Sayuni yambeba Barnaba kibabe

Sayuni yambeba Barnaba kibabe

MSANII wa bongofleva, Barnaba Classic licha ya kuwateka mashabiki wa muziki huo, amepanua wigo wa wafuasi wa nyimbo za Injili baada ya kuachia ngoma inayokweda kwa jina la Sayuni, aliyomshirikisha Joel Lwaga.

Wimbo ya Sayuni kwa sasa umeteka mitandao ya kijamii, mashabiki mbalimbali wanajirekodi wakiimba kuonyesha hisia zao za kuguswa na ujumbe uliomo ndani ya mashairi yake, huku Barnaba akifunguka kwamba kazi yake ni kuihudumia jamii bila ubaguzi.

Barnaba anayetamba na albamu yake ya Sounds Differently, alisema msanii ni kioo cha jamii katika nyanja mbalimbali ikiwemo utunzi na uandishi wa mashairi yao, akisisitiza licha ya kujikita na nyimbo za kijamii haimaanishi hawafai kumtukuza Mungu.

“Kwenye utunzi wangu nazingatia ujumbe unaoihusu jamii ninayoipelekea muziki wangu, ndani yake kuna burudani, elimu ambayo ina mapana kama kutia moyo na kukemea vitu ambavyo haviendi sawa kwenye jamii.”

Staa huyo aliyejaliwa sauti ya kuimba laivu, aliongeza: “Kila msanii ana dini yake, sanaa ni kazi ambayo haiwezi kututenganisha na ibada, ukiachana na kumshirikisha Lwaga kwenye albamu yangu, nilifanya kolabo ya nyimbo ya wimbo wa Ambwene Mwasongwe unaoitwa Upendo wa Kweli.”

Pia alizungumzia albamu yake kwa ujumla kwamba imebeba maana kubwa ya muziki wake alioufanya ndani ya miaka 18. “Ukisikiliza wimbo mmoja baada ya mwingine utajua vitu vingi na uzoefu wangu kwenye muziki tangu nilipoanza kuufanya.”