Roma aukana wimbo wa ‘Mama Leta Suluhu’

Muktasari:

Wimbo huo ulioanza kusikika kwenye mitandao ya kijamii siku tatu zilizopita, unataja mambo kumi ambayo msanii huyo angetaka Rais Samia Suluhu Hassan, kuyafanyia kazi katika uongozi wake.

Msanii wa muziki wa Hip Hop, Roma Mkatoliki ameukana wimbo wa ‘Mama Leta Suluhu’.

Wimbo huo ulioanza kusikika kwenye mitandao ya kijamii siku tatu zilizopita, unataja mambo kumi ambayo msanii huyo angetaka Rais Samia Suluhu Hassan, kuyafanyia kazi katika uongozi wake.

Katika wimbo huo picha iliyotumika na jina ni la Roma, lakini mwenyewe leo Jumapili Aprili 4, 2021, kupitia ukurasa wake kwenye mtandao wa Instagram amekanusha kuwa hausiki nao.

Roma ameandika” Ninaulizwa sana hili swali. Kuna wimbo uko youtube una cover ya picha hiyo hapo juu (akaonyesha picha yake), kuwa ni wa kwangu!!

“Majibu.Huo wimbo sio wangu,wala hiyo inayosikika siyo sauti yangu, na sijashiriki kwa chochote kwenye wimbo huo!!Wimbo wangu wa mwisho kutoa ulikuwa ‘Diaspora ‘ulitoka mwaka December 9, 2020.

Katika wimbo huo,msanii amezungumzia mambo kumi ambayo angependa kuona Rais Samia akiyaletea suluhu na kati yake ni pamoja na kuviacha vyombo vya habari kuwa huru, kuwepo tume huru ya uchaguzi na kutaka kujua msimamo katika kupanda na corona ambapo anahoji watu waendelee kupiga nyungu au kupiga maombi.

Jingine msanii huyo aliloliongelea ni mchakato wa katiba mpya, kurudisha bunge live na kuondoa kinga kwa Rais kutoshtakiwa.

Vilevile msanii huyo aligusia suala la wakina Halima Mdee kuwepo bungeni,kuwa wapo kupitia  chama gani, viongozi kuonyesha mfano wa kijikinga na corona kwa kuvaa barakoa kama anavyofanya Rais Mstaafu wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete.

Aidha aligusia suala la wanafunzi wanaopata mimba kuruhusiwa kuendelea na shule na kujua kuhusu uchunguzi wa tukio la Makamu Mwenyeti Taifa wa Chama cha Demokrasia (Chadema) Bara, Tundu Lissu ilipofikia baada ya kupigwa risasi akiwa mjini Dodoma ambapo wakati huo alikuwa Mbunge wa  Singida Mashariki.