Rayvanny asepa na kijiji maadhimisho ya Ukimwi duniani

Rayvanny asepa na kijiji maadhimisho ya Ukimwi duniani

Muktasari:

  • Msanii  Rayvan alikusanya kijiji wakati akitoa burudani kwenye kilele cha maadhimisho ya kitaifa ya siku ya Ukimwi duniani Mkoani Mbeya.

Mbeya. Msanii wa bongofleva kutoka WCB, Ryamond Mwakyusa 'Rayvanny'  leo amekuwa kivutio katika kilele cha maadhimisho ya kitaifa siku ya Ukimwi duniani yanayofanyika mkoani Mbeya.

Maadhimisho hayo yanafanyika katika viwanja vya Ruanda  zovywe jijini hapa ambapo Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ndiye mgeni rasmi akimwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan.

Rayvanny alionekana kuwateka wananchi waliojitokeza katika maadhimisho hayo kwa nyimbo kadhaa baada ya kutambulishwa na mshereheshaji wa tukio hiyo, Shaban Kisu.

Msanii huyo alianza kutoa ngoma ya 'Amaboko' aliyomshirikisha Diamond Platinum kabla ya kushuka na kuchangamana na wananchi kwa burudani tofauti.

Hali hiyo iliwafanya wananchi kumzingira wakitaka kupiga naye picha wengine wakirekodi anachofanya jukwaani kisha kuelekezwa kuwafikia wananchi wote viwanjani hapo.

Msanii huyo mzaliwa wa mkoani hapa kabla ya kumaliza shoo yake alimuomba Waziri Mkuu, Majaliwa kumshika mkono kwa niaba ya wana Mbeya ambapo kiongozi huyo alikubali na kumkaribisha meza kuu.

Rayvanny aliyekuwa na ulinzi wake wa takribani watu sita, walimsindikiza meza kuu ambapo Waziri alimpatia bahasha ambapo haikujulikana kilichomo ndani alionyesha ishara ya kushukuru kisha akapokea.