Rais Mwinyi akutana na muigizaji Sanjay Dutt wa India

Tuesday November 09 2021
Dutt PIC
By Jesse Mikofu

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Hussein Mwinyi amesema ujio na nia ya muigizaji nyota wa filamu za Kihindi, Sanjay Dutt visiwani humo ni fursa nzuri ya kuutangaza utalii wa Zanzibar.

Ametoa kauli hiyo leo Jumanne Novemba 9, 2021 alipokutana na kufanya mazungumo na muigizaji huyo Ikulu Zanzibar.

Dk Mwinyi amesema Serikali itampa ushirikiano wote kuhakikisha azma yake hiyo inafanikiwa na mipango yote aliyoipanga kuwekeza Zanzibar.

Mbali na kuwekeza katika sekta ya filamu, pia Dutt anataka kuwekeza katika sekta ya utalii, afya, miundombinu, sanaa na kutoa huduma kwa Jamii hasa kwa wale wanaoishi katika mazingira magumu.

“Ujio wake ni muhimu kuutangaza utalii wa Zanzibar pamoja na vivutio tulivyonavyo,” amesema

Dk Mwinyi amemueleza nyota huyo jinsi Serikali ya awamu ya Nane ilivyodhamiria kukifanya kisiwa cha Pemba kuwa ni sehemu maalum ya uwekezaji na mikakati ya kuhakikisha hilo linatekelezwa baada ya muigizaji huyo kueleza alivyovutiwa na mazingira ya kisiwa hicho.

Advertisement

Naye Dutt ameeleza nia yake ya kuanzisha kampuni yake hapa Zanzibar ambayo itasaidia kuimarisha tasnia ya filamu na kuitangaza Zanzibar katika uga wa kimataifa.

Amesema kuanzisha kampuni ya filamu Zanzibar itaifanya kuwa sehemu mojawapo ya kuigizia filamu zake kupitia kampuni hiyo.

Naye Waziri Utalii na Mambo ya Kale, Leila Muhamed Mussa amesema Wizara yake imevutiwa na utayari wa nyota huyo wa kuitangaza Zanzibar hasa ikizingatiwa hivi sasa Zanzibar inajikita kutafuta soko la utalii katika Bara la Asia.

Sanjay Dutt ambaye ni muigizaji nguli wa Filamu za Bollywood, ameigiza zaidi ya filamu 80 ukiachilia mbali zile alizoalikwa ambapo alionekana kwenye ulimwengu wa filamu kupitia filamu yake ya ‘Rocky’ ambayo iliongozwa na marehemu baba yake Sunil Dutt mwaka 1981.

Advertisement