Shilole atoa neno ajali aliyoipata Kigoma
Muktasari:
- Mapema jana Januari 3, 2026, kulikuwa na taarifa kupitia mitandao ya kijamii ikieleza, Shilole amepata ajali ya gari akiwa njiani kurejea Dodoma kutoka mkoani Kigoma
MWIGIZAJI na mwimbaji wa muziki wa kizazi kipya nchini, Zuwena Mohamed 'Shilole' kwa mara ya kwanza tangu apate ajali, mjini Kigoma ametoa neno kupitia instagram yake akiposti video ya gari ambalo kinadaiwa alipata nalo ajali na kuandika ujumbe huu:
"Nimemwona Mungu kwa macho yangu. Baada ya ajali, nimesimama leo kwa neema yake. Sifa na Utukufu ni zake milele, Kila pumzi ninayovuta leo ni ushuhuda juu yake.
"Asante ni kwa jumbe zenu, Asanteni kwa simu zenu kwangu na kwa watu wangu wa karibu. Asanteni sana kwa dua zenu, Hakika Mungu ni mwema sana."
Hata hivyo, baada ya ujumbe huo, Mwanaspoti lilimtafuta Shilole kupitia simu yake ya mkononi, lakini ilikuwa ikiita bila ya kupokelewa.
Mapema jana Januari 3, 2026, kulikuwa na taarifa kupitia mitandao ya kijamii ikieleza, Shilole amepata ajali ya gari akiwa njiani kurejea Dodoma kutoka mkoani Kigoma, alikokuwa ameshiriki katika shughuli ya kijamii iliyoandaliwa na Mbunge wa Jimbo la Kigoma Mjini, Clayton Revocatus maarufu Babalevo, iliyojulikana kama Pilau Day.
Baba Levo kupitia ukurasa wake wa mitandao ya kijamii wa Instagram, alithibitisha tukio hilo akisema:
“Jana usiku dada yangu Shilole alipokuwa anatoka Kigoma kurudi Dodoma alipata ajali ya gari aina ya Alphard baada ya kugonga ng’ombe maeneo ya Maragalasi. Tunafuatilia afya yake kwa ukaribu, kwa sasa anaendelea kupata matibabu Tabora.”
Taarifa hiyo imeeleza kuwa hali ya afya ya Shilole inaendelea kufuatiliwa kwa karibu
Hata hivyo, Mwanaspoti lilimtafuta Babalevo jana kuzungumzia tukio hilo ambapo alisema, Shilole amepata ajali mbaya hivyo anahitaji maombi apone haraka.
"Ni kweli Shilole amepata ajali, anahitaji maombi apone haraka, anaendelea kupata matibabu Tabora," alisema Baba Levo, kabla ya Polisi mkoani humo leo kutoa taarifa kwamba haikuwa na taarifa za ajali hiyo, kwani haijaripotiwa kituo chochote.
Taarifa hiyo ya Polisi ikamtaba Shilole kwenda kituo cha Polisi kutoa taarifa ili hatua stahiki zichukuliwe kutokana na ajali hiyo.