Meneja Chopa apigilia msumari ishu ya Diamond, Harmonize

Muktasari:

  • Sasa meneja huyo kaingilia kati na ameliambia Mwanaspoti kauli hizo za Diamond amezisikia kupitia mitandao ya kijamii kwenye shoo yake aliyofanya hivi karibuni kwenye viwanja vya posta na kusema imekuwa kama ni msimango.

INAKERA. Ndivyo anavyoanza kusema meneja wa msanii wa Bongo Fleva, Harmonize, Rajabu Mchopa 'Chopa' akikazia kauli ya msanii wake huyo aliyedai amechoshwa na kila mara Diamond Platnumz anapopanda stejini kusema amemtoa kimuziki.

Sasa meneja huyo kaingilia kati na ameliambia Mwanaspoti kauli hizo za Diamond amezisikia kupitia mitandao ya kijamii kwenye shoo yake aliyofanya hivi karibuni kwenye viwanja vya posta na kusema imekuwa kama ni msimango.

“Sio tu Hamornize, hata mimi sifurahishwi na hiyo kauli ya mara kwa mara kusema umemtoa Hamornize. Hata kama ni kweli umemtoa mtu kimuziki sasa isiwe sababu ya kila wakati ukijisikia tu kuongea katikati ya shoo yako unaongea tu, kuwa, hii ni kama masimango mtu hapumui kabisa. Mimi nashauri wangeendelea tu kufanya muziki haya mambo hakuna mtu asiyeyafahamu na uzuri hata Hamornize mwenyewe alishawahi kusema na kushukuru hadharani sasa isiwe ni fimbo,” alisema Chopa.

Aprili 27, 2024 Diamond alikuwa na shoo kwenye viwanja vya Posta iliyohudhuriwa na wasanii wengine ambao wengine walitumbuiza.

Baada ya Mondi kupanda na kutumbuiza katikati ya shoo alisema daima Harmonize na Rayvanny watasalia kuwa wanawe na atazidi kujivunia mafanikio yao kimuziki, kwani bila yeye, pengine hasingejulikana kimuziki.

Itakumbukwa Harmonize alikuwa msanii wa kwanza kabisa kusainiwa katika lebo ya Wasafi Classic Baby (WCB) ilipozinduliwa 2015, kabla ya ujio wa akaja Rayvanny na wasanii wengine kama Lava Lava, Queen Darleen na baadae Mbosso na Zuchu na mwaka jana akamalizia kwa Dvoice.

Baada ya Diamond kusema hivyo, tamko hio lilionekana kutomfurahisha Harmonize ambaye anakerwa na kauli za kusema kila mara alimsaidia.

Harmonize alimjibu Diamond akimwambia anakaribia kujuta kukubali msaada wake kimuziki, pia akamwambia aache kujivunia mafanikio yake kwani alishamlipa hela za kuvunja mkataba.

“Mshindi ni wewe kaka uliyenitoa. Tena najilaumu kwa nini nilijibu wakati bado ni haki yako kujivunia. Ni vile umejivunia sana hadi inachosha na huwa unajivunia pale unapotaka huruma ya watu. Ila kisirisiri huku ukiwaambia waandaaji wa shoo hasa za nje nikiwepo mimi Konde Boy huwezi kufanya maana tutaonekana tupo kiwango sawa."

Kwa kumjibu, Diamond alionekana kukubali akisema na hakuwa anajua Harmonize alikuwa amejitayarisha kwa malumbano.

Diamond alimwambia Harmonize ameshinda katika vita hiyo ya maneno akijitaja kama mnyonge ambaye hawezi tena kuendelea kubiashana.

“Oooh, kumbe una dhamira ya kubishana. Mimi ni mnyonge siwezi kubishana na wewe mtu mzito. Mataji yote nakupa chukua ushindi,” Diamond alisema.

Ikumbukwe Machi 12,2024 Diamond na Hamornize walionekana kwenye picha ya pamoja wakiwa Ikulu kenye mwaliko wa Iftari. Picha hiyo ilizungumzwa na watu wengi sana na kudai wawili hao kama walikuwa na bifu kama wanavyodaiwa basi litakuwa limeisha.