Salamu ya Mondi ilivyogeuka dili

SUPASTAA wa Bongo Fleva, Diamond Platinumz anajua vyema kuchanga karata zake hususani pale anapotaka kuongea ama kuongelewa. Ni mtaalamu sana wa ‘timing’.

Machi 12, mwaka huu, akiwa pale Ikulu na wadau mbalimbali walioalikwa kwenye futari na Rais Samia Suluhu Hassan, Mondi alithibitisha hilo baada ya kukutana na aliyekuwa kijana wake, Harmonize kabla ya kutengana na kuanza kutupiana vijembe mitandaoni na kwenye vyombo vya habari.

Ilikuwa ni kwa mara ya kwanza wawili hao wanaotikisa muziki wa Bongo kukutana tangu mwaka 2019, walivyovunjiana mkataba ambao Mondi alimsainisha Harmonize kupitia lebo yake ya Wasafi Classic Baby (WCB) mwaka 2015.

Bila hiyana walisalimiana na kupiga soga mbili tatu sambamba na picha kadhaa ambazo baadaye waliziposti kwenye kurasa zao za mtandao wa Instagram na hiyo tayari ikawa habari ya mjini licha ya kwamba hakuna uwazi wa nini walizungumza kutokana na mambo ya pale Ikulu kubana. Lakini furaha na amani vilitawala.

Hata hivyo, salamu hiyo tu imetosha kuzua mijadala kibao nchini na kwingineko duniani kwani anapokuwa Diamond na Harmonize basi linakuwa jambo la kimataifa, kwani linapokuja suala la ‘kiki’ jamaa wanajipata.

Salamu hiyo ikaamsha kumbukumbu za ile kauli ya ‘nipe mkono tushindane’ aliyoitoa Harmo akidai aliambiwa na Mondi na ikazua mijadala mizito ikiwamo kuhusishwa na imani za giza.

Wapo wanaoamini wawili hao kwa sasa wamepatana baada ya kurushiana vijembe muda mrefu na kila mmoja kuchukua hamsini zake lakini wapo wanaoamini ni salamu ya kiungwana tu kama ilivyo jadi ya Waswahili. Ingekuwa vipi wangekunjiana roho mbele ya Rais. Ingeleta picha gani?

Hapo ndipo Diamond anapokamata vichwa vya habari na mitandao kwani mara kibao amefanya hivyo na watu ambao inadaiwa walikuwa na bifu lakini wanapokutana basi hutoa mkono na kuonyesha yuko freshi na kila mmoja na jambo hilo huwa habari kubwa.

Mwanaspoti linakushushia baadhi ya matukio yanayoendana na lile la Mondi na Konde Boy na ikawa habari.


DIAMOND VS ALIKIBA

Hawa ni washindani wakubwa kwenye muziki hapa nchini. Unaweza kusema ndio mafahali wawili kwenye gemu hii Bongofleva na kwa muda mrefu wamekuwa wakitupiana vijembe na kuonyesha kila mmoja kutokubaliana na njia za mwenzake licha ya kwamba kitambo waliwahi kuwa washikaji.

Mwaka 2018 wawili hawa walikutana kwenye msiba wa aliyekuwa mwanamitindo Agness Gerald ‘Masogange’. Wakati huo Diamond alifika na kumkuta Kiba akiwa amekaa ambapo alimfuata na kumsalimu kwa kumpa mkono. Kiba alijibu lakini bila ya kufungua mkono akibaki amekunja ngumi na Mondi akamshika na mambo mengine yakaendelea.

Jambo lile liligeuka kuwa gumzo kuliko hata msiba wenyewe na watu kuwa na mitazamo tofauti baina ya wawili hao na mkono ule kutrend kinoma.

DIAMOND VS RICH MAVOKO

Mwaka huo 2018, ilizuka sintofahamu nyingine kati ya Diamond na aliyekuwa msanii wa lebo yake ya WCB, Rich Mavoko baada ya Mavoko kudai kuna mambo ya kimkataba aliousaini mwaka 2016 hayafuatwi na kuamua kukaa pembeni.

Ilikuwa kama bifu fulani hivi na baadaye Baraza la Sanaa (BASATA), likaingilia kati kutafuta suluhisho la jambo hilo kwa kuwaita wawili hao ofisini.

Ilikuwa Agosti 2023, Mavoko na Mondi walipotinga ofisi za Basata kwa mara ya kwanza baada ya sekeseke hilo.

Mavoko ndiye alitangulia kufika ofisini hapo akiwa na wadau wake lakini baadaye Mondi naye alifika na kuwakuta kina Mavoko wamekaa chumba kimoja kisha kuwasalimia na kila mmoja kuendelea na shughuli zake.

Hiyo pia iligeuka kuwa habari ya mjini kwa wakati huo. Mwisho wa siku Mavoko na lebo ya WCB waliachana na sasa kila mmoja anapiga mishe zake kivyake vyake.

DIAMOND VS MZEE ABDUL

Sehemu nyingine ambayo Diamond aligonga vichwa vya habari ni pale alipokutana laivu na aliyetambulika kama baba yake, mzee Abdul Juma, mwaka 2019 kwenye kipindi cha Radio ya Wasafi kilichokuwa kikiitwa Block89.

Hapo Mondi alipigwa sapraizi kwa kuletewa mzee huyo ambaye kwa kipindi kile alitambulika kama baba yake mzazi lakini kabla walikuwa hawajawahi kukutana kwenye mazingira kama yale.

Mondi alipomuona mzee Abdul aliinuka na kumsalimia kisha kuendelea na kipindi na jambo hilo likatikisa mitandao kinoma noma.

Hata hivyo, baadaye mondi na mama yake, walifunguka kuwa mzee Abdul sio baba yake Diamond na kwamba baba mzazi wa msanii huyo ni Salum Idi Nyange ambaye ni baba mzazi wa mchambuzi wa soka, Ricardo Momo.