Afrika  litakalofanyika Zanzibar Mei 22 hadi Mei 29.

Dar es Salaam. Tamasha la Sanaa na Utamaduni lijulikano  kwa jina la Festac Africa 2022 kukutanisha nchi 54 kutoka bara la Afrika  litakalofanyika Zanzibar, Mei 22 hadi Mei 29.

Hayo yamesemwa leo Jumatano Aprili 27, 2022 na Mkurugenzi wa Jumuiya ya Waratibu ya Waongozaji misafara ya watalii (ZATO), Hassan Ali Mzee alipozungumza na waandishi kuhusu tamasha hilo.

Mzee alisema tamasha hilo ambalo mara ya mwisho lilifanyika nchini Nigeria mwaka 1977 lina lengo la kutangaza utalii wa Zanzibar na Tanzania kwa ujumla na kuwa moja ya njia ya kuwakutanisha waafrika kusherehekea Sanaa, utamaduni na urithi wao.

"Katika tamasha hilo katika kusheherekea Sanaa na utamaduni wetu tutakuwa na shughuli mbalimbali ikiwemo maonyesho ya biashara, mavazi vyakula vya kiasili, miziki, ngonjera na michezo mbalimbali ikiwemo gofu na mpira wa ufukweni," amesema Ali Mzee.

Kutokana na hilo amewaomba wafanyabiashara mbalimbali kujitokeza kuweza kuonyesha bidhaa zao ambapo kutakuwa na mabanda katika hoteli ya Hotel Verde Zanzibar huku bidhaa zaidi ya 300 zilizotengenezwa kutoka nchi za Africa zikitarajiwa kuonyeshwa.
Mzee amesema Tanzania inatarajiwa kuwa mwenyeji wa tamasha hilo kwa miaka mitano mfululizo huku akiwataka wa Tanzania kuchangamkia fursa hiyo adhimu.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa tamasha hilo, Yinka Abioye amesema Afrika ni bara lililojaliwa rasilimali nyingi ambapo anaamini kwa kujumuika pamoja kuna biashara kubwa wanaweza kufanya wenyewe kwa wenyewe bila kutegemea mataifa ya nje.

"Kwa mfano sasa hivi dunia inapitia mambo mbalimbali ikiwemo ugonjwa wa covid  ,Afrika tunaweza kufanya biashara wenyewe na watu wetu wakapata kipato," amesema Abioye.

Wakati kuhusu historia ya tamasha hilo, amesema lilinza mwaka 1966 nchini Senegal ambapo walitakiwa kuandaa kwa miaka miwili mfululizo  lakini kutokana na sababu za kisiasa wakaishia kuandaa mara moja.