Shamsa Ford akumbushia utoto wake
Muktasari:
- Akizungumza na Mwanaspoti, Shamsa alikiri licha ya kuonekana leo kama mwanamke mwenye juhudi na anayepambana kwa nguvu zote, ukweli, alipokuwa mtoto alikuwa na tabia ya uvivu uliopitiliza kiasi cha kuwapa wakati mgumu walezi wake.
MSANII wa Bongo Movie, Shamsa Ford amewashangaza wengi baada ya kufunguka kwa kina kuhusu maisha yake ya utotoni, mambo ambayo hayakuwahi kujulikana kwa urahisi, ikiwemo tabia yake ya uvivu pamoja na mbinu alizokuwa akitumia kukwepa majukumu ya nyumbani.
Akizungumza na Mwanaspoti, Shamsa alikiri licha ya kuonekana leo kama mwanamke mwenye juhudi na anayepambana kwa nguvu zote, ukweli, alipokuwa mtoto alikuwa na tabia ya uvivu uliopitiliza kiasi cha kuwapa wakati mgumu walezi wake.
“Uvivu wangu ulikuwa wa kiwango ambacho hata nikikumbuka leo najishangaa sana," alisema Shamsa na kuongeza;
"Nilikuwa sipendi kabisa kutumwa au kufanya kazi yoyote ya nyumbani, na kila nilipoona nimetumwa, nilikuwa natafuta sababu ya kukwepa, njia yangu kubwa ilikuwa ni kusingizia ugonjwa wa tumbo, nikiigiza maumivu makali ili tu nipate huruma na niachwe nisifanye kile nilichoagizwa.”
Aliendelea kufafanua hali hiyo ilimfanya mama yake kuanza kumuonea huruma kupita kiasi, bila kujua alikuwa anaigiza, hali iliyofikia hatua ya kupewa hata jina la utani kutokana na kile kilichoonekana kama kuumwa mara kwa mara bila sababu ya msingi.
Shamsa aliongeza; kadri anavyokumbuka matukio hayo sasa, anajihisi vibaya na kuona jinsi alivyokuwa akimpa wakati mgumu mzazi wake, huku akisisitiza yale yalikuwa ni makosa ya utoto ambayo yamemfundisha mengi katika maisha yake ya sasa.