Rihanna amjenga moyo shabiki mwenye saratani
Muktasari:
- Video iliyosambaa mitandaoni inamuonyesha shabiki huyo ambaye alikuwa katika duka la bidhaa nchini Marekani akimuomba Rihanna kupiga naye picha lakini kama alikuwa na wasiwasi fulani.
MWANAMUZIKI maarufu duniani, Rihanna ameendelea kugusa mioyo ya mashabiki wake baada ya kumfariji mwanamke anayepambana na saratani aliyekuwa akihofia muonekano wake.
Video iliyosambaa mitandaoni inamuonyesha shabiki huyo ambaye alikuwa katika duka la bidhaa nchini Marekani akimuomba Rihanna kupiga naye picha lakini kama alikuwa na wasiwasi fulani.
Wakati Rihanna akikubali ombi la kupiga picha naye alijisemea kuwa anaishi na saratani na anahisi hana muonekano mzuri.
Rihanna alionekana kutofurahishwa na kauli ya shabiki huyo na kumueleza kuwa ajiamini kwa kuwa ni mzuri wa asili.
Baadaye wawili hao waligundua kuwa wote wanatumia jina la kwanza Robyn, jambo lililoongeza furaha katika mazungumzo yao.
Shabiki huyo alimwonyesha Rihanna picha aliyokuwa nayo kwenye simu akiwa amevaa wigi, lakini msanii huyo alimhimiza ajiamini na kujivunia mwonekano wake wa asili.
“Napenda kuona mstari mzuri wa nywele. Hivi ndivyo ninavyopenda kuona usijidharau tena unapokutana na watu, wewe ni mrembo ulivyo,” amesema Rihanna.