Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Rommy3D afichua nyuma ya talaka yake kwa Shilole

SHILOLE Pict

Muktasari:

  • Aprili 22, 2021, Shilole alifunga ndoa na Rommy3D ambapo walidumu kwa takribani miaka mitatu hadi Mei 28, 2024 ilipotoka taarifa ya kuachana kwao ambapo hivi sasa kila mmoja anaendelea na maisha yake.

MMOJA wa wapigapicha maarufu kwa sasa ni Rommy3D. Ukizitazama picha zake na ubora wake, hautajiuliza mara mbili kwa nini kapewa jina la 3D.

Majina yake kamili ni Rajab Issa na katika safari yake ya maisha iliyojaa misukosuko ya kibiashara, maumivu ya mapenzi na ndoa na maisha mapya aliyonayo sasa.

Katika mahojiano na Mwanaspoti, Rommy3D anafunguka mambo mengi hasa ndoa yake na msanii Zuena Mohamed ‘Shilole’ tangu wafunge ndoa  Aprili 22, 2021 na hadi walipoachana Mei 28, 2024 na namna talaka aliyoitoa ilivyozua gumzo mitandaoni na namna hapa anafichua kila kitu.

Rommy3D afichua ishu ya talaka, ataja kilichowakutanisha na Shilole


PICHA ZILIWAKUTANISHA

Rommy3D anasema katika harakati zake za kujitafuta kwa masuala ya kupiga picha za mastaa mbalimbali akiwamo Aunt Ezekiel aliyemwomba awe mpigapicha wake, ndipo alikutana na Shilole na kuanza uhusiano.

“Aunt Ezekiel alikuwa na mpiga picha wake, kwa kuwa nilikuwa karibu na Aunt na tulizoea kumuita mama, akanambia kwa nini nisimpige picha wakati mimi naweza kushika kamera,” anasema na kuongeza;

“Akasema nimpige picha na picha ya kwanza ilikuwa ile ya sabuni zake za murua, tangu hapo nikawa mpiga picha wake rasmi na akanifungulia studio, na akawa ananitafutia tenda za kupiga picha kwenye maharusi na wasanii,” anasema.

“Nikawa nakutana na wasanii wengi kina Hamisa Mobetto, Elizabeth Michael ‘Lulu’, Dude wasanii wengi sana, jina langu likaanza kusikika kwa kupiga picha bora kabla hata watu hawajaijua sura yangu, huyo Shilole mwenyewe amenifahamu kutokana na kazi hii,” anasema.

SHILO 09

ISHU YA TALAKA MTANDAONI

Anasema sababu za kuweka talaka mtandaoni ilikuwa ni makusudi ili kila mtu aone na hakuwa na mpango wa kurudiana naye tena.

“Niliamua kuposti ili nipigilie msumari, sikutaka ndugu wala marafiki waanze kuniletea mazungumzo ya kunirudisha kwenye ndoa.”

SHIL 02

KISA SHILOLE, APATA PIGO

Anasema moja ya vipindi vigumu alivyowahi kupitia ni baada ya kuachana na Shilole.

“Kuachana na Shilole sikutarajia kabisa, kilikuwa kama bomu,” anasema na kuongeza; baada ya kuachana naye alipata pigo ambalo lilimsababishia maumivu baada ya mali zake kuharibika kutokana na mvua.

“Studio yangu ya Kinondoni aliingia maji kupitia chooni, laptops, kamera na meza vikaharibika. Nilijikuta nimepoteza kila kitu kwa wakati mmoja,” anasema.

SHIL 01

KUMBE ILIKUWA NDOA YA TATU, AOPOA MWINGINE

Anasema wengi hawajui ameoa mara tatu na ya mwisho ndiyo aliyokuwa na Shilole kabla ya kuachana na kwa sasa ana penzi jipya na mtoto wa Kariakoo.

Anasema mwaka 2014 alioa mwanamke wa Kiishombe na kudumu naye hadi 2018, akaoa tena mwaka 2018 na kuachana naye 2021, kabla ya kumuoa Shilole mwaka 2021 na kuachana rasmi 2024.


KWA MTOTO WA KARIAKOO NDO KAFIKA

“Kwa sasa nipo kwenye mahusiano na mwanamke kutoka Kariakoo, ambaye hapendi mitandao ya kijamii,” anasema na kuongeza;

“Safari hii nimeamua kuwa na mwanamke wa kawaida ambaye nimemzidi kipato. Wake zangu waliopita walikuwa na pesa kuliko mimi, hivyo kukawa na changamoto kubwa ndani ya nyumba,” anasema.

“Nataka utulivu na naamini, huyu atanipa amani na nimeona naweza kudumu naye,” anasema na kuongeza ana mpango wa kufunga naye ndoa kabla mwaka haujaisha.

SHILO 08

BADO ANAONGEA NA SHILOLE

Pamoja na kuachana, anasema hana ugomvi na Shilole na akiwa na shida ambayo anaona anaweza msaidia anampigia simu na kusaidiwa.

