Safari ya mwisho ya mume wa Luiza Mbutu duniani
Muktasari:
- Mwili wa msanii huyo umezikwa kwenye makaburi ya Kondo, Ununio jijini Dar es Salaam, huku salamu mbalimbali zikitolewa kutoka kwa viongozi wa dini na wasanii.
MAELFU ya waombolezaji leo Desemba 29, 2025 wamejitokeza kushiriki mazishi ya mwanamuziki Faliala Mbutu ambaye ni mume wa mkurugenzi wa Bendi ya Twanga Pepeta, Luiza Mbutu.
Mwili wa msanii huyo umezikwa kwenye makaburi ya Kondo, Ununio jijini Dar es Salaam, huku salamu mbalimbali zikitolewa kutoka kwa viongozi wa dini na wasanii.
Waombolezaji walianza kumiminika nyumbani kwa Faliala eneo la Salasala kuanzia saa moja asubuhi na ilipofika saa nne mwili wa marehemu uliwasili kutoka katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.
Saa kumi na moja jioni mazishi yalifanyika katika makaburi hayo.
Faliala alifariki dunia Desemba, 25, 2025 baada ya kuugua kwa wiki moja akisumbuliwa na presha, lakini ghafla alipata tatizo la tumbo ambalo ndilo lilichukua uhai wake.
Akizungumzia kifo cha mumewe, Luiza alikaririwa na Mwanaspoti akisema: “Alikuwa anasumbuliwa na presha tu, ila akaja kuumwa tumbo ghafla likavimba, tukampeleka Hospitali ya Muhimbili akafanyiwa vipimo akakutwa na tatizo la mrija wa kupitisha chakula umevimba ikabidi (madaktari) wamfanyie upasuaji wakapunguza utumbo kisha wakaunganisha tena, sasa akawa anaendelea na matibabu ndiyo amefariki jioni hii."
Faliala mwenye asilli ya Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo enzi za uhai wake aliwahi kuwa mwanamuziki wa bendi ya Kilimanjaro Connection iliyokuwa ikiongonzwa na Kanku Kelly, lakini hadi umauti unamkuta alikuwa mpiga gitaa la besi na mmiliki wa bendi ya The Buffalo ambayo ilikuwa inapiga muziki katika hoteli.
Luiza na Fariala walifunga ndoa mwanzoni mwa miaka ya 2000 na kufanikiwa kupata mtoto mmoja wa kiume anayeitwa Bryan.