Tyla arudi kivingine na albamu yake ya pili
Muktasari:
- Hiyo itakuwa albamu ya pili ya Tyla tangu atoke kimuziki mwaka 2021 na ya kwanza iliyoitwa 'Tyla' aliachia mwaka 2024 iliyofanya vizuri kwa vibao kama 'Water', 'Truth or Dare' na nyinginezo zilizompa umaarufu mkubwa.
MWANAMUZIKI kutoka Afrika Kusini, Tyla ametangaza Julai 24 mwaka huu ataachia albamu yake mpya inayokwenda kwa jina la 'APOP'.
Hiyo itakuwa albamu ya pili ya Tyla tangu atoke kimuziki mwaka 2021 na ya kwanza iliyoitwa 'Tyla' aliachia mwaka 2024 iliyofanya vizuri kwa vibao kama 'Water', 'Truth or Dare' na nyinginezo zilizompa umaarufu mkubwa.
Licha ya albamu hiyo kusubiriwa kwa hamu lakini tayari mkali huyo ameachia nyimbo tatu ambazo zitakuwa ndani ya albamu hiyo na hadi sasa zimeanza kufanya vizuri.
Ngoma hizo ni 'Chanel', 'Is It' na 'She Did It Again' aliyomshirikisha Zara Larsson hadi sasa nyimbo hizo zimefanya vizuri kwenye mtandao wa YouTube.
Akizungumzia hilo, Tyla alisema; "Albamu ya kwanza ilikuwa ya haraka sana kutokana na mambo mengi yaliyokuwa yanatokea. Lakini sasa nimepata utulivu na ninaelewa vizuri uelekeo ninaoutaka, kile ninachotaka kusema na aina ya muziki ninaotaka kuufanya."
Aliongeza ndani ya albamu hiyo ametumia mtindo wake wa kipekee alioupa jina la 'Popiano' yaani mchanganyiko wa muziki wa Pop, R&B na Amapiano ya Afrika Kusini.
"Niligundua huo ndiyo ulikuwa utambulisho wangu wa muziki. Popiano ni jina zuri na linaendana na kile ninachokifanya," alisema.
Tyla alisema mafanikio aliyoyapata kwa muda mfupi baada ya kutoa albamu yake ya kwanza mwaka 2024 yanaweza kuathiri albamu hiyo.
"Nimebadilika sana katika miezi michache iliyopita. Albamu ya kwanza ilikuwa ya kujitambulisha duniani, lakini sasa nataka kujifurahisha zaidi, kuonyesha asili yangu na kucheza na mitindo tofauti ya muziki," alisema.
Mkali huyo anayesimamiwa na lebo za Epic Records na Fax Records alianza kupata umaarufu mwaka 2023 baada ya kuachia kibao chake cha 'Water' ambacho kilitawala chati mbalimbali duniani na kumtambulisha kama moja ya nyimbo kutoka Afrika zilizofanya vizuri zaidi duniani.
Mwaka 2024 aliandika historia baada ya kushinda tuzo yake ya kwanza ya Grammy Awards katika kipengele cha Best African Music Performance kupitia wimbo wa 'Water', na kuwa mmoja wa wasanii wachache wa Afrika Kusini kufikia mafanikio hayo.
Mbali na Grammy, amewahi kushinda na kuteuliwa katika tuzo mbalimbali za kimataifa zikiwemo MTV Video Music Awards, BET Awards na Billboard Music Awards.
Sasa swali ni je albamu anayotarajia kuiachia hivi karibuni inaweza kufanya vizuri na kuvunja rekodi ya 'Tyla' ambayo ilimtangaza duniani na kumpa tuzo mbalimbali ikiwemo Grammy?