Ni mfumo au Nandy, Zuchu wanataka?

Muktasari:
- Lady Jaydee mwenye miaka zaidi ya 25 katika Bongofleva anaingilia kati na kusema sio vizuri kuwashindanisha wasanii kwa kuwa kila mmoja ana nafasi yake ya kufanya vizuri kwenye muziki na kujitengenezea himaya wake.
MWANZONI walidai kuwa Zuchu anatengenezwa ili kumshusha Nandy kimuziki, lakini miaka kadhaa nyuma ni watu haohao waliosema Nandy anatengenezwa ili kumshusha Ruby aliyeibuliwa na Tanzania House of Talent (THT).
Lady Jaydee mwenye miaka zaidi ya 25 katika Bongofleva anaingilia kati na kusema sio vizuri kuwashindanisha wasanii kwa kuwa kila mmoja ana nafasi yake ya kufanya vizuri kwenye muziki na kujitengenezea himaya wake.
Anasisitiza hasa ukizingatia kuwa wasanii wa kike ni wachache katika muziki, hivyo haipaswi kuwagawa kwa mtindo huo wa kuamini ili huyu apande juu, basi lazima aliye juu yake ashuke kumpisha.
Nakubaliana na Lady Jaydee kwa sababu alishakumbana na hilo pale Linah alipofanya vizuri na watu haohao wakaibuka na kudai Linah anaandaliwa kuchukua nafasi ya Jide katika Bongofleva.
Namuona Jide mwenye hekima sana, Profesa Jay hakukosea kumpachika a.k.a ya Dada Mkuu wa Bongofleva. Kiukweli anastahili heshima hiyo, lakini pengine kuna baadhi ya wasanii wanapenda jambo hilo hasa wanapokuwa wanapanda.
Juni 2017, Nandy alidai kuwa yeye ndiye msanii wa kike namba moja Tanzania kitu kilichoibua mjadala mkali mitandaoni wakati mashabiki wengi walihoji inawezekanaje msanii aliyefanya vizuri miaka miwili tu kuwa namba moja. Wakati Nandy, mshindi wa TMA mara nne anatoa tambo hizo alikuwa ameshatoa nyimbo kama Nagusagusa (2016), One Day (2016), Wasikudanganye (2017), Kivuruge (2017) na Ninogeshe (2017) ambazo zilifanya vizuri.
Nandy alisema fedha zinaongea katika muziki wake kwani wakati huo ndiye aliyekuwa msanii wa kike ambaye video zake zilikuwa zinatazamwa sana YouTube na ndiye mwenye wafuasi wengi kwenye mtandao huo. Licha ya tambo hizo alikiri kuwa kuna ambao wamemtangulia kimuziki na anawaheshimu, lakini watu watazame zaidi wakati uliopo na sio historia.
Hii ni 2025, Zuchu anaonekana kufikia hilo alilotamba nalo Nandy - kwa hiyo tumtaje Zuchu kama msanii namba moja wa kike Tanzania kwa sasa au tuseme tayari amefanikiwa kuchukua nafasi ya Nandy katika Bongofleva maana meza imepinduka?
Nafikiri Nandy alipaswa kuwa mtulivu na kufurahia kilele cha mafanikio yake. Nazungumzia utulivu kama alionao Ray C kwa sasa licha ya kipindi cha nyuma naye kusemekana kaletewa mshindani katika muziki. Ikumbukwe baada ya Recho wa THT kutamba na wimbo wake Kizunguzungu (2011) ikaanza kusemwa anamuinga Ray C kwa kila kitu. Baadhi ya watu wakaenda mbali zaidi na kudai anatengenezwa kumshusha Ray C kimuziki.
Hata hivyo, shukrani muda ambao umekuja kukata mzizi wa fitna kila kitu kipo wazi na figisu hizo zimekoma. Nampenda Lady Jaydee kwa kuwa anaelewa jinsi huu mchezo unavyokwenda na mwisho wake utakavyokuwa.
Lady Jaydee anasema haoni wivu kwa wasanii wapya wa kike kuja na kuonekana kufanya vizuri na wengine kutajwa au kujitaja kuwa namba moja kwa kuwa naye alikuwepo hapo kwa muda mrefu na kila shabiki anajua hilo. Lakini TID kwa upande wake hataki watu wa kumsemea, anadai kuwa nafasi yake kwenye muziki ilichukuliwa na Diamond Platnumz baada ya yeye kugombana kituo cha redio chenye nguvu kubwa ya ushawishi nchini.
TID anadai redio hiyo ina uwezo wa kumshusha msanii na kumpandisha mwingine inayemtaka. Kama anachosema ndio uhalisia wa mambo, basi bado kuna safari ndefu huko mbeleni.
Hoja hiyo inaungwa mkono na One The Incredible ambaye anasema wamiliki wa vyombo vya habari ndio wawekezaji wakubwa kwenye kiwanda cha muziki Bongo, hivyo wanaweza kutoa fursa kwa msanii yeyote wampendaye kwa maslahi mapana ya biashara yao, na hapo msanii huyo atakuwa juu kimuziki vyovyote vile.