Anaeleza bado wanawasiliana inapobidi, akitolea mfano kuna tukio ambalo lilitokea baada ya kupeana talaka na aliposhikiliwa na polisi msanii huyo alimsaidia.

SHILO 03

KWA NINI Rommy3D

Anafunguka alikolitoa jina hilo huku akimtaja kaka yake, Peti Farasi  ndiye aliyempa kutokana na kazi hiyo ya kupiga picha.

Anasema alipewa jina hilo tangu akiwa shule na alianza kwa kujiita Rommy kabla ya 3D kuongezwa na kaka yake, Farasi.

“Hili jina limetokana na mimi nilikuwa najiita Rommy, ila 3D amenipa kaka yangu Farasi,” anasema na kuongeza, alijiita hivyo kutokana na wasanii Lil Romeo na DJ Romy Jones na anawakubali sana.

“Kwa sababu kipindi hicho teknolojia ya 3D ilikuwa ndiyo imeshika kasi, ndipo nikaitwa Rommy3D,” anasema.

SHILO 05

ALIANZA KUBEBA TAA, SASA ANAJITAFUTA MWENYEWE

“Nilianza kama ‘light man’ nabeba taa kwenye kampuni ya kaka yangu inaitwa Farasi, nilikuwa pia nashika boom,” anasema na kuongeza hatua kwa hatua alianza kuaminiwa zaidi hadi kuanza kushika kamera.

“Akawa ananiachia kamera akienda kushuti movie maana alikuwa pia mtu wa kuandaa kazi hizo,” anasema.

“Hapo ndipo nilipoanza kujua vitu vingi maana nilikuwa najifunza kushika kamera, kupiga picha, kuhariri na mambo mengine mengi juu ya picha,” anasema na kuongeza kutokana na kampuni hiyo ya kaka yake ‘Farasi’ alijenga mtandao mkubwa wa watu, hatua iliyompa ujasiri wa kufungua yake mwenyewe.

SHILO 07

AANZA NA FILAMU

Anasema akiwa na rafiki yake Prince HDV walipata nafasi ya kufanya kazi ya filamu mwaka 2014 na kazi ya kwanza waliyoshuti iliitwa ‘Mdau’ mwaka 2014 na ilifanya vizuri na ndipo wakatoka rasmi.

Hata hivyo, anasema baada ya hapo soko la filamu lilianza kushuka na kumlazimu kubadili mwelekeo.

“Baada ya hapo movie zikaanza kushuka, haya mabadiliko ndiyo yakanifanya akili yangu ihame na kuanza kupiga picha ‘photo shoot’,” anasema na kuo ngeza kazi hiyo alifundishwa na kaka yake Farasi, Hank pamoja na BMC Photography aliyemfundisha pia kuhariri ‘editing’ na Aunt Ezekiel ndiye aliyemnunulia kamera yake ya kwanza na kumfungulia studio Kinondoni.

SHILO 10

BIASHARA INALIPA?

Anasema kwa sasa angalau kazi hiyo inalipa tofauti na zamani na haikuwa na thamani.

“Zamani picha ilikuwa Sh5000 tu, lakini sasa tunafanya kwa package, unaweza kupiga picha tano kwa laki moja,” anasema na kuongeza hata video fupi za mitandaoni zimepanda thamani.

“Video za ‘Highlights’ za Instagram zinaweza kufika hadi Sh3 milioni hadi 4 milioni kutokana na gharama za vifaa na uendeshaji,” anasema na kuongeza nje ya kazi hiyo anapenda kukaa kijiweni na marafiki zake kusikiliza stori na kukaa na watoto wake wawili, Samira na Raika na kusisitiza anawapenda sana. Pia anapenda sana kula pilau.

SHILO 02

SHABIKI WA YANGA

Anasema ni shabiki wa Yanga SC na nyota wa timu hiyo anayemkubali ni Salum Abubakar ‘Sure Boy’, Ibrahim Hamad ‘Bacca’ na kipa Djigui Diarra, huku upande wa Simba SC akiwakubali Shomari Kapombe, Libase Gueye na Enock Inonga ambaye kwa sasa hayuko na timu hiyo.


KIBA, MONDI WANAJUA, HARMONIZE KAMA YEYE

“Namkubali sana Alikiba kwa nyimbo zake za zamani kama Cinderella na Nakshi Nakshi,” anasema.

Anaongeza pia anasikiliza nyimbo za zamani za Diamond, huku kwa sasa akimkubali Kusah kutokana na uwezo wake wa kuandika mashairi.

Pia anasema anamkubali Harmonize kwa sababu pia ana jina kama lake ‘Rajab’ na anapenda mfanano huo .

“Mimi na Harmonize wote ni Rajab na hata vitu tunavyopenda vinafanana sana,” anasema Rommy3D huku akicheka